Magufuli azindua flyover, atema cheche

Rais John Magufuli (kulia), akisikiliza maelezo ya Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale kuhusu mchoro wa barabara ya juu itakayojengwa eneo la Tazara, wakati Rais alipozindua mradi huo jijini Dar es Salaam jana. Wa tatu kutoka kushoto ni Balozi wa Japan nchini Toshio Nagase na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.

Picha na Salim Shao

Muktasari:

Ingawa hakufafanua wala kuzungumza kwa undani juu ya methali hiyo, hivi karibuni Bodi ya Shirika la Changamoto za Millenia (MCC) ya Marekani ililitangaza kufuta ufadhili wa miradi yenye thamani ya Sh1.3 trilioni kwa madai kuwa Tanzania ilikiuka misingi ya kidemokrasia kwa kurudia uchaguzi wa Zanzibar na kushindwa kusimamia Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli jana aliweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa barabara za juu (flyover) huku akiwaambia wananchi: “Ni heri kula muhogo kuliko kula mkate wa kusimangiwa.”

Ingawa hakufafanua wala kuzungumza kwa undani juu ya methali hiyo, hivi karibuni Bodi ya Shirika la Changamoto za Millenia (MCC) ya Marekani ililitangaza kufuta ufadhili wa miradi yenye thamani ya Sh1.3 trilioni kwa madai kuwa Tanzania ilikiuka misingi ya kidemokrasia kwa kurudia uchaguzi wa Zanzibar na kushindwa kusimamia Sheria ya Makosa ya Mtandao.

Hata hivyo, katika hotuba yake, Rais Magufuli aliishukuru Serikali ya Japan kwa kuendelea kuisaidia Tanzania akisema imekuwa rafiki kwa miaka zaidi ya 30 sasa.

Japan ni marafiki wa kweli… lakini tunawashukuru kwa sababu wanaona usimamizi tunaofanya katika fedha zao,” alisema.

Shirika la Japan la Ushirikiano wa Kimataifa (JICA) ndiyo wafadhili wakuu wa mradi huo ambao. Litatoa Sh93.4 bilioni na Serikali ya Tanzania itatoa 8.3 bilioni.

Methali hiyo ya Dk Magufuli imepokewa kwa hisia tofauti na wanasiasa akiwamo, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Salum Mwalimu ambaye alisema: “... Wakati mwingine tunapewa misaada kwa sababu ya kudumisha mahusiano na si kwa sababu ya umasikini.”

Alisema sababu zinazotolewa na Serikali kukataa misaada hazina msingi kwa maelezo kuwa fedha za MCC zilikuwa na sharti dogo la kuheshimu demokrasia.

“Kama tungeikataa misaada kwa kulazimishwa ndoa za jinsia moja au ushoga tungeipongeza Serikali ila kunyimwa kwa sababu ya kukiuka demokrasia ni aibu kubwa. Fedha za MCC zilikuwa zisaidie miradi ya umeme tujiulize ni Watanzania wangapi wanakosa nishati hii?” alidai.

Alisema sura ya bajeti mwaka 2016/17 ya Sh29 trilioni haiwezi kutekelezeka bila kutegemea misaada kwa maelezo kuwa uwezo wa Serikali kukusanya mapato hauzidi Sh17 trilioni na kwamba nchi haiwezi kujiendesha kwa makusanyo ya kodi pekee.

Profesa Mohammed Bakari wa Idara ya Sayansi ya Siasa na Utawala Bora, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) alisema kauli hiyo ni ya kisiasa zaidi kuliko uhalisia.

Alisema sababu za kukosa msaada wa MCC zinajulikana wazi, ilikuwa ni kukiuka masharti yake.

“Kwa hivyo kauli hiyo inaonekana kuwa kulinda zaidi masilahi ya viongozi wanaotaka madaraka kuliko ya Watanzania wanaohitaji misaada hiyo kwa maendeleo,” alisema.

Alifafanua mchambuzi huo akisema hakuna nchi inayoweza kukataa misaada hiyo kwa sasa na kwamba masharti yaliyotolewa hayakuwa yanapokonya au kuingilia uhuru wa Tanzania na badala yake yalilenga kuimarisha utawala bora.

Mwanaharakati wa haki za binadamu na mtetezi wa masuala ya kijinsia hapa nchini kutoka Mtandao wa Jinsia Tanzania (TGNP), Gemma Akilimali alisema hakukuwa na sababu ya Rais Magufuli kuzungumza kauli hiyo kwa nchi iliyotusaidia kwa miaka mingi.

Alisema kama ambavyo Rais Magufuli amekuwa akitamani kudhibiti mianya ya ufisadi na rushwa, ndivyo pia wahisani wamekuwa wakitamani kuona utawala bora ukionekana kwa nchi nyingi wanazozisaidia.

“Hata hao aliowasifia wana masilahi yao, hakuna asiyekuwa na masilahi ila yanatofautiana, kwa hivyo tunatakiwa kuheshimu misaada iliyotolewa na kujiandaa baadaye tujitegemee wenyewe,” alisema.

Azungumzia Dart

Katika hotuba yake, Rais Magufuli alizungumzia awamu ya kwanza ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dart) na kusema Serikali imelazimika kuusimamisha kwanza baada ya kubaini dosari katika mkataba ambazo zingeisababishia hasara.

“Watu wanadhani watatumia vibaya fedha za umma nawaahidi hachomoki mtu, endapo mtu atajaribu kutumia vibaya fedha za umma, ‘achomoke’ mwenyewe,” alisema.

