MAONI YA MHARIRI: Tutoke sasa kujadili yaleyale kwenye kilimo

Friday May 18 2018

 

Baada ya mjadala moto wa siku mbili kuhusu hotuba ya Wizara ya Kilimo hatimaye juzi, Bunge lilipitisha bajeti yake.

Bajeti iliyopitishwa imeitengea sekta ya kilimo Sh170.2 bilioni, kiwango ambacho ni pungufu kwa asilimia 23 ikilinganishwa na ya mwaka 2017/18 iliyotengewa Sh221 bilioni.

Kama ilivyokuwa katika mjadala wa mwaka jana na hata miaka ya nyuma, mjadala wa mwaka huu ulijikita katika mambo yaleyale ambayo wabunge wamekuwa wakiyapigia kelele kila msimu wa bajeti.

Masuala kama bajeti ndogo inayotengwa, uhaba na ucheleweshwaji wa pembejeo kama mbolea na zuio la kutouza mazao nje sio mageni katika vinywa vya wabunge na hata wadau wengine wa kilimo. Lakini kinachoonekana ni kuwa kilio chao kimekosa msikilizaji.

Ndio maana wabunge kama Hussein Bashe (Nzega Mjini), Nape Nnauye (Mtama), Richard Ndassa (Sumve), Joseph Musukuma (Geita Vijijini) na wengineo waliamua kuwa mbogo wakifikia hatua ya kutaka bajeti hiyo isipite.

Haiwezekani kila mwaka wa bajeti, mijadala bungeni ihusu wawakilishi wetu kushupalia ucheleweshawaji wa pembejeo au kuzuiwa kwa wakulima kuuza mazao yao wanakotaka.

Angalau Serikali baada ya mjadala mkali, imeridhia wakulima kuuza mazao ya nje lakini tukiwa ni Taifa linalojali sekta hii nyeti na nguzo muhimu ya uchumi wa nchi, huko tulipaswa kuwa tumeshatoka.

Kwa sasa na kwa kadri miaka inavyokwenda, mijadala kuhusu kilimo ilipaswa kujikita katika aina za teknolojia za kisasa za kutumia katika kilimo, mazao ya kutiliwa mkazo ili kuteka soko la kimataifa, elimu ya kisasa kwa wakulima na kukuza wigo wa maeneo zaidi ya kilimo hasa kile cha umwagiliaji.

Kuendelea kujadili masuala yaleyale kwa miaka nenda rudi ni dalili kuwa kama nchi bado tuna safari ndefu kuelekea kwenye mafanikio ya kweli kwenye sekta ya kilimo.

Hii ni sekta inayoelezwa kuwa ndio uti wa mgongo wa uchumi wetu huku ikihusisha zaidi ya asilimia 70 ya wananchi wa Tanzania wanaojishughulisha na kilimo, lakini kwa masikitiko bado inatengewa bajeti isiyotesheleza mahitaji hasa eneo la fedha za miradi ya maendeleo.

Mwaka huu Serikali imepanga kununua magari malumu kwa ajili ya kutembea vijijini kupima udongo. Tunachojua kiuzoefu ni kuwa suala la upimaji wa udongo linaweza kushughulikiwa kikamilifu hata kwa ngazi ya halmashauri kwa kuwawezsha maofisa ugani kuwa na vifaa vya kupima udongo na kuwashauri wakulima mazao ya kulima kulingana na aina ya udongo na virutubisho vilivyomo.

Ni vifaa ambavyo bajeti yake hata kijiji achilia mbali halmashauri au wilaya kinaweza kuvimudu na hatimaye kuwasaidia wakulima wengi wanaoendesha kilimo cha mazoea.

Hatuoni namna dira ya Tanzania ya uchumi wa kati utokanao na maendeleo ya viwanda inavyoweza kutekelezeka ikiwa sekta muhimu ya kutufikisha huko inatengewa fedha kiduchu za maendeleo.

Tungetenga fedha za kutosha, leo tungekuwa tunafanya mijadala tofauti na iliyopo sasa. Badala ya kujadili madeni ya wasambazaji wa pembejeo, leo wabunge wangekuwa wanajadili masuala kama vile teknolojia za kuboresha kilimo, fursa za masoko kimataifa na namna ya kukuza wigo wa mazao ya biashara tofauti na mazao yaleyale tuliyorithi kutoka kwa wakoloni.

Advertisement