Kuzaa katika umri mdogo hakukunifanya nikate tamaa

Sunday June 21 2015Madam Rita

Madam Rita 

By Maimuna Kubegeya

Unapotaja orodha ya wanawake maarufu hapa nchini huwezi kulikosa jina la Rita Paulsen. Mama huyu anayefahamika zaidi kama Madam Rita ni miongoni mwa wanawake wenye mchango mkubwa katika maendeleo ya vijana.

Ni mama wa watoto wawili na pia ni mkurugenzi wa kampuni ya kutengeneza video inayofahamika kama Benchmark Production 360 ambao ni waandaaji wa ‘Bongo Star Search’

Safari ya mama huyu ilikuwa na changamoto nyingi. Kama sio kutiwa moyo na mama yake asingeweza kufika.

“Siwezi kusema nimefanikiwa kwani kila kukicha natamani kwenda mbele zaidi ya hapa nilipo,” anasema na kuongeza “Ukweli ni kwamba nimepitia changamoto nyingi sana za maisha.”

Anasema kupata ujauzito katika umri mdogo, iikuwa ni changamoto moja kubwa, iliyoingilia maisha yake.

“Nilipata ujauzito nikiwa na miaka 14 lakini kwa kuwa hakuna lisilokuwa na majibu chini ya jua. Nilianguka nikasimama na nikaendelea na mapambano kwani ujauzito ule ulikuwa kama chachu katika safari yangu ya maisha na kupipatia ujasiri wa aina yake ulionisukuma kusoma kwa bidii.”

Madam Rita anasema kama wahenga wasemavyo ‘Mungu hamtupi mja wake’ ndivyo ilivyokuwa kwake kwani alisoma na kuhitimu elimu ya sekondari na baadaye alifanya shahada ya masoko.

Kwa mujibu wa Ritha vilevile alijifunza kutengeneza video taaluma anayoifanya kwa ufanisi zaidi.

“Licha ya kuongoza kampuni pia huwa nashiriki kikamilifu kwenye utengenezaji wa video pamoja na matangazo,” anafafanua.

Akiwa ITV

Madam Rita anasema kuwa, kabla ya kuanzisha Kampuni ya BenchMark alikuwa mwajiriwa wa Kampuni ya IPP inayomilikiwa na mfanyabiashara maarufu nchini, Reginald Mengi akifanya katika kazi kwenye televisheni hiyo upande wa masoko.

“Katika maisha yangu hakuna kitu ninachofurahia kama kuwasaidia watu wengine. Hivyo baada ya kufanya kazi kwa muda mfupi kwenye kampuni hiyo nilitoka na kwenda kuanzisha kampuni yangu ili nipate fursa ya kutimiza azma hiyo.”

Anasema kuwa wakati anaanzisha kampuni hiyo, alikuwa na chumba kimoja na mfanyakazi mmoja aliyekuwa akimsaidia kwenye masuala ya usafi kwa kuwa alikuwa akijua anachokifanya haikumchukua muda kuanza kukamilisha ndoto zake.

Anaongeza kuwa jambo kubwa alilozingatia wakati anaanzisha kampuni hiyyo ni jinsi gani angeweza kuibua vijana na kuwawezesha kumudu kuendesha maisha yao na hilo lilidhihirika muda mfupi baada ya kuibua vijana katika fani mbalimbali ya urembo kama Irine Kiwia, Millen Magese na Jokate Mwegelo.

Madamu Rita anasema aliweza kufanya yote hayo akiwa na umri wa miaka 23 tu na kutaja baadhi ya kazi alizowahi kuzifanya kuwa ni pamoja na onyesho la Tuzo Muziki za Kilimanjaro na Shoo ya Miss Tanzania kwa miaka mitano mfululizo.

Anasema katika kipindi hiko ni kampuni yake pekee ndiyo ilikuwa ikifanya kazi za ‘production’ kidigitali na hivyo kuwa kampuni bora zaidi ya ‘video production’ nchini.

Kuzaliwa kwa Bongo star Search

Ujio wa kampuni nyingi katika biashara ya ‘video production’ kwa kiasi fulani ulimfanya afikirie biashara nyingine zaidi lakini akiwa na lengo lake ni kuibua vipaji na kutengeneza ajira kwa vijana.

“Mimi ni mfuatiliaji na mpenzi mkubwa wa onyesho la ‘American Idol’ la nchini Marekani. Kuangalia kipindi hiki kwa muda mrefu kulichangia kwa kiasi kikubwa kuchochea wazo langu la kuwa shoo yangu itakayohusisha vijana moja kwa moja” anafafanua.

Anasema hapo ndipo lilipozaliwa wazo la ‘Bongo Star Search’, shoo ambayo inampa faraja katika maisha yake ya kila siku.

Pamoja na kuwa na kufanya vizuri katika shoo hiyo, Madam Rita anasema kuwa safari yake haijafikia mwisho, kwani baada ya kufanya kwa muda wa miaka minane mfululizo, ameona ipo haja ya kuongeza mradi mwingine.

‘Rita Paulsen talk show’ mradi huu umekamilika kwani tayari ametengeneza vipindi kadhaa. Anachosubiri kwa sasa ni kupata wadhamini ili kiweze kwenda hewani.

“ Nina hakika ni miongoni mwa kazi niliyoitendea haki. Lakini kama ilivyo kwa BSS inalenga kuwa saidia wenye mahitaji lakini pia kuwasimulia hadithi za wenye mafanikio ambazo hazijawahi kusikika.”

Hadithi hizo zitasaidia kuwahamasisha wale walio chini hususani vijana, kujifunza kuona ni jinsi gani wanaweza kujikwamua kimaisha.

Mbali na hilo pia tutatoa darasa la kujipodoa hususan kwa wanawake. Hapo watapata fursa ya kubadilisha muonekano wao na kuonekana wenye kupendeza zaidi.

Rita anatoa wito kwa wanawake wa Kitanzania hususani vijana kuhakikisha wanapambana kwa kile wanachokiamini.

“Hakuna njia rahisi katika kufanikiwa. Binafsi huwa sina tabia ya kukata tamaa. Siku zote huwa nafanya kazi zaidi kuhakikisha kile ninachoamini kinafanikiwa” anafafanua

Ikiwa uko kwenye mzunguko wa watu wanaokatisha tamaa, jitoe huko na tafuta watakaokuhamasisha kufikia ndoto zako anasisitiza.

Advertisement