Asilimia 90 ya wanawake wenye uwezo sawa na wanaume hupanga siku za kujamiiana

Sunday January 14 2018

 

By Kalunde Jamal, Mwananchi [email protected]

Wanawake wenye nguvu ya maamuzi na wenye fedha wanaelezwa kutoona umuhimu wa ngono na kuwapangia wenza wao siku za kujamiiana.

Hilo limebainika katika utafiti uliofanyika hivi karibuni na Jarida la Match’s Singles la nchini Marekani, kwa kushirikiana na wataalamu wa saikolojia kutoka katika baadhi ya vyuo vikuu nchini humo.

Utafiti huo uliohusisha watu 5,000 kutoka katika mabara kadhaa ikiwamo baadhi ya nchi za Afrika zikiwamo Tunisia, Mauritius na Swaziland umebainisha kuwa harakati za mwanamke kujikomboa kiuchumi na kifikra umebadili kabisa dhana nzima ya mapenzi kwa wapenzi na wenza.

Jarida hilo limefafanua kuwa kwa kiasi fulani mabadiliko hayo hayajawafurahisha baadhi ya wanaume hususani waliokuwa wakiwatumia wanawake kingono kwa ujira wa fedha na ahadi mbalimbali.

Katika utafiti huo uliochapishwa katika majarida mbalimbali ya familia yakiwamo Your Family Tree, Ebony, Family Office Magazine na Look-In, ulibaini asilimia 37 ya wanaume na asilimia 47 ya wanawake wanafurahia wanawake kuwa na nguvu sawa na wanaume katika uhusiano wa kimapenzi na kiuchumi.

Ilibainika asilimia 35 ya wanaume waliohojiwa katika utafiti huo walisema wanawake kuwa na nguvu, nafasi sawa na wanaume katika jamii kumefanya uhusiano wa kimapenzi kati yao kuwa mgumu.

Unaeleza asilimia 43 walisema wanawake kuwa na nguvu katika uhusiano wa kimapenzi ina maana nyingi tofauti na kupendana wawili waliooana.

“Mwanamke akiwa nguvu sawa na mwanaume katika familia au uhusiano wa kimapenzi, kuna mambo mengi, wana sifa ya kutunza fedha, wanajua kuunganisha familia, wavumilivu, hizo ni miongoni mwa faida, lakini pia ni wachapakazi wakipata nafasi ya kufanya hivyo,” alisema Connie Shehan Profesa wa masomo ya jamii na wanawake kutoka Chuo Kikuu cha Florida.

Alisema usawa katika maamuzi ya ngazi ya taifa, jamii na familia huleta mapenzi zaidi ya watu wanavyodhani, kuliko uhusiano ukiwa tegemezi wa upande mmoja, huwa na manung’uniko yasiyo na majibu.

“Wanawake kuwa na nguvu katika uhusiano haimaanishi wataacha kuwa na ile asili ya kike, itabaki isipokuwa watakuwa na nafasi ya kushiriki katika kufanya maamuzi, na hilo ndiyo gumu kukubaliwa na wanaume wengi ndiyo maana wanaona imekuwa taabu kuwa nao, ” alisema Profesa Shehan. Alisema mabadiliko ya usawa kwa wanawake na wanaume kwa kiasi fulani yameleta faida, kwa sababu wapo wanaume leo wanawasaidia wanawake kazi zao.

Utafiti huo pia ulibaini kuwa asilimia 90 ya wanaume walisema haki sawa kati ya jinsi hizo mbili inafanya mambo mengi kuwa magumu na kusababisha wao kunyanyasika.

Naye mtaalamu wa masuala ya jamii kutoka Chuo Kikuu cha Jimbo la New York Brockport, Profesa Bridges Tristan alisema kuwepo kwa usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kufanya kazi, kumiliki mali, kulipia gharama za familia si suala linalolalamikiwa na wanaume.

Alisema wanaume wanacholalamikia ni kutopata nafasi ya kuwakandamiza wanawake kwa sababu moja ama nyingine ikiwamo ya kiuchumi ambayo ilikuwa ni kikwazo cha kufikia malengo yao.

“Hapa kuna mambo mawili, asilia ya mwanamke kuwa chini ya mwanaume na mwanamke mwenye nguvu ya kufanya maamuzi, lakini bado yupo chini ya mwanaume.

“Wanaume wanaona karaha kuwa na wanawake wenye nguvu, waelewa wa mambo, wanaoweza kujenga hoja, wanaojulikana ndani ya familia na nje kwa juhudi zao, bila kujali wapo chini yao au laa.

Alisema linapokuja suala la mapenzi, wanawake wenye uwezo wa kifedha na upeo wa kuzitafuta, wameelekeza nguvu, akili huko na kuchukulia mapenzi kama kitu cha kawaida.

“Ukiangalia wanawake wasiokuwa na uwezo wa kifedha, hutumia muda mwingi kuwaza kuhusu wapenzi wao wakitamani wawafanyie hili na lile, si kama wanapenda, bali ndiyo silaha pekee waliyobaki nayo.

“Wakikubali makosa hata yasiyo yao, tofauti na anayetafuta fedha hata kama atakubali kosa ni kwa sababu ni mwanamke ameumbwa hivyo kiasili, lakini ataendelea kufanya maamuzi mengine, hatarudi nyuma kamwe,” alisema Profesa Tristan.

Alisema wanawake hujisikia faraja wanapokuwa na uwezo wa kushiriki mijadala, kufanya kazi, kufanya biashara kwa sababu huamini wamekuwa sawa na wanaume, huku wakichukuliwa tofauti na kuonekana ni walioweza kutokana na karne na karne kuonekana ni watu wanaohitaji kusaidiwa ili wafike mahali fulani.

Profesa Shehan alisema kila jambo zuri lina changamoto zake, kubwa waliyobaini katika uchunguzi mdogo waliofanya katika utafiti huo ni wanawake walio na nguvu ya kufanya maamuzi, wana tabia tofauti wakati wa kujamiiana.

Alisema wanawake wa namna hiyo asilimia 95 hutaka kutawala suala la kujamiiana, hupanga siku ipi ashiriki na siku gani asiguswe.

Ilibaini kuwa asilimia 90 ya wanaume walitaka wanawake waanze kuwabusu na waonyeshe kutamani kujamiiana nao, huku asilimia 92 ikiona hilo si jambo la busara na anayepaswa kufanya hivyo ni mwanaume.

“Si wanaume wote wanaoweza kushughulika na mpenzi ambaye ana nguvu na haogopi kusema kile anachopenda, maoni yake ni nini ambayo inaweza kuwa changamoto,” Shehan alisema.

Shehan alisema wamebaini kuwa tofauti na siku za nyuma, wanawake sasa wana uwezo wa kuhoji pale wanapoona wanaonewa hususani katika suala la uhusiano, badala ya kulia na kulalamika.“Kweli wanafanya maamuzi ya kuendelea au kuachana na uhusiano usiokuwa na faida upande wao, hili limejitokeza uhalisia wake baada ya kupata nguvu ya kushiriki masuala mbalimbali sawa na wanaume, ”alisema.

Matokeo ya ziada yalionyesha asilimia 78 ya wanawake wa namna hii hulipia gharama wanapotoka na mwanaume mwenye lengo la kuwa na uhusiano naye wa kimapenzi kwa mara ya kwanza.

Advertisement