Baraza jipya la Rais Kenyatta lasababisha mgawanyiko Jubilee

Sunday January 14 2018

 

Je, ni moto unawaka chini ya viti vya Rais Uhuru Kenyatta na Naibu wake William Ruto au ni uvumi tu kutoka kwa wanasiasa wanaomba usiku na mchana wawili hao wakosane ili ndoto ya makamu wa rais ya urais 2022 isije ikatimia?

Kwa wiki moja sasa tangu Rais Uhuru atangaze kikosi chake kitakachounda Baraza la Mawaziri, kauli za wanasiasa na wananchi wa kawaida zimekuwa zikibainisha kuhusu kuzorota kwa uhusiano kati ya Uhuru na Ruto.

Hali hiyo inachipuka kutokana joto la kisiasa kuhusu ni nani atakayemrithi Rais Uhuru inatishia kutawala ulingo wa kisiasa hata kabla ya kiongozi wa nchi kumaliza kufungasha virago ili safari yake ya muhula wa pili ing’oe nanga.

Rais Uhuru amesema zaidi ya mara 10 kuwa atamuunga mkono Ruto 2022 kuwania urais kama ishara ya kumshukuru kwa kumuunga mkono 2013 na mwaka 2017.

Hata hivyo, kuna wanasiasa wasiomtakia mema Ruto na wanajaribu kuweka vizingiti kwenye ndoto zake za kumfanya Rais wa saba wa Kenya.

Uhuru alipotangaza majina ya watu watakaounda Baraza lake jipya la mawaziri wiki jana, makamu wake Ruto hakuwapo. Hili liliibua kivumbi cha maneno kuhusu ni kwa nini wanasiasa hao wamebadilisha mtindo wa kufanya kazi. “Hii si kawaida kabisa,” wengi walisema. Uhuru na Ruto wana mazoea ya kufanya mambo yao pamoja tangu 2013. Wamekuwa wakitekeleza masuala ya kitaifa pamoja na kuleta taswira ya viongozi wanaoelewana, kuaminiana na kupendana kama chanda na pete. Wakati mwingi, walivaa mavazi yanayofanana wakati wanahutubia taifa au wanapotangaza jambo. Kwa hivyo, Wakenya wengi walianza kuhoji mahali alipo, hadithi za chanda na pete kutoachana zikatoweka.

Uhuru na Ruto huenda wamefika kwenye njiapanda ya maisha yao ya kisiasa. Baada ya muhula huu wa pili kukatika 2022, Uhuru hawezi kukubaliwa kisheria kuwania urais tena.

Baadhi ya vyombo vya habari vilisema Ruto alikosa kufika ikulu kuungana na bosi wake wake wakati akisoma majina mawaziri wake wapya kwa sababu hakufurahishwa na hatua ya Uhuru ya kuwaondoa mawaziri ambao wangemsaidia (Ruto) kushinda urais 2022.

Lakini huenda hayo yakawa si ukweli. Hii ni kwa sababu miongoni mwa mawaziri waliobakizwa na Uhuru ni Charles Keter (Kawi). Huyu ni rafiki mkubwa wa Ruto. Rais pia alitangaza majina matatu ambayo ameyapendekeza kuunda Baraza la Mawaziri, mmoja wao ni aliyekuwa gavana wa Kaunti ya Wajir, Ukur Yatani ambaye pia ni rafiki wa makamu wa Rais.

Sasa uadui ulitokea wapi ilhali rafiki zake wamejumuishwa kwenye Baraza jipya la mawaziri? Pengine Ruto anataka kuwa na mamlaka ya kuwateua mawaziri wapya pamoja na Rais. Duru za kuaminika zinasema watu fulani wenye ushawishi mkuu katika uteuzi wa mawaziri wapya walitupilia mbali orodha ya majina yaliyopendekezwa na Makamu wa Rais, jambo lililomuudhi mno na kumfanya kuamua kushinda mchana kutwa kwenye ofisi yake iliyoko katika barabara ya Harambee na kujipatia shughuli huku Rais Uhuru akitangaza mabadiliko katika Baraza la Mawaziri, wakuu wa polisi na idara ya ujasusi.

Lakini, Makamu wa Rais amepuuza gumzo hilo kwenye Twitter akisema wanasiasa wa Jubilee hawana budi kujitenga na siasa za kupotosha kuhusu 2022.

Msemaji wake David Mugonyi aliwashangaza Wakenya alipotishia kutumia ushawishi wake serikalini kuhakikisha kwamba mwanahabari aliyeandika habari kwamba Ruto ametengwa na Uhuru, amefutwa kazi mara moja.

Mugonyi alisema kinyume na habari kwamba Ruto alikuwa ofisini Uhuru alipokuwa akitangaza majina ya mawaziri wapya, ni uongo mtupu. Alisema Ruto alikuwa nje ya nchi tangu mwaka jana.

