MAONI: Utapiamlo ukidhibitiwa Tanzania itaondokana na umasikini

Friday May 18 2018

 

By Elias msuya

Utapiamlo unahusisha ukosefu wa virutubisho mwilini au kuongezeka kwa virutubisho hivyo bila sababu za msingi.

Ukosefu wa virutubisho mwilini husababisha uzito kupungua, kudumaa na upungufu wa kinga mwilini.

Wataalamu wa tiba lishe wanasema upungufu huo husababishwa na kutokula chakula cha kutosha au kula chakula kisicho na virutubisho vya kutosha vikiwamo vya nishati, protini, vitamini na madini ambayo mwili unayahitaji kwa ajili ya kuimarisha afya.

Ukosefu huo unaweza kusababishwa na maradhi, matunzo mabaya kwa watoto hasa wakati wa kula chakula, uchafu na kutopatikana kwa huduma bora za afya na majisafi na salama.

Hata hivyo, inaelezwa pia kuongezeka kwa virutubisho mwilini husababishwa na kula chakula kingi kuliko kile kinachohitajika, hivyo kumfanya mtu kuongezeka uzito na kutokwa na kitambi. Tabia hii huleta hatari ya shinikizo la damu, kisukari, maradhi ya moyo, kiharusi na saratani.

Takwimu za Tanzania Demographic Health Survey za mwaka 2016 zinaonyesha hali mbaya ya lishe nchini, jambo linalopaswa kuangaliwa upya na Serikali na wadau ili kupambana nalo.

Katika unyonyeshaji wa watoto, inaonekana asilimia 57 ya wenye umri kati ya 0 hadi miezi sita hawanyonyeshwi vya kutosha na mama zao. Vilevile inaonekana asilimia 57 ya watoto walio chini ya miaka mitano wana upungufu wa damu, huku asilimia 45 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wakiwa na upungufu huo wa damu.

Inaonekana pia asilimia 37 ya wanawake wa mjini hasa Dar es Salaam wenye miaka kati ya 15 na 49 wana uzito uliozidi, huku asilimia 36 ya wanawake wenye umri huo wakiwa na upungufu wa madini ya iodine na asilimia 34 ya watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano wamedumaa ilhali asilimia 33 ya watoto kama hao wana ukosefu wa vitamini huku asilimia 14 wakiwa na uzito pungufu.

Hii ni hali mbaya kwa sababu matokeo yake yanaiathiri nchi kiuchumi na kijamii. Kwa mfano, utapiamlo ndiyo chanzo kikuu cha watoto kudumaa na mwisho kusababisha mtoto huyo kuelekea kwenye umaskini.

Hiyo ni kwa sababu udumavu huathiri ukuaji wa mwili na akili, hivyo kumfanya mtoto kuwa mjinga, asiyefundishika na kupata matokeo mabaya darasani na mwisho wake hataweza kuzalisha kiuchumi.

Utapiamlo huambukiza kizazi na kizazi, kwani wajawazito waliodumaa nao huzaa watoto wenye uzito mdogo. Kwa mujibu wa wataalamu, watoto hao hawana kinga za kutosha kupambana na maradhi.

Wasichana wanaojifungua wakiwa na uzito mdogo hupata matatizo wakati wa kujifungua. Utapiamlo hupunguza kinga za mwili za kupambana na hata na maradhi ya kawaida tu, jambo linalosababisha vifo vya watoto 130 kwa siku nchini.

Kutokana na tishio hili, Serikali na wadau wanapaswa kuwekeza kwenye lishe ili kukuza uchumi wa nchi.

Takwimu za Profiles za mwaka 2014 zinaonyesha ifikapo mwaka 2025 kama Tanzania itaondokana na upungufu wa madini ya iodine, itaongeza uzalishaji wa uchumi kwa kiasi cha Sh750 bilioni.

Vilevile, zaidi ya watoto 120,000 walio chini ya miaka mitano wanaodumaa kila mwaka wataokolewa, athari kwa watoto wapatao 800,000 walioathiriwa ubongo kwa kukosa madini ya iodine nayo itapungua.

Pia, idadi ya vifo vya wanawake 15,000 na watoto 72,000 kila mwaka itapungua, vifo vya watoto 85,000 wanaokufa kwa kukosa maziwa ya mama kila mwaka vitapungua na hali ya watoto 101,000 walio na umri chini ya miaka mitano wanaokosa vitamini itapungua.

Ili kuondokana na hali hii mbaya, kila mkoa unatakiwa kuwekeza kwenye lishe ya watoto hasa walio chini ya miaka mitano na akina mama na wasichana. Jitihada zinahitajika zaidi kuimarisha lishe katika afya, kilimo, maji na maendeleo ya jamii.

Kwa mfano, wakuu wa mikoa na wilaya wanapaswa kuhakikisha kila kaya inakuwa na shamba lenye mazao yaliyorutubishwa kama viazi lishe, muhogo na ya mikunde.

Maofisa lishe wilayani wanapaswa kuhakikisha akina mama wanakwenda kliniki ili kupima hali za lishe za watoto wao na kuwahimiza kunyonyesha kwa kufuata utaratibu.

Lakini wajibu huo unapaswa kutekelezwa pia na familia.

Nasema hivyo kwa sababu, kama wataalamu watajitokeza kutoa elimu kwa jamii, ni vyema ikatilia maanani kuitekeleza kwa vitendo ili nchi iepukane na tatizo hili kubwa la udumavu na utapiamlo.

Elias Msuya ni mwandishi mwandamizi wa Gazeti la Mwananchi

Advertisement