Sababu miradi ya maendeleo kutofikia lengo la uanzishwaji

Thursday May 17 2018

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 

By Joseph Alphonce

Kwa tafsiri ya kawaida, mradi ni shughuli yoyote ambayo inaanzishwa kwa lengo la kutatua changamoto iliyopo kwenye jamii.

Mradi wowote unajumisha vitu kadhaa ikiwamo muda wa kuanza na kuisha, rasilimali fedha, nguvukazi na vifaa. Kwa ajili ya kuhakikisha mradi unatekelezwa kiurahisi na ufanisi ,hutawanywa katika shughuli ndogo kisha ndogo zaidi.

Pamoja na kuwa mradi huanzishwa kwa lengo la kutatua changamoto fulani katika jamii, zipo sababu kadhaa ambazo husababisha ama kutekelezwa kwa ufasih uliokusudiwa, kuchelewa, chini ya kiwango au kushindwa kabisa kutimiza lengo la uanzishwaji wake.

Kukosekana kwa ushirikiano kutoka kwa uongozi wa eneo ambapo mradi unatekelezwa ni miongoni mwa sababu zinazoathiri utekelezaji wa mradi.

Endapo mradi husika hautapata ushirikiano wa uongozi hasa wa kisiasa ni vigumu kutekelezwa kwa viwango vilivyokusudiwa.

Aidha kukosekana dhamira na nia ya pamoja ya kuhakikisha mradi unafanikiwa ni jambo jingine muhimu. Kila kiongozi akiwa na mtazamo tofauti juu ya utekelezaji wa mradi bila ya kuafikiana kabla ya kuanza utekelezaji, hakika inaweza kuwa moja ya sababu ya kukwamisha utekelezaji.

Kutokueleweka au kuandikwa vyema kwa mawanda ya mradi nayo ni sababu. Aidha baadhi ya makaridio ya mradi kutokuwa na uhalisia.

Sababu nyingine ni utaratibu usiokubalika wa kubadili kwa ama kuongeza au kupunguza mahitaji ya mradi wakati mradi umeshaanza kutekelezwa huathiri maendeleo ya mradi husika.

Mradi unaweza kushindwa kufikia lengo la uanzishwaji kama hauendani na matarajio ya wadau wanaotakiwa kuwa na dhamira na nia moja.

Kila mdau akiwa na mtazamo wake si kiashiria kizuri kwa ufanisi wa mradi. Aidha ni muhimu pawepo na mawasiliano ya mara kwa mara kati ya wadau kwa faida ya mradi.

Upungufu wa rasilimali fedha, vifaa, na watu ni suala linalohitaji kuangaliwa kwa jicho la tatu. Uwezo duni wa kukusanya fedha za utekezaji wa mradi, endapo ni wa muda mrefu hukwamisha ukamilishaji wake.

Kutokuwapo kwa wataalamu wenye sifa na weledi wa kusimamia mradi husika na ukosefu wa motisha kwa wasimamizi wa mradi nalo ni kitu cha kutazamwa kwani huweza kusababisha wasimamizi kukosa dhamira na nia nzuri ya usimamizi wa mradi.

Kuchelewa kufanyika kwa uamuzi ni kiashiria kibaya kwa ufanisi na ubora wa mradi. Wanasaikolojia wanasema kuchelewa kufanya uamuzi ni kiasharia cha kutokufanya kabisa. Ni lazima wahusika wawe na uharaka wenye tahadhari wa kuchukua hatua na kuruhusu mambo yaende kwa faida ya mradi.

Uamuzi ni lazima uwe wa viwango vinavyoendana na uhitaji. Ukiwa chini ya kiwango nayo ni kiashiria kibaya cha utekelezaji wa mradi wa aina yoyote.

Ununuzi ni eneo ambalo hutumia tarkibani asilimia 70 ya fedha zote za Serikali. Kuchelewa kwa ununuzi wa vifaa na huduma huchelewesha ukamilishaji wa mradi. Ununuzi wa vifaa au huduma ulio chini ya kiwango au usioendana na mahitaji nayo ni sababu ya kukwama kwa miradi mingi.

Rushwa inayoweza kutokea wakati wa kutangaza zabuni au kufanya tathmini ni sababu nyingine. Kama mifumo ya utangazaji wa zabuni na tathmini haikuwa wazi, upatikanaji wa mkandarasi kwa njia ya rushwa inaweza kusababisha mradi kutofikia lengo la uazishwaji. Rushwa nyingine hutokea wakati wa ununuzi ya vifaa au huduma.

Kutokuwapo kwa mgawanyo unaoeleweka wa mamlaka (majukumu) kati ya watendaji wanosimamia na kutekeleza mradi ni eneo jingine.

Kila mtu anayehusika katika utekelezaji wa mradi ni lazima awe na majukumu yaliyoanishwa na yasiyoingiliana na mwingine ili kuepuka migongano na migogoro.

Pasipo mgawanyo wa mamlaka kati ya watendaji usitegemee mradi kukamilika kwa wakati na kwa ubora uliokusudiwa.

Mabadiliko ya teknolojia huweza kusababisha mradi kuchelewa endapo watekelezaji wataamua kusubiri ununuzi wa teknolojia mpya au kutofikia matarajio endapo itatumika teknolojia ya zamani.

Mabadiliko ya sheria na utaratibu wa nchi pia ni sababu mojawapo ya mradi kushindwa kufikia lengo la uanzishwaji endapo mabadiliko hayo yanakindhana na malengo ya mradi.

Mradi unaweza usifikie lengo la uanzishwaji endapo huduma au bidhaa inayozalishwa haitapokelewa vizuri na walaji. Sababu zinaweza kuwa madhara yatokanayo na matumizi ya bidhaa au huduma inayozalishwa na mradi.

Aidha bidhaa au huduma inaweza kushindwa kuhimili ushindani hivyo kupotea sokoni.

Hivyo kabla taasisi haijaanzisha mradi wowote wa maendeleo ni vyema ikajiridhisha katika maeneo yote niliyoorodhesha hapo juu ili lengo la unazishwaji wa mradi liweze kutimia na kufikia lengo lililokusudiwa.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango

Advertisement