Je, una kiu na ndoa yenye mafanikio?

Sunday February 18 2018

 

Malengo yako ya maisha na ndoto zako lazima ziwe na uhusiano na ndoa unayoitaka au uliyonayo.

Usifunge ndoa kwa ajili ya watoto, kwa ajili ya tendo la ndoa au kwa ajili ya kupata mtu utakayekuwa naye karibu.

Ikiwa umefunga ndoa kwa miaka mitatu au minne na umebaki palepale kimaisha na kimtazamo basi utakuwa haujajua malengo yako au labda unaishi na usiyestahili kuwa naye kwa sababu Mungu wetu