Imani za kishirikina zakwamisha mradi kwa miaka sita

Thursday May 17 2018

 

By Ngollo John, Mwananchi [email protected]

Wakati wadau wakisisitiza umuhimu wa ujasiriamali kwa lengo la kukuza kipato cha kaya na kupunguza umaskini, imani za kishirikina bado ni kikwazo kufanikisha baadhi ya miradi.

Hali hiyo inajitokeza katika Kijiji cha Ilalambongo wilayani Misungwi ambako kikundi cha ufugaji samaki kimeshindwa kufanikisha lengo walilolikusudia wanachama wake kwa miaka sita sasa.

Inaelezwa kuwa mwaka 2012, wajasiriamali hao walipata Sh24 milioni kutoka Mradi wa Mazingira wa Bonde la Ziwa Viktoria (LVEMPII) walizozielekeza kwenye ufugaji samaki, lakini mpaka sasa hawajapata chochote kutokana na changamoto wanazokutana nazo.

Baada ya kupata fedha hizo, kikundi hicho kilichimba mabwawa sita na kuweka samaki na mwanzoni walikuwa wakivuta maji kutoka Ziwa Viktoria kwa kutumia jenereta na kuyajaza kwenye mabwawa hayo.

Kwa utaratibu huo, walifanikiwa kuvuna samaki mara moja na kuwauza kama walivyokusudia, lakini kutokana na uzoefu walioupata wakatafuta mbinu ya kupunguza gharama za uendeshaji.

Changamoto zilivyoanza

Katika kufanikisha hilo, walibadilisha chanzo cha maji na kuamua kutumia kisima cha asili kilichopo kijijini hapo ndipo changamoto zikaanza kujitokeza.

Mabwawa yakawa hayajai maji na hata yakijazwa maji yanakauka, hivyo kukwamisha ukuaji wa samaki na biashara ya wajasiriamali hao.

Baadhi ya wakazi wa kijiji hicho wanasema suala la kushindwa kuhamisha maji kutoka kwenye kisima cha asili kijijini hapo kuyaingiza kwenye mabwawa hayo ni changamoto inayowasumbua kwa muda mrefu.

Mkazi wa kijiji hicho na mwanakikundi, Peter Lutonja anasema tangu walipobadilisha chanzo cha maji na kuamua kutumia ya kisima wamejikuta wanagonga mwamba.

“Unaweza ukaweka maji kwenye mabwawa baada ya siku mbili unakuta yamekauka na hamuoni yalikoelekea,” anasema Lutonja.

Anasema walibadili maji baada ya kuvuna samaki waliowafuga mara ya kwanza na kukubaliana wabadilishe chanzo cha maji licha ya kanuni kuwataka kubadilisha maji kila baada ya mavuno. Kutokana na changamoto hiyo, Lutonja anasema waliwaita wataalamu kuangalia chanzo na kutoa ushauri, lakini hakuna sababu ya msingi waliyoelezwa wala ushauri makini wanaotakiwa kuuzingatia kubadili hali hiyo.

“Tuliamua kutumia maji ya kisima ili kupunguza gharama kwa kuwa kipo jirani na mabwawa hayo,” anasema.

Mabwawa hayo yapo kilomita tano kutoka ziwani ilhali kisima hicho kipo ndani ya mita 50.

Diwani wa Lubili kilipo kijiji hicho, Ngangizi Zozozo anasema anadhani tatizo hilo linatokana na udongo uliopo eneo hilo kufyonza maji kwa muda mfupi.

Mila zahusishwa

Akizungumzia sababu ya maji hayo kutokaa muda mrefu, mzee marufu kijijini hapo, Onesmo Zezema anasema maombi maalumu yanahitajika kabla maji ya kisima hicho hayajaanza kutumika kwenye mabwawa hayo.

“Tulikuwa na visima vya asili viwili katika kijiji hiki, mwaka 1984 Wazungu kutoka Marekani walitujengea kimoja lakini baada ya kukikamilisha kilikauka ndipo kikabaki hiki,” anasema Zezema.

Kisima hicho kinahudumia zaidi ya kaya 200 za kijiji hicho na vingine jirani hususan wakati wa kiangazi kunapokuwa na uhaba za maji baada ya visima vingi kukauka au kupungukiwa maji.

Kuhusu maji kutoingia kwenye mabwawa ya samaki, mzee Zezema anasema yapo maombi maalumu yatakayofanywa na wazee wa kimila wa kijiji hicho na uongozi wa halmashauri umeahidiwa kwamba yatafanyika hivi karibuni.

