MAONI YA MHARIRI: Serikali isikilize ushauri wa sekta binafsi nchini

Ushauri kwamba Serikali inatakiwa kushirikiana kikamilifu na wawekezaji binafsi ili kufanikisha dhana ya Tanzania ya viwanda ni jambo jema la kupigiwa mstari na linalopaswa kuwekewa msisitizo.

Ushauri huo uliotolewa juzi na mwenyekiti wa maofisa watendaji wakuu wa kampuni nchini (CEOrt), Ali Mufuruki katika hafla ya uzinduzi wa mwonekano mpya wa gazeti la The Citizen jijini Dar es Salaam, unaibua kilio cha muda sasa cha wafanyabiashara na sekta hiyo kwa ujumla kuwa ni kama vile wamewekwa kando licha ya kuwa wadau muhimu wa maendeleo.

Yamekuwapo malalamiko kwamba mipango ya Serikali imekuwa ikiwaacha nyuma wadau wa sekta binafsi, hasa katika kuwapatia mazingira wezeshi ya kuendesha shughuli zao na kufanikisha mkakati wa Serikali wa kuifanya nchi kuwa ya viwanda.

Badala yake wanadai kuwa kinachoangaliwa na kusisitizwa ni ongezeko la kodi na tozo mbalimbali, kuwekwa sheria na kanuni za kuwabana zaidi, mambo yanayoelezwa kufanya makampuni mengi kuyumba. Pamoja na kwamba nia ya Serikali ya kuongeza mapato na kuhudumia miradi mikubwa kwa fedha za ndani ni njema, lakini hatua zinazochukuliwa katika kuongeza mapato hayo zimekuwa zinadaiwa kuleta athari mbalimbali kwa sekta hiyo kama vile kufungwa kwa biashara, kupunguza wafanyakazi na hata kupungua wigo wa kodi.

Masuala hayo kwa vyovyote vile mwisho wake ni kuathiri uchumi uleule uliokusudiwa kusisimuliwa na kukuzwa, kwa kuwa wananchi wengi watakuwa hawana kazi na shughuli za uwekezaji zitakuwa hazina faida ya kutosha kuendeleza mitaji yake.

Ni kutokana na hali hiyo, Mufuruki akasema hata vile viwanda vilivyokuwa vya Serikali vilivyobinafsishwa, baadhi yake vilikufa kutokana na Serikali kushindwa kuwasaidia wawekezaji waliovinunua kwa kuvilea.

Akifafanua hoja yake, Mufuruki anasema katika ubinafsishaji Serikali zilizopita hazikujikita kuwalea wawekezaji waliouziwa viwanda, hivyo wakajikuta wakipata matatizo ya uendeshaji kwa kuwa hawakupatiwa malezi mazuri ya uwekezaji.

Kwa maelezo hayo, hata kwa viwanda vinavyojengwa sasa kama Serikali inawakaribisha wawekezaji lakini inashindwa kutoa ushirikiano siku uwekezaji ukiyumba na yenyewe inaishia kulaumiwa.

Kwa siku za karibuni Serikali imekuwa ikiwalaumu wafanyabiashara au wawekezaji walioshindwa kuendeleza viwanda vilivyobinafsishwa na wengine kuwanyang’anya viwanda hivyo, jambo linaloishangaza sekta binafsi kuona wawekezaji wakilaumiwa kwa viwanda hivyo kufa huku Serikali ikiwa haijafanya lolote kutoa ‘sapoti’ kwao, kama kuongezewa mitaji.

Hata hivyo, kutokana na nia njema ya Serikali kama inavyothibitishwa na kauli ya kaimu mkurugenzi wa Idara ya Uwekezaji, Aristides Mbwasi aliyoitoa kwenye hafla hiyo kwa niaba ya waziri wa Viwanda, Charles Mwijage, tunayo imani kuwa kilio cha sekta binafsi kinasikika na kitafanyiwa kazi.

Mbwasi alisema kuwa Serikali itaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Kama Mbwasi anavyowaomba wawekezaji wa kampuni mbalimbali kujitokeza katika maonyesho ya pili ya viwanda yatakayofanyika mwezi ujao katika viwanja vya maonyesho vya Sabasaba jijini Dar es Salaam, ni imani yetu pia kuwa watafanya hivyo ili kupata fursa ya kukutana na mamlaka za Serikali na kueleza mazingira yanayowakwamisha, na Serikali itaendelea kuwasikiliza na kufanyia kazi malalamiko na ushauri wao ili hatimaye kwa pamoja waweze kusukuma mbele gurudumu la maendeleo.