SAUTI KUTOKA ARUSHA: Ukuta uwe fursa Watanzania kunufaika na tanzanite

Madini ya tanzanite yalipogunduliwa na Jumanne Ngoma, ambaye hivi karibuni amezawadiwa Sh100 milioni na Rais John Magufuli, yalianza kutambulika rasmi kimaabara kati ya mwaka 1968 na 1971.

Aprili Mosi mwaka 1971, Serikali ilitaifisha migodi yote ya tanzanite Mererani na kuikabidhi kwa Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) ambayo ilianzisha kampuni tanzu ya Tanzania Gemstone Industries Ltd (TGI).

Mwaka 1972 Serikali iliunda shirika la madini ya Taifa (Stamico) na TGI ikawekwa chini ya usimamizi wake, lakini walishindwa kulilinda eneo hilo na ndilo lilivamiwa na wachimbaji wadogo.

Katika hali ya kulidhibiti eneo hilo, Julai 21 mwaka 1987 Serikali ililigawa eneo hili katika vitalu vinne kwa njia ya zabuni ambapo Kitalu A chenye ukubwa wa kilomita za mraba 0.8 ilipewa kampuni ya Kilimanjaro Mines Ltd.

Eneo la Kitalu B maarufu kama OPEC, lenye ukubwa wa kilomita za mraba 1.31 ilipewa kampuni ya Bulding Utilities na baadaye kutokana na vurugu, wakapewa wachimbaji wadogo.

Eneo la Kitalu C lenye ukubwa wa kilomita za mraba 7.6 walipewa kampuni ya Graphtan Ltd iliyokuwa na ubia na TGI na Samax na wao baadaye ndio waliuza eneo hilo kwa kampuni Afrika Kusini ya AFGEM ambayo na baadaye ililiuza kwa Tanzanite One.

Eneo la migodi ya Tanzanite One, kwa kiasi kikubwa ndilo limekuwa likisababisha migogoro hasa kutokana na kuvamiwa mara kwa mara na wachimbaji baada ya kuwa mikononi mwa wawekezaji wa nje kwa miaka 22, sasa linamilikiwa na wazawa kupitia kampuni ya Sky Associate na ubia na Stamico.

Mererani ya miaka 22 iliyopita ni tofauti na sasa, walau sasa kuna miradi mikubwa mingi ambayo imefanywa na wamiliki wapya, ikiwemo ujenzi wa hospitali, shule na miradi mbalimbali ya kijamii.

Mapato ya tanzanite nayo sasa yameongezeka. Taarifa ya Wizara ya Madini, inaeleza kuwa kipindi cha Julai 2015 hadi Juni 2016, jumla ya kilo 419,622 na caret 60,024.50 za tanzanite ghafi ziliuzwa nje dola kwa 19.64 milioni na Serikali kupata mrabaha wa Sh1.43 bilioni. Mapato haya ni tofauti na miaka 10 iliyopita.

Ujenzi wa ukuta huo wenye urefu wa kilomita 24.5, uliokuwa unafanywa na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) Ukuta huu kwa Sh5 bilioni umekamilika.

Kukamilika kwake kutasaidia kudhibiti utoroshaji wa madini na unapaswa kuwa ni faraja kwa wakazi wa Mirerani na vijiji vya jirani ambao uchumi wao unategemea madini haya.

Lakini, machimbo hayo ya tanzanite kuna vijana zaidi ya 10,000 ambao wanafanya uchimbaji na wengine kazi yao ni kuchekesha mchanga uliotolewa migodini maarufu kama ‘murere’, ambao wataathirika na hatua hizo.

Hivyo kwa masharti mapya ya kuingia katika migodi hiyo kuna idadi kubwa ya vijana wataondoka katika machimbo hayo hasa wale ambao walikuwa hawana migodi rasmi ya kuchimba.

Vilevile maagizo ya kutaka wamiliki wa migodi kuwalipa mishahara wachimbaji kila mwezi badala ya kufuata utaratibu wa zamani, kugawana madini mara baada ya kupatikana umeibua sintofahamu kuhusu hatma yao. Tayari Serikali imetangaza kuanzia sasa kuingia katika machimbo hayo ni lazima wawe na vitambulisho maalumu.

Pamoja na hayo, itoshe kutoa wito kwa serikali na wadau kuhakikisha ukuta huo unakuwa faraja kwa maslahi mapana ya Watanzania.

0754 296503