“Ni kisima cha ajabu kwa kweli na bila maombi huwezi ukahamisha na kubadilisha matumizi ya maji hayo kufanyia shughuli nyingine, kwani walishajaribu hata wataalamu kuyatoa yakiingia kwenye mabwawa hayakai siku mbili, yanakauka,” anasema.

Mzee huyo anaenda mbali zaidi na kudai kuwa kisima hicho kinaweza kubadilika na kuwa na maji mekundu kama damu ikiwa kuna mtu amefanya kosa akienda hapo kuchota maji.

“Kisima hakiruhusu watu wenye vitovu vikubwa kuchota maji kabla hawajapewa baraka kutoka kwa wazee, vinginevyo kinamzamisha,” anasema mzee huyo.

Uongozi wa halmashauri

Kutokana na maelezo hayo, mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya Misungwi, Eliurd Mwaiteleke aliagiza uongozi wa kijiji hicho kushirikiana na wazee wa mila kufanya maombi na kuhamisha maji hayo kwenda kwenye mabwawa ili mradi wa samaki uendelee.

Anasema halmashauri itatoa fedha kwa ajili ya kununua vifaraga vya samaki ili kuwawezesha wajasiriamali hao kuimarisha mradi wao.

“Hatuwezi kukubali mradi upotee hivihivi wakati fedha za LVEMP ziliwekezwa hapa, lazima mradi uanze kufanya kazi uwanufaishe wakazi wa kijiji hiki,” anasema Mwaiteleke.

Ofisa mifugo na uvuvi wa halmashauri hiyo, Chrispine Shami anasema atashirikiana na wataalamu wengine kutoka LVEMP pamoja na wazee wa mila na wakazi wa kijiji hicho kuhakikisha mradi unatekelezeka.

Mbali na mradi huo, Shami anasema halmashauri hiyo ina mpango wa kuanzisha ufugaji wa samaki kwenye maeneo mbalimbali ili kuongeza uchumi wa wananchi na kulinda rasilimali za maji zizidi kuongezeka na kukidhi mahitaji.

Anasema kuwa Wilaya ya Misungwi ina mabwawa 110, lakini yanayofanya kazi ni 14. “Mkakati wa halmashauri ni kuyafufua mabwawa yote ambayo hayafanyi kazi hivi sasa ili kuongeza uzalishaji wa samaki,” anasema.

Jambo la msingi katika kufanikisha lengo hilo, anasema ni kukabiliana na ukame kwani wafugaji wengi wanategemea maji ya mvua kujaza mabwawa yao suala linalopunguza uzalishaji.

Wadau wanasemaje?

Mtaalamu wa ukuzaji viumbehai wa Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (Sua), Dk Nazael Madalla anasema zipo sababu nyingi za maji kupotea ambazo zinahitaji umakini kuzishughulikia.

Anasema taaluma ya ujenzi wa mabwawa ya ufugaji inahitaji kuzingatia vigezo muhimu ili kupunguza uwezekano wa maji kupotelea ardhini.

“Asili ya udongo ni kitu muhimu cha kuzingatia. Udongo wa mfinyanzi ndio mzuri kwa mabwawa haya. Kama wajasiriamali wa kijiji hicho wamejenga kwenye udongo mwingine, uwezekano wa kupoteza maji ni mkubwa zaidi,” anasema Dk Madala.

Madalla anasema maji yoyote isipokuwa ya chumvi yanafaa kwa ufugaji na kuhusu hali iliyopo kwa wananchi wa Kijiji cha Ilalambogo, anasema inawezekana kina cha maji katika kisima hicho kimepungua, hivyo hayatoshi kujaza mabwawa hayo.

Mratibu wa kitengo cha ufugaji samaki wa Chuo cha Uvuvi Mwanza, Peter Masumbuko anasema ufugaji ni chanzo kizuri cha ajira za uhakika kwa wajasiriamali hasa vijana na wanawake kwa kuwa una uhakika wa kipato.

“Mfugaji anayemiliki bwawa lenye mita 300 za mraba linaloweza kutunza samaki 1,200 hawezi kukosa Sh3.6 milioni baada ya miezi sita atakapowavuna. Kitu muhimu ni kukabiliana na changamoto zake tu,” anasema Masumbuko.

Hivi karibuni, waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina akiwa kwenye ziara mkoani Mwanza alisema takwimu za Taasisi ya Utafiti wa Mazao ya Samaki Ziwa Viktoria (Tafiri) zinaonyesha limesaliwa na asilimia tatu ya samaki wenye ukubwa wa kati ya sentimita 50 hadi 85 ambao wanastahili kuvuliwa.

Samaki waliozidi sentimita 85 ambao ni wazazi wasiotakiwa kuvuliwa ili kuendeleza uzao wamebaki asilimia 0.4 pekee.

Advertisement