Alisema mradi huo umetumia Sh388 bilioni ambazo zilikopwa na Serikali lakini kuna mazingira yalikuwa yanaandaliwa ya utapeli ili kula fedha za walipakodi.

“Haiwezekani Serikali ikope fedha Benki ya Dunia, isitoshe Serikali ina ubia wa asilimia 49 katika mradi huo, halafu anakuja mtu anasema fedha hizo ni zake, sisi tulikataa na tukasema hawapati kitu hapa, mbele ya Serikali yangu nikafunga huo utapeli kwa makufuli kama jina langu,” alisema huku akisisitiza;

“Haiwezekani mradi wa kuwasaidia Watanzania halafu uwakandamize tena kwa gharama kubwa.”

Watumishi hewa

Rais Magufuli pia alizungumzia suala la watumishi wanavyotafuna fedha za umma akitoa mfano wa mhasibu aliyejilipa mishahara ya watumishi 57 ambao wameshastaafu.

“Leo (jana) nimesoma gazeti moja limeandika habari ya mtumishi mmoja, ambaye yeye alikuwa anajilipa mishahara ya wastaafu 57, kwa hali hii hapana, Watanzania wamechoka kusubiri kwa hivyo lazima tubanane hukuhuku,” alisema na kuongeza:

“Ninawahakikishia kwa kuwa nyinyi ndiyo mmenichagua basi hachomoki mtu kwenye hili, labda achomoke mwenyewe, nataka fedha zipatikane na ziendelee kusaidia maisha ya Watanzania.”

Kupunguza msongamano

Rais Magufuli alisema katika juhudi za kupunguza foleni katika jiji hilo, Serikali imejiandaa kutekeleza miradi mbalimbali huku akiahidi kuifanya Dar es Salaam kuwa mpya katika kipindi cha uongozi wake.

“Taarifa ya Ofisi ya Takwimu 2013, zinaonyesha kuwa tatizo la foleni katika jiji hilo imesababisha kupotea kwa Sh411.3bilioni, ukiacha wengine wanaofariki njiani kwa kuchelewa huduma za afya na ndoa nyingine za watani zangu Wazaramo zinazovunjika kwa sababu ya foleni,” alisema na kuwafanya wananchi waliohudhuria hafla hiyo kuangua vicheko.

Alisema jiji la Dar es Salaam ni kioo na kitovu cha usafirishaji wa mizigo inayokwenda nchi jirani hivyo ni lazima kuimarisha usalama na kupunguza kero ya msongamano wa magari.

Alisema katika awamu ya pili ya mradi wa Dart, Serikali itapanua Barabara ya Kilwa na kutoka Chang’ombe -Kawawa. Katika mradi wa awamu ya tatu, Serikali itafanya upanuzi wa Barabara za Nyerere, Uhuru na Azikiwe huku akiahidi kutenga Sh1 trilioni kwa ajili ya ujenzi wa reli kutoka Dar hadi Ruvu. Miradi mingine aliyoitaja ni flyover Ubungo na ule wa barabara ya Dar – Chalinze.

Rais Mgufuli alisema Watanzania wamechoka kusikia uchungu (wa maisha) kwa miaka mingi ndani ya Taifa lao huku akiwataka watendaji wavumilie katika kipindi hiki ili kuwapeleka maendeleo.

“Ndiyo maana tumetenga asilimia 40 ya bajeti iende kwenye maendeleo tofauti na miaka ya nyuma, sasa hivi fedha za safari, viposho, viseminasemina na vichaichai maofisini tunazikata zote zikasaidie Watanzania kwenye miradi na kama kuna watakaoona hawawezi, bora waache kazi ila fedha lazima zikahudumie afya na elimu bure,” alisema.

Aliwataka wakazi wa jiji Dar kulinda barabara zinazojengwa huku akiwapongeza mameya wa Temeke na Ilala waliohudhuria sherehe na kuwataka kuimarisha usafi.

Baada ya Rais hotuba yake, Rais Magufuli aliamua kutembea kwa miguu kutoka eneo la sherehe hizo, akipita katikati ya barabara inayoelekea Posta huku akiwasalimia vijana waliokuwa wakimshangilia ‘Rais Rais, Rais na wengine wakiimba ‘tumbua majipu, tumbua majipu’.

Kuhusu flyover

Awali, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Tanroads, Mhandisi Patrick Mfugale alisema lengo la mradi huo ni kupunguza foleni jijini.

Alisema mradi huo utapunguza muda wa kukaa kwenye foleni kwa asilimia 80, akimaanisha kupungua muda kutoka dakika 45 hadi kufikia dakika 10 za kuvuka kwenye makutano hayo na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2018.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa, wabunge, mameya wa Ilala na Temeke na wenyeviti wa taasisi zote za ujenzi kutoka wizara hiyo.

Pamoja na utambulisho huo, hotuba zilizowasilishwa kwa lugha ya Kiswahili na Balozi wa Japani nchini na

Hotuba ya Wajapani kivutio

Katika hafla hiyo, hotuba zilizotolewa kwa lugha ya Kiswahili na Balozi wa Japan nchini Masaharu Yoshinda na Mwakilishi wa JICA Tanzania, Toshio Nagase ziliwasisimua viongozi na wananchi waliohudhuria kutokana na jinsi walivyokuwa wakijitahidi kutamka baadhi ya maneno.