UCHAMBUZI: Wateule wa Rais wanaposahau majukumu yao nani wa kuwakumbusha

Friday January 12 2018Fidelis Butahe

Fidelis Butahe 

Wiki hii, Rais John Magufuli alitoa kauli ambayo mpaka ninapoandika uchambuzi huu ninaitafakari.Nakumbuka Novemba 5, 2015 siku ambayo Dk Magufuli aliapishwa kuwa Rais wa Awamu ya Tano, ilimchukua muda kidogo kuteua Baraza la Mawaziri.

Hata alipoteua mawaziri 34, kuna wanne hakuwataja akijipa muda zaidi wa kutafuta watu sahihi katika wizara hizo nyeti, akiamini akiwapata wachapa kazi, mambo yatakwenda sawasawa.

Baada ya hapo amekuwa akiwatumbua baadhi ya watendaji wa Serikali wakiwamo mawaziri aliokwisha kuwateua. Mpaka kufikia jana watendaji takribani 100 wameshaondolewa katika nafasi zao katika kipindi cha miaka miwili.

Wakati Rais akifanya hivi niliamini wazi anataka kutengeneza viongozi wanaokwenda sambamba na kasi yake ya ‘Hapa Kazi Tu’. Kupata wasaidizi wenye mtazamo na fikra zinazofanana naye.

Sasa imekuwaje? Juzi tu Rais aliweka bayana udhaifu wa mawaziri wa madini na kilimo, manaibu na watendaji wao, akiwapa wiki moja, kubainisha kwamba kuna baadhi ya wateule wake bado hawajamuelewa anataka nini. Siku hiyo alitengua uteuzi wa Kamishna wa Madini, Benjamin Mchwampaka ambaye aliteuliwa Aprili mwaka jana, kwa kushindwa kumshauri Waziri wa Madini kuhusu kanuni za Sheria ya Madini Namba 7 ya mwaka 2017. “Labda ataenda kuamsha waliolala”, Rais alitoa kauli hiyo katika hafla ya kumuapisha Naibu Waziri wa Madini, Dotto Biteko akimaanisha huenda uteuzi wake utakwenda kuamsha waliolala.

Tangu alipoingia madarakani hadi sasa, Rais amekuwa akizungumza mambo mengi lakini yapo ambayo huyarudia mara kwa mara jambo linaloashilia kuna kitu hakipo sawa.

Masuala ya watumishi hewa, vyeti feki, vita ya uchumi na mafisadi pamoja na mapambano dhidi ya dawa za kulevya amekuwa haachi kuyasemea.

Unaweza kusema huenda anazungumzia maeneo aliyoyafanya tofauti na marais wengine ili kuonyesha mafanikio yake lakini miongoni mwa mambao hayo ni sugu yaliyolitesa Taifa kwa miaka mingi.

Anatilia mkazo masuala hayo ili nchi isije kurudi ilikotoka kwa kuwa sasa walau kuna mwanga unaonekana. Kwa mantiki hiyo, watendaji wakiwamo mawaziri wanapaswa kusoma alama za nyakati.

Lazima wahakikishe mambo yanayopigiwa kelele kila siku na Rais yanapatiwa ufumbuzi. Ni jambo la aibu kuona Rais anabaini uozo wakati kuna waziri, naibu waziri, katibu mkuu na hata vyombo vya ulinzi na usalama. Wakati uozo huo unatokea wahusika walikuwa wapi mpaka wasijue ajue Rais?

Wapo baadhi ya viongozi na wapambe wao kutwa wanafanya kazi ya kumsifia Rais, lakini haohao ndiyo wamekuwa wakishukiwa na kiongozi mkuu huyo wa nchi pale mambo yasipokuwa sawa.

Huu si wakati wa kuhangaika na mambo yasiyo na msaada kwa Taifa. Wajikite kupambana na yale ambayo Rais amekuwa akiyasisitiza.

Mambo ya kuinua uchumi na ujenzi wa viwanda, kuboresha huduma ya elimu, uhusiano wa kimataifa, kuepuka uamuzi wa ghafla, kushughulikia ipasavyo migogoro ya ardhi, kuboresha sekta ya afya ni miongoni mwa maeneo ya kufanyia kazi, si watendaji kusifiasifia tu.

Mfano ni kauli aliyoitoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa siku takribani sita zilizopita akiwataka mawaziri, naibu mawaziri, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya na wakurugenzi kujenga utamaduni wa kutoa taarifa za fedha za miradi ya maendeleo kwa wananchi badala ya kusubiri kufanya hivyo katika ziara za viongozi wakuu.

Aliwataka kila wanapoenda kwenye ziara ya kikazi vijijini, waelezee thamani za kazi zilizofanyika na waeleze ni lini miradi hiyo itakamilika.

0754 597315

Alibainisha wanapaswa kueleza Serikali imetoa fedha kiasi gani, kwa ajili ya kitu gani kwani kufanya hivyo kutasaidia kutoa taarifa za utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Rais Magufuli.

Kila mmoja anapaswa kutekeleza wajibu wake kwa wakati. Sidhani kama wananchi wanafurahia hatua mbalimbali wanazochukuliwa watendaji, ikiwa ni pamoja na kutumbuliwa kwa tuhuma, makosa na uzembe.

Siku za hivi karibuni Rais Magufuli alifanya ziara katika Bandari ya Dar es Salaam na maswali aliyokuwa akiyauliza wasaidizi wake walishindwa kuyajibu na kuonekana kupishana kauli, jambo hilo lilileta picha kuwa watendaji hao hawashirikiani katika utendaji wao.

Inawezekana vipi magari yaingie bandarini Waziri wa Fedha, TRA na Wizara ya Mambo ya Ndani wasijue. Ndio maana Rais anasema hamumuelewi anataka nini.

Advertisement