NJIA BORA ZA KUEPUKA MADHARA YA FITINA NA MAJUNGU KAZINI KWAKO

Friday May 18 2018

 

By Kelvin Mwita, Mwananchi [email protected]

Maeneo ya kazi yana watu wa kila aina na kuna msemo unaosema kwenye wengi pana mengi. Taasisi uwa zina mifumo rasmi ya kupokea, kutunza na kutoa taarifa lakini asilimia kubwa ya taarifa zinazozunguka na kutumiwa katika uwa hazipiti kwenye mifumo hii rasmi. Hii inafanya watu wengi kufungua masikio na macho yao kwenye taarifa zinazopita kwenye mfumo usio rasmi.

Viongozi katika taasisi nao ili kulinda maslahi yao hupenda pia kusikiliza nini kinazungumzwa nyuma ya migongo yao kuhusu masuala mbali mbali ikiwemo wao wenyewe. Suala hili limefungua milango inayosababisha watu kuongea maneno yanayoweza kueneza chuki na kuleta migogoro maeneo ya kazi.

Wapo watu ambao kiasili hawapendi kuona mtu yoyote yule anafanikiwa hasa katika maeneo ya kazi. Neno ‘zengwe’ limekuwa likitumika sana siku hizi katika maeneo ya kazi likimaanisha fitina zinazotengenezwa ili kumwangusha au kumkwamisha mtu katika shughuli zake. Ukitaka kufanya kitu chema na chenye maslahi kwako wapo watu wanaoweza kukuundia zengwe kuhakikisha haufanikiwi. Wakati mwingine wapo tayari kufikisha maneno ya uongo hata kwa bosi wako ili kuhakikisha tu unaonekana unasifa mbaya. Wakati unahisi kupanda cheo kunaweza kuwa furaha kwako na kwa jamaa zako wapo watu wanaotengeneza mikakati ya kukukwamisha bila sababu za msingi.

Unaweza kufanya mambo kadhaa yanayoweza kukusaidia kuepukana na madhara ya mambo ya namna hii maeneo ya kazi;

Fanya mambo yako kwa utaratibu

Mianya ya mtu kukuharibia ipo kwenye makosa madogo madogo unayoweza kuyafanya na mwisho yakatumika kama sababu ya kukuza mambo au kutengeneza mazingira ya kukujengea sifa mbaya.

Wakati mwingine kwa makusudi wapo wanaoweza kukutengenezea mitego inayoweza kukufanya ukajikuta kwenye matatizo bila kutarajia. Njia rahisi ya kuliepuka hili ni kuhakikisha mambo na shughuli unazofanya zinafuata taratibu, miongozo na sheria.

Unajua kabisa ili kupewa ruhusa ni lazima watu wawili waridhie kwa kuweka saini zao; hakuna haja ya kuondoka ukijua fika idadi haijatimia. Kunguru muoga huishi siku nyingi.

Tenda wema na kuwa mkweli

Ubaya siku zote unashindwa kwa wema hivyo hivyo uogo unashindwa kwa ukweli. Jifunze kutenda haki na kusema ukweli na kuusimamia pia. Kuna wakati itakubidi kutoa hesabu ya maneno na matendo yako.

Ukiwa mtu wa kuonea wengine na kutokuwa mkweli ni rahisi watu kukujengea mipango yenye nia mbaya ya kukuangusha ikiwa ni pamoja na maneno ya uongo juu yako ili kuhakikisha unaonekana mbaya kwa wengine na haufanikiwi katika mambo yako.

Kuna watu ambao wamefanikiwa sana kwenye hili kiasi kwamba hata ukiwatengenezea maneno ya uongo kuwakwamisha kuna watu kwa hiari yao bila kushawishiwa watasimama kuwatetea.

“Kwa kweli labda mtu mwingine lakini John hawezi kufanya hicho kitu” kauli kama hizi wala sio ngeni. Jenga mazingira ya kuaminika kwa kutenda haki na kuwa mkweli siku zote.

Kuwa makini na nyaraka

Katika maeneo ya kazi matumizi ya nyaraka yamewaponza watu wengi sana hasa pale yanapotumiwa kama ushahidi. Jifunze kutambua umuhimu wa kila nyaraka, soma na elewa matumizi yake.

Wapo ambao walijikuta katika wakati mgumu hasa katika kutumia nyaraka za ofisi. Ni vyema kukumbuka kutunza nakala za nyaraka unazozithibitisha na kuthibitishiwa pia.

Kama kuna nyaraka inayokutaka kuiidhinisha hasa kwa kuweka saini yako ni vyema kuhakikisha kuwa unabaki na nakala walau moja ya kukulinda pale itakapotumiwa ndivyo-sivyo au kupotea.

Mtu mmoja aliwahi kunisimulia kisa cha kuandikiwa barua ya onyo kwa kutokuwepo eneo la kazi pamoja na ukweli kwamba alikuwa na ruhusa ya kufanya hivyo.

Baada ya kusainiwa ruhusa na mkuu wa idara aliyekuwa akikaimu ilionekana mkuu wa idara huyo hakuwa na mamlaka ya kufanya hivyo na mwisho wa siku kesi ikamrudia aliyepewa ruhusa ambae alishindwa kuthibitisha kuwa aliyekaimu aliidhinisha ruhusa yake kwa sababu alipoteza fomu ya rushusa.

Tafuta ushauri na msada kwa wengine

Kuna kipindi inafika mahali ujikuta upo njia panda katika kutoa maamuzi au kufanya jambo fulani na pengine sababu kubwa ni kutokuwa na uhakika au kutukuwa na taarifa sahihi.

Usikubali kuingia kwenye mtego wa kujaribu ikiwa unaweza kupata msada kutoka kwa wenye taarifa sahihi au uwezo wa jambo husika.

Endapo utafanya maamuzi yanaweza kukuweka matatani ni rahisi zaidi kwa mtu au watu kukuundia zengwe na kuhatarisha kibarua chako. Ujuaji wa kupita kiasi pia ni hatari; usidhani kuwa unaweza kujua kila kitu. Jifunza kujifunza kutoka kwa wengine.

Tambua kuwa ni lazima watu wataongea

Ukifanya vibaya watu watakusema vibaya na ukifanya vizuri bado wapo watakao kusema vibaya pia. Ukionyesha ukaribu na mtu fulani ofisini kwako wapo watakao sema unajipendekeza au unamaslahi binafsi.

Ukiamua kuendelea na mambo yako kivyako vyako wapo watakaosema unaringa na kujiona bora kuliko wengine.

Hii ni kawaida ya sisi binadamu na hautakiwi kupata msongo wa mawazo eti kisa tu kuna watu wanakusema vibaya kwa kufanya vizuri.

Chuki na wivu ni vitu vilivyokaa ndani ya baadhi ya watu hivyo ni vyema kukumbuka kuwa hata usipofanikiwa kazini hao hao wanaokusema kuwa una kihelehele kwa kujifanya hodari watakusema kwa kuwa mvivu na mtu usiyejituma.

Jifunze kukubali kuwa wewe ni watofauti na kuna muda utafanya jambo au mambo ambayo pengine hayatawafurahisha wengine hata kama ni mazuri.

Usikubali maisha ya kazini kwako ya kawa na kero zisizo za lazima kama maneno ya watu.

Kelvin Mwita ni Mhadhiri Chuo Kikuu Mzumbe, anapatikana kwa 0659 081 838, [email protected], www.kelvinmwita.com

Advertisement