MC-MKONGWE : Ukatili umeshamiri miongoni mwa jamii

Sunday May 29 2016Mackie Mdachi

Mackie Mdachi 

Najua kuwa Jeshi la Polisi na hata baadhi ya viongozi wengine hasa wa kitaifa na waitwao wanasiasa watalipinga tamko hili na hata kutaka kutoa uthibitisha kwa kutoa taarifa za kiofisi, ama hesabu za matukio yaliyoripotiwa kwao, yaani kwa vyombo vya usalama.

Iwe iwavyo, hali ya kutisha na kusikitisha imezagaa maeneo mengi ya vijijini na hata mijini hali inayoizingira amani kuwa shakani. Jambo usilolijua, wahenga wanasema ni ‘usiku wa giza’. Amani yetu wanajamii iko katika hali-tete. Vibaka, ujambazi, ‘Panya Road’, mauaji kutokana na wivu wa mapenzi na mateso ya kijamii.

Mauaji ya albino

Hili siyo tukio geni au jipya kulisikia, bali ni moja ya matukio endelevu ambayo yamekuwa yakitokea miaka kadhaa kwenye mikoa ya Shinyanga, Tabora na Mwanza hadi kutoa ‘mbiu’ ya kutisha nchini kote na kujulikana ulimwenguni, kiasi cha kulitia doa taifa letu. Inatisha.

Nakumbuka mwaka 2014 nikiwa kwenye mji wa Ahmedabad huko India, mara kwa mara nilipokwenda kwenye maeneo yenye mkusanyiko wa watu wengi au kwenye ‘mihanjo’ yangu ya kijamii, wananchi wengi wenyeji yaani ‘Wahindi’, walikuwa wakiniangalia kwa kunistaajabia na kuniuliza “Tanzania, killing albino, you kill too?’. Yaani Mtanzania mnaua maalbino na wewe unawaua pia?’. Niliwakatalia kwa nguvu zote kuwa matukio hayo hayatokei kila mara, bali ni watu wachache wakatili na wala hayakubaliki nchini kwetu. Swali hilo lilinihuzunisha na kunifedhehesha.

Nakumbuka pia, juu ya juhudi zinazosemekana zimefanywa na Serikali kuzuia ukatili huo, lakini bado mambo yako vile-vile. Pia, nakumbuka kampeni kubwa iliyofanywa kwa kaulimbiu isemayo ‘Imetosha’ kuwaua maalbino, ikiongozwa na Henry Mdimu, mwandishi wa habari ambaye pia ni albino.

Rais mstaafu Jakaya Kikwete alionana na Chama cha Maalbino Tanzania pale Ikulu kwa kuipokea kaulimbiu hiyo ya ‘Imetosha’ na kuwaahidi kuwasaidia ipasavyo ili kupunguza au kuondoa kabisa ukatili huo wa mauaji yasiyostahiki. Lakini niwe muwazi, bado mauaji kwao yanaendelea.

Ubakaji

Hali ni mbaya, kila uchwao tunasikia na hata kushuhudia aina zote za ukatili kwa wanajamii wenzetu hasa wasichana, hata vipigo na mauaji kwa baadhi ya wakina mama kutokana na kadhia tofauti zinazoweza kabisa kuepukika ama kuzuilika. Ukatili umeshamiri.

Ubakaji vijana wadogo niseme watoto wadogo mno na wasichana, tena kwa kuwaingilia kinyume na maumbile hatimaye kuwaua. Tembea vijijini usikie yanayojiri na kutisha. Baadhi ya vijiji hawaruhusu wasichana wao kwenda kutafuta kuni au maji, kwani vyote hupatikana mbali na siyo salama kwa wanajamii hao.

Jambo la kusikitisha zaidi ni kuwa wanaohusishwa na ukatili huo siyo vijana wadogo, bali ni watu wazima tena wengine ni wanao aminika ndani ya jamii.

Tunasoma kwenye baadhi ya magazeti habari au kesi zao wengine wakipewa ‘dhamana’ kesi zinalegalega na mwisho wake haujulikani. Wanajamii na hasa walio maskini na fukara huishia kupiga mayowe yasiyo na kimbilio stahiki. Najiuliza Tanzania ya kabla ya ‘uhuru’ inaelekea wapi?

Nani wa kumuamini?

Enzi hizo aliyekuwa akiogopwa na wanajamii alikuwa mnyama wa porini. Hivi sasa imegeuka tunaogopana na kutoaminiana sisi wenyewe wanandamu. Enzi hizo utembeapo peke yako huna wasiwasi na ukimwona mwenzako mbele yako unamkimbilia mfuatane. Hivi sasa siyo hivyo labda uwe unamfahamu na kuzijua tabia zake.

Niwe muwazi, enzi hizo ukimwona Polisi hata usiku wa manane utamfuata na atakupa msaada wa kukusindikiza hadi kwako au jirani na utakuwa salama na mali yako. Hivi sasa unamkwepa hata Polisi. Kunani?

Idara za mahakama nazo zinapigiwa kelele kwa miongo kadhaa ni kama wameziba masikio; kutokana na tuhuma za malimbikizo ya kesi lukuki hasa zile zinazowahusu watu maarufu ama wenye uwezo, wakihusishwa na ubadhirifu wa mabilioni ya fedha.

Wezi wa kuku na bata ndiyo wamejaa magerezani, hata kesi za waliobambikizwa. Wazito hao au wenye madaraka kwao kulindana kwa ubadhirifu wa wazi kwao ni ‘fasheni’ mpya. Hawaoni soni asilaani. Tanzania inaelekea wapi?

Maadili stahiki yatoweka

Maadili mema ya maisha yetu yametoweka kwa kiasi kikubwa. Mafunzo na maelekezo yalikuwa yanaanzia vijijini; bali sasa ni ‘shagalabagala’ kwa wanajamii wote.

Naweza kuiunganisha hali hii na elimu duni, uchumi mbovu, kukosekana kwa ajira, ukame wa nchi na mengineyo. Lakini pia, ni kutokana na uongozi dhaifu, viongozi wengi wanajali zaidi masilahi binafsi. Mambo haya huchagiza tabia ya ‘kila mtu na lake’. Kutowajali wananchi. Tumwamini nani?