Habari zisizothibitika zinasema kwamba Ruto hajafurahia uwezekano wa wanasiasa wa chama cha Kanu kupata vyeo katika Baraza la Mawaziri. Mwenyekiti wa Kanu, Gideon Moi amekana madai hayo akisema ametosheka kuhudumu kama Seneta wa Kaunti ya Baringo. Tangu utotoni, Uhuru na Gedion wamekuwa marafiki wa karibu kwa sababu baba zao – Mzee Jomo Kenyatta na Daniel arap Moi walikuwa Rais na makamu wa Rais mtawalia.

Pia, kila anapokuwa na changamoto ya uongozi, Uhuru na mamake Mama Ngina Kenyatta humtembelea Mzee Moi nyumbani Kabarak au Nairobi kutafuta ushauri. Katika ziara hizo, Uhuru humwacha Ruto nyuma na kupalilia uvumi kwamba huenda Uhuru anapania kumrudishia Mzee Moi asante kwa kumfanya mrithi wake 2002 alipostaafu.

Uhuru na mamake wanajua bayana kuwa wana deni la kisiasa la Moi na wangependa kulilipa 2022 kwa kumpiga debe Gideon.

Mnamo Januari 9 mwaka huu, maseneta wa Jubilee walimchagua Gideon kuwa mwenyekiti wa Kamati ya Seneti ya ICT, yaani Habari, Mawasiliano na Teknolojia. Wahenga walisema penye moshi hapakosi moto. Tunaona dalili ya moshi kati ya uhusiano wa Uhuru na Gideon. Ikiwa wanasiasa wa Kanu watapewa nafasi katika Baraza jipya la mawaziri, wengi wataona hali hii kama mpango wa kumtayarisha kitinda mimba huyu wa Rais Mstaafu kumrithi Uhuru.

Lakini hii haitakuwa jambo geni. Historia ya kisiasa katika nchi hii imesheheni uvunjaji wa mikataba ambao huleta hisia za usaliti kati ya aliyeahidiwa na aliyeahidi.

Mnamo 1997, Rais Moi alimpuuza Makamu wake wa muda mrefu (miaka 13), Profesa George Saitoti na kumteua Uhuru kuwa mrithi wake. Ingawa Uhuru hakushinda urais mwaka huo, Moi hakupata lepe la usingizi hadi mwana wa Mzee Kenyatta aliposhinda urais 2013.

Hata hivyo, wengine wanahofia yasije yakajitokeza yaliyomkuta Raia Odinga. Mnamo 2002, mwanasiasa mkongwe, Raila Odinga alimuunga mkono Rais Mwai Kibaki na aliposhinda urais, kiongozi huyo katika mkataba maalumu akamuahidi Raila kwamba atamuunga mkono mwaka 2007 kupigania urais. Lakini yaliyofanyika matukio ya 2007 yanajulikana. Kibaki alimwacha Raila kwenye ‘stesheni ya reli’ na kutoroka na urais.

Haikuwa vigumu kwa Kibaki kumwinda atakayeamini uongo wake wa mikataba na uungwaji mkono. Kalonzo Musyoka alikubali kuwa naibu wake akiamini kwamba mkataba waliosaini ambapo Kibaki alikubali kumpigia debe 2013 ingetimia, lakini wapi! Kalonzo aliachwa kwenye mataa akishangaa shetani gani alimdanganya hadi akaamini maneno ya Kibaki.

Nini kitamfanya Uhuru asizingatie haki za walio wengi na kumpigia debe Ruto? Hili swali litajibika baadaye.

Mbali na hayo, baadhi ya wanasiasa wa Kenya ya Kati ambapo Uhuru anatoka wameongeza mafuta kwenye moto. Mbunge wa Nyeri Mjini Ngunjiri Mbugua amesema si lazima eneo lake limuunge mkono Ruto 2022.

Matamshi haya ya siku chache zilizopita, si mapya. Viongozi wengine wa eneo hili wamesema hawatakubali kushinikizwa na mkataba kati ya Uhuru na Ruto na kulazimishwa kumpigia kura makamu wa rais 2022.

Pengine kwa kuona aibu, baadhi ya wanasiasa wa eneo hili wamejitokeza wakiwataka wanasiasa wanaorusha maneno kuhusu 2022 wakome kabisa.

Baadhi yao wamemhusisha Raila na mgogoro huo kwa kudai kuwa wale wanaopinga mkataba kati ya Uhuru na Ruto wametumwa na kiongozi huyo wa Nasa kwa lengo la kusababisha migawanyiko katika chama cha Jubilee.

Uhuru amewatimua mawaziri 13 kutoka katika Baraza la Mawaziri. Rais amejikuta pabaya kwa kubakisha wanaume pekee kwenye Baraza hilo. Wanawake wamemshutumu kwa kupuuza mchango wa jinsia katika ujenzi wa taifa.

Lakini kwa vile Baraza la Mawaziri halijapata mawaziri wa kutosha (nafasi 22). Nafasi 13 zimesalia na Uhuru bila shaka atawateua wanawake.

Advertisement