Madaktari bingwa waeleza kinga, tiba ya kunuka kinywa

Ulishawahi kuzungumza na mtu mwenye harufu mbaya ya kinywa? ulijisikiaje na ulimshauri vipi?

Ni wazi kuwa mtu mwenye tatizo la kunuka kinywa huwapa kero anaozungumza nao kwa sababu huwa wanajitahidi kumkwepa kwa kuangalia pembeni ili wasikutane na adha hiyo.

Harufu mbaya ya kinywa huweza kuathiri uhusiano, siyo kwa mpenzi tu bali hata marafiki na jamii kwa ujumla.

Kinachoshangaza watu wanaokwepa harufu hiyo, wamekuwa wakiogopa kumwambia ukweli wenye tatizo hilo ili atafute tiba sahihi ya kinywa chake.

Kwa mujibu wa wataalamu wa afya, kuna zaidi ya aina 600 ya bakteria wanaoishi kwenye kinywa cha binadamu, wapo sehemu ya juu ya ulimi, fizi na kuzunguka meno, lakini harufu nyingi hutokana na vyakula vyenye asili ya protini.

Mtandao wa Daily Mail unaeleza kuwa, kile unakula kinachafua hewa unayotoa iwe mdomoni au sehemu nyingine.

Kwa mujibu wa mtandao huo, baadhi ya vyakula vina matokeo mabaya kwa hurufu unayotoa kinywani na kwamba kiwango cha harufu hutofautiana kutokana na muda (mchana, usiku na asubuhi).

Mkazi wa Ilala, Salum Hussein anasema binafsi hana tatizo la kunuka kinywa, lakini huwa anakwenda kliniki ya meno kila baada ya miezi mitatu kuangalia afya ya kinywa chake.

“Binafsi harufu ya kinywa siipendi na inakera sana, wakati mwingine unazungumza na mtu, harufu inapuliza hasa na unashindwa kumwambia, labda kama umemzoea sana,” anasema.

“Lakini, tujenge utamaduni wa kwenda kliniki ya kinywa na meno kucheki afya zetu, hilo litasaidia.”

Wataalamu wa afya

Hata hivyo, mwandishi wa gazeti hili, amefanya mahojiano maalumu na madaktari bingwa wa kinywa na meno kutoka Hospitali ya Taaluma na Tiba Mloganzila (MAMC) kuhusu tatizo la kinywa kutoa harufu.

Madaktari hao wametaja sababu za harufu mbaya kinywani, jinsi ya kujitambua, kuepuka, kujikinga na tiba yake.

Bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya kinywa na meno MAMC, Dk Luka Mboboyu anasema harufu mbaya kitaalamu inaitwa halitosis.

Chanzo kikuu cha harufu hiyo ni ugonjwa wa fizi na mgonjwa mengine ya mfumo wa mwili kama saratani ya damu, shinikizo la damu, kisukari na mengineyo.

“Ugonjwa wa fizi husababishwa na mawe au ugaga unaotokana na bakteria, mabaki ya chakula na madini mbalimbali kutoka kwenye meno na mdomo kuunda mawe magumu tunaita ‘calculus’, hizo husababisha fizi kutoa damu na harufu mbaya mdomoni,” anasema Dk Mboboyu.

Anaeleza kuwa tiba yake ni kujisafisha meno na kinywa angalau mara mbili kwa siku hasa usiku baada ya kula, “zaidi ni kutibu magonjwa jumuishi ya mwili,” anasema.

Daktari bingwa wa afya ya kinywa na meno MAMC, Cecilia Kayombo anasema tatizo la kutoa harufu mbaya kinywani lina visababishi vingi na mojawapo ni matundu kwenye meno kama yametoboka huhifadhi mabaki ya chakula.

Anasema ikiwa mtu anaposafisha meno hasafishi vizuri, yale mabaki yanasababisha harufu mbaya kinywani lakini mengine ni magonjwa ya fizi.

“Kwa mfano una ugaga kwenye meno ile ni mchanganyikiko wa mabaki ya chakula na bakteria ambao wako mdomoni, ambao wanakula katika yale mabaki na wanatoa kemikali fulani zinazosababisha harufu mbaya mdomoni,” anasema Dk Kayombo.

