Zao la ufuta limeanza kufuta umaskini kwa wakulima vijijini

Thursday February 19 2015

 

Nimeingia katika Kijiji cha Erri, Tarafa ya Mbugwe Wilaya ya Babati, mkoani Manyara. Ni eneo ambalo uchumi wa wakazi wengi wanategemea kilimo.

Naona mazao ya aina mbalimbali kama vile mahindi na maharagwe kwa ajili ya chakula na vilevile wanalima ufuta, kama moja ya zao lao la biashara.

Ama kweli, watu katika kijiji hiki wanaonekana wakijibidisha sana katika kilimo maana karibu kila mtu mzima na vijana, ama ana jembe, panga na zana jingine kwa ajili ya kilimo.

Nafika katika moja ya shamba la mkulima wa ufuta. Anajitambulisha kwangu kuwa ni Romana Ezekiel. Ananimbia: “Awali niliwakuta wazazi wangu wanalima zao hili la ufuta lakini sikufahamu thamani yake na wakati mwingine mimi binafsi nimekuwa nikilipuuza kwa miaka kadhaa,” alisema na kuongeza; “Katika miaka ya karibuni Shirika la Kilimo la Farm Africa lilifika kijijini kwetu na kutuelimisha juu ya kilimo hiki.”

Anasema yeye na wakulima wenzake kwa sasa wanajua umuhimu wa zao hilo na ndiyo maana wanajitahidi kulilima kwa ajili ya kuuza na kupata fedha.

Mkulima huyo anasema kwa sasa zao hili limebadili mwenendo wa maisha katika familia yake kwa sababu baada ya kuuza anapata fedha kwa ajili ya kuwagharimia watoto kielimu, kiafya, mavazi, chakula na kuboresha makazi yake.

Mkulima mwingine katika Kijiji cha Vilima Vitatu, Mwanaidi Salim anasema, amefurahi kupata kazi nyingine inayomwongezea kipatao katika shughuli zake za kilimo.

“Hivi sasa nimeweza kujenga nyumba pia kuboresha maisha ya familia,” anasema Salim.

Alisema kilichomsaidia yeye kuweza kufanya zao la ufuta kama mkombozi, ni kufuata masharti ya kanuni na taratibu za kulima zao hilo na hata baadaye kuyajua masoko.

Salim anasema baada ya kulima ufuta, aliuza baadhi yake na nyingine akatumia kwa kutengeneza unga wa lishe na kashata.

Kwa kufanya hivyo anasema ilimuongezea kipato na kuondokana na maisha ya awali ya kuishi nyumba ya tembe na sasa amejenga nyumba za kisasa kwa maana ya zile za matofali na kuezekwa kwa bati.

Edina Walele, mkulima wa Kijiji cha Vilima Vitatu, anasema kutokana na kulima zao hilo ameweza kunufaika kwa kununua mbuzi wa kisasa wa maziwa, kuweka umeme kwenye nyumba yake na kuongeza mtaji katika duka lake la rejareja lililopo kijiji hapo.

Mbinu za kilimo

Mkulima wa Kijiji cha Mawemairo, Moshi Mohamed anasema awali hakufahamu njia za uzalishaji bora wa ufuta, kwani alikuwa akiuchukua na kuurusha katika shamba la mahindi, ambapo wakati mwingine uliota na wakati mwingine haukuota hivyo akapata hasara.

“Baada ya Farm Africa kutupa elimu kuhusiana na kilimo hiki nimeelewa namna ya kupanda na hata jinsi ya kutunza zao limee vizuri,” anasema akifafanua zaidi:

“Hivi sasa navuna mazao mengi na kupata faida ambayo imenisababisha nipate maendeleo na kusomesha watoto wangu bila tatizo lolote.”

Zebedayo Barite ambaye ni mkulima wa Kijiji cha Erri, alisema kuwa baada ya kujiunga kwenye kikundi cha wakulima wa ufuta, alipata mafunzo na mbegu bora, tangu kipindi hicho amenufaika na anaishi katika nyumba nzuri ya kisasa.

Waelimishaji

Mratibu wa mradi huo, William Mwakyami anasema Farm Africa ilianzishwa mwaka 1985 na Sir Michael Wood na David Campbell, waliokuwa na dira ya pamoja ya maendeleo vijijini Afrika kwa kutambua kuwa chakula ni dawa bora na kuendeleza kilimo ni muhimu kwa ufanisi wa suluhisho la kuondokana na umaskini vijijini.

Mwakyami anasema maono ya Farm Africa ni kuona mafanikio vijijini katika nchi na Afrika kwa ujumla.

Mbali na Tanzania, anasema wapo pia Kenya, Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia.

Lengo la shirika, anasema ni kupunguza umaskini kwa kutafuta suluhisho la kudumu kwa kuwajengea uwezo wakulima wa Afrika, ili waweze kukuza kipato chao na kusimamia maliasili zao ziwe endelevu.

“Pamoja na malengo hayo Farm Africa ina nia ya kupunguza umaskini na kupunguza upungufu wa chakula na tunafanya kazi na wakulima wadogo wadogo, wafugaji na jamii zinazoishi karibu na misitu katika Bara la Afrika.”

Anasema shirika hilo lisilo la kiserikali lilifika kwenye vijiji hivyo mwaka 2009 na kufanikiwa kuunda vikundi katika vijiji 23 vya tarafa hiyo.

Ofisa Masoko wa Farm Africa, Rahel Pazzia anasema mradi wa uzalishaji ufuta na masoko ulianza kutekelezwa mwaka 2010 katika Tarafa ya Mbugwe ukiwa umelenga kuwanufaisha wakulima 920.

Pazzia anasema Farm Africa ilichunguza na kubaini zao linalowafaa wakulima hao ni ufuta na ndiyo maana waliamua kuwaelimisha na kuwapatia mbinu za mafanikio.

Ofisa Kilimo wa Farm Africa, Tumaini Elibariki anasema miongoni mwa changamoto zinazowakabili wakulima wa ufuta wa Tarafa ya Mbugwe ni pamoja na wadudu na magonjwa ya mimea hiyo na wakati mwingine hali mbaya ya hewa.

Elibariki anaeleza kwamba, baadhi ya wakulima wanasababisha ubora wa ufuta kupungua kutokana na viwango vya chini vya usafi wakati wa uvunaji.

Anasema wanachofanya ni kuwaelimisha ili wafaidike zaidi na zao hilo.

Advertisement