Erica anavyomwimbia Mungu na kuendeleza ujasiriamali

Muktasari:

  • Anasema baada ya kuhitimu uandishi, alifahamu kwamba suala la kupata ajira ni gumu hivyo aliamua kujaribu maisha kwa njia tofauti ambayo pia alifahamu kwamba ni changamoto kwake kutokana na kukosa ujuzi.

Aricah Fungo (27) ni mwimbaji wa nyimbo za injili na afisa mauzo wa Gombo Tv, wilayani Nyamagana jijini Mwanza.

Anasema baada ya kuhitimu uandishi, alifahamu kwamba suala la kupata ajira ni gumu hivyo aliamua kujaribu maisha kwa njia tofauti ambayo pia alifahamu kwamba ni changamoto kwake kutokana na kukosa ujuzi.

“Nilimuomba mjomba wangu mkopo ili kuanza biashara ndogo ndogo. Nilianza kwa kununua baadhi ya bidhaa kutoka jijini Dar es Salaam na kupeleka Mwanza. Nilikuwa nachukua vitambaa za kushona na mawigi ya nywele na kuwapelekea wateja wangu mkoani Mwanza. Nilipata faida ingawaje sio sana,” anasema.

“Pia nafanya kazi katika kituo cha matangazo cha Gombo kama afisa mauzo na ninaimba nyimbo za kumsifu na kumuabudu Mungu zinazoakisi safari ya maisha yangu,” anasema.

Anaeleza kwamba tangu akiwa mdogo, hakuwahi kuwaza kuhusiana na sanaa ya kuimba lakini amejikuta akiimba na kukubalika na watu wengi hususan waumini.

Anasema huu ni wito ambao ni lazima aitike katika kutekeleza wajibu wa kiroho.

Arica anatamba na nyimbo mbili ambazo ni Mipango na Daima na lengo lake ni kuhakikisha kwamba anatoka na albamu ya nyimbo kumi kabla ya Julai mwaka huu,chini ya Famara Promotions inayomilikiwa na Fanuel Fabian.

Je, unamudu?

Anasema anahakikisha kwamba kila kitu kinaenda kwa mujibu wa mipangilio na kwamba shughuli zote zinaendeshwa kulingana na ratiba husika.

“Kusimamia mradi au shughuli ya mauzo ndani ya mikoa sita ya Kanda ya Ziwa si kazi rahisi lakini kwa kuwa kila kitu na wakati wake, nahakikisha kwamba naweka mabo sawa na ikifikia hatua ya kuimba naenda studio na kama ni kazini, nazunguka kama inavyotakiwa kuhakikisha kwamba kazi inaenda sawa,” Arica.

Kwa sasa Arica, ametenga siku za wengine kama sehemu ya muda wake wa kumtumikia Mungu.

Mbali na nafasi yake kama meneja masoko Aricah bado anajihusisha na shughuli ya ujasiriamali. Anaagiza mafuta ya alizeti kutoka mkoani Singida na kusafirisha hadi jijini Mwanza na kuwauzia wateja wake.

Anasema ujasiriamali huo umemsaidia kutekeleza na kutimiza baadhi ya ndoto zake kama vile kununua kiwanja na kujenga nyumba.

Kujichanganya na aina yote ya watu bila kujali jinsia wala rika, watu wengi huitafsiri kwa mitazamo mbali mbali ila neno ‘mhuni’ likipewa uzito zaidi.

“Mimi mbali na watu ninaofanya nao kazi, hadi mitaani najichanganya na watu wa aina zote ili kubadilishana mawazo ya kijasiriamali na kufahamu mambo mbali mbali yakiwemo ya kijamii, lengo ni kupata uelewa mpya ambao unanisaidia katika biashara zangu na utunzi,” Arica.

Anasema kutokana na kujiamini kwake kama mwanamke shupavu, anavumilia tu na hana daima anajichunga ili asije akawa mfano mbaya kwa jamii.

Anatoa wito kwa vijana wenzake hususan wa kike kuendelea kutafuta maisha kwa njia halali kwani hakuna hatua inayoanza na moja, bali sifuri.

Anasema enzi za kukaa nyumbani na kusubiri ajira hata baada ya kumaliza masomo, imepitwa na wakati kwa kuwa takwimu za watu wanaostaafu na wanaohitimu masomo katika vyuo, haziendani kamwe, hivyo basi, lazima vijana wawe na jicho la tatu la utafutaji katika kuendana na hali halisi ya maisha kwa sasa.