Anaeleza kuwa wakati mwingine wapo waliofikia hatua ya kung’oa meno kwa kudhani kuwa ndiyo sababu ya harufu mbaya mdomoni.

“Utajikuta unang’oa meno mengi, mwisho wa siku unajikuta huna meno, lakini ukiona unalo hilo tatizo jitahidi kufika kwa daktari ili kuchunguzwa nini chanzo cha tatizo ulilonalo,” anasema Dk Kayombo.

Anafafanua kuwa wakati mwingine siyo meno wala fizi bali mhusika anaweza kuwa na tatizo tumboni linalosababisha harufu.

Dk Kayombo anasema ni vyema unapofahamu tatizo hilo au kuambiwa na jirani kumuona daktari.

Anasema unaweza kujitambua kama unatoa harufu mbaya mdomoni kupitia kiganja kwa kutoa hewa mdomoni na kisha kuizuia na kiganja na baada ya sekunde kadhaa kunusa kiganja.

“Lakini unaweza kukaa na majirani zako mmekaa ukiongea kila mtu anaangalia pembeni kwa hiyo hapo lazima utambue kuwa una tatizo,” anasema Dk Kayombo.

Hata hivyo, anataja sababu nyingine ya kutoa harufu mbaya mdomoni kuwa ni kukaa kwa muda mrefu bila kula chochote au kuzungumza. “Huwa inatokea inasababishwa na gesi sanasana ukikaa muda mrefu hujaongea au kula,” anasema.

Madhara

Alipoulizwa kama kuna madhara yoyote ambayo mhusika anaweza kuyapata ikiwa ana tatizo la kutoa harufu mbaya kinywani, anasema; “Yeye mwenyewe anaweza kujitenga na jamii, anakuwa anashindwa kuchangamana na watu na wengine wanatabia ya kula ‘big G.’

“Hiyo haiwezi kusaidia, kama ni meno yatibiwe na kama ni magonjwa ya fizi pia yatibiwe na kama ni magonjwa ya ngozi pia aangaliwe na kupewa tiba sahihi kujua tatizo ni gesi ya tumboni au vinginevyo.”

Dk Kayombo anasema matibabu ya tatizo hilo hutegemea na iwapo mgonjwa ana matundu huzibwa, tunang’oa kama ni ugaga hunasafisha na kama ni vinginevyo wanaangalia namna ya kumsaidia na kumtibu kabisa.

Anataja vihatarishi vilivyopo iwapo mgonjwa hatatunza vizuri afya ya kinywa na meno.

“Mojawapo ni saratani ya ulimi, midomo, saratani ya kwenye matezi inayosababishwa na kutotunza vizuri afya ya kinywa, kuna vihatarishi kwa mfano kuvuta sigara, kula ugoro, kutafuna mirungi, tumbaku, shisha.

“Mara nyingi wanaotumia vitu hivyo wanakuwa hawako makini katika kusafisha kinywa na meno ndiyo maana kunakuwa ni kihatarishi kikubwa kwao lakini pombe pia, wito wangu kwa wananchi wote ni kwamba kinywa na meno ni muhimu kwa mwili mzima, piga mswaki (kusafisha kinywa) angalau mara mbili kwa siku na hakikisha unatumia dawa yenye madini ya floride.”

Kinachosababisha harufu mbaya

Kutokuwa makini na usafi wa kinywa kama vile kusafisha kinywa kwa mswaki vizuri kunaacha mabaki ya chakula ambayo huoza na kusababisha harufu mbaya.

Maambukizi ya magonjwa kama vile fizi kutoka damu, mfumo wa upumuaji na kisukari. Kinywa kuwa kikavu kutokana na kuvuta sigara au kunywa kahawa.

Jinsi ya kujitambua

Wanasayansi wamekiri kwamba ni ngumu sana mtu kujijua mwenyewe kama ana harufu mbaya kwa sababu ya mazoea (habituation).

Lakini ni rahisi sana kutambua harufu kutoka kwenye kinywa cha mtu mwingine. Unaweza kutambua kama una harufu mbaya mdomoni kwa kumuuliza mtu unayemuamini. Pia, unaweza kujua harufu mbaya kwa kulamba nyuma ya kiganja na kunusa, kisayansi unaweza kutumia vifaa kama Halimeter, Gas Chromatography na Bana Test.