UCHAMBUZI: Maandalizi ya Taifa Stars CHAN 2020 yanatia shaka

Fainali za Afrika Kwa Wachezaji Wanaocheza Ligi za Ndani (CHAN) zitafanyika Cameroon kuanzia Aprili 4 hadi 25, mwaka huu.

Mashindano hayo yanakutanisha wachezaji wanaocheza katika ligi za ndani na Tanzania ni miongoni mwa timu zitakazoshiriki.

Tanzania iliyopangwa Kundi D na Zambia, Guinea, Namibia na itashiriki kwa mara ya pili fainali hizo baada ya kufuzu mwaka 2009 nchini Ivory Coast.

Tanzania imefuzu CHAN baada ya kuzitoa Kenya na Sudan ikiwa chini ya kocha Mrundi Etienne Ndayiragije.

Katika mashindano ya mwaka huu Cameroon imepangwa Kundi A na Zimbabwe, Mali, Burkina Faso.

DR Congo yenye rekodi ya kutwaa ubingwa wa mashindano hayo mara mbili ipo Kundi B dhidi Congo Brazaville, Libya na Niger.

Mabingwa watetezi Morocco wapo Kundi C wakichuana na Rwanda, Uganda, Togo ambao wanashiriki fainali hizo kwa mara ya kwanza.

Kundi A litakuwa na Burkina Faso inayocheza kwa mara ya tatu fainali hizo, Zimbabwe, Mali na Cameroon.

Katika mashindano hayo, Taifa Stars imepangwa kufungua dimba dhidi ya Zambia kabla ya kuzivaa Namibia na Guinea Bissau.

Taifa Stars itajitupa kwenye Uwanja wa Limbe Aprili 7 kabla ya Aprili 11 kuivaa Namibia na itamaliza mchezo wa kundi lake Aprili 15 dhidi ya Guinea Bissau.

Hii itakuwa mara ya pili Taifa Stars kucheza na Zambia katika fainali hizo kwani mwaka 2009 zilitoka sare ya bao 1-1 zilipokuwa Kundi A.

Wakati Taifa Stars haina dalili ya kutangaza kikosi, baadhi ya timu zinazoshiriki fainali hizo zimecheza mechi za kirafiki za kupima vikosi vyao.

Mechi za kirafiki zina maana kubwa kwa timu inayokwenda kushindana kimataifa kwa kuwa inatoa nafasi kwa kocha kupima ubora wa wachezaji wake.

Timu za nje zimeanza kujifua mapema kwa kuwa zinatambua Aprili 4 si mbali, ni muda mfupi umebaki kabla ya kuanza mashindano hayo.

Maandalizi yanayofanywa na timu hizo ni vyema pia yakaanza kwa Taifa Stars kwani imepangwa kundi gumu ambalo lina timu zenye ushindani.

Rekodi ya Zambia katika mashindano ya kimataifa ni kubwa. Hata hivyo Namibia na Guinea hazipaswi kudharauliwa ni timu zilizopiga hatua katika soka kwenye miaka ya hivi karibuni.

Kwa mujibu wa viwango vya ubora duniani vilivyotolewa Februari 20, mwaka huu, Namibia inashika nafasI 117 na imewahi kushika nafasi ya 68.

Guinea inashika nafasi ya 74 na imewahi kufanya vyema hadi nafasi ya 22. Zambia ipo nafasi ya 88 na imewahi kukamata namba 15. Tanzania ipo nafasi ya 134, imewahi kufika namba 65.

Tutakosea kama tutadhani mchezo wa kufuzu Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) dhidi ya Tunisia Februari 27 na ile ya marudiano Februari 31 utakuwa kipimo kwa Taifa Stars.

Naamini katika mechi hizo mbili Taifa Stars itawatumia kina Mbwana Samatta, Simon Msuva na wengine wanaocheza nje ya nchi.

Katika mechi hizo mbili kocha ana nafasi kubwa ya kuwatumia wachezaji wanaocheza soka nje ambao hawatacheza fainali za Chan.

Maandalizi ya mapema yana faida kubwa kwa kuwa kocha ana nafasi nzuri ya kuwa na wigo mpana wa kupata kikosi cha kwanza na wale watakuwa wakianzia benchi.

Naamini kocha wa Taifa Stars atakuwa na nafasi nzuri ya kuita timu bora yenye damu mchanganyiko hasa wachezaji wanaotoka timu za mikoani ambao wameonyesha viwango bora msimu huu.

Tangu kuanza msimu huu ligi imekuwa na ushindani hasa katika eneo la ufungaji ambapo wamechomoza idadi kubwa ya wachezaji wasiokuwa na majina, lakini wamekuwa tishio.

Miongoni mwa wachezaji wanaofanya vyema katika mashindano hayo ni kinara wa mabao wa Namungo, Reliant Lusajo.

Maandalizi ya zimamoto yamekuwa yakigharimu wanamichezo wetu na hilo lilithibitika katika mchezo wa ngumi ambako mabondia wote wanne waliokwenda Dagal, Senegal kusaka viwango vya kufuzu mashindano ya Olimpiki walipoteza mapambano yao.

Mabondia hao hawakupoteza mapambano yao kwa bahati mbaya, walishindwa kwa kuwa hakuwafanya maandalizi ya kutosha.

Anguko kama hili naliona pia kwa wanariadha wetu wawili waliofuzu Olimpiki Alfonce Simbu na Failuna Abdi ambao hadi hawako kambini.

Wanariadha wa majirani zetu Kenya wako kambini katika mji wa Eldoret tangu Januari wakijiandaa na fainali.

Mashindano ya Olimpiki yamepangwa kuanza Julai 26 na yatashirikisha wanamichezo nyota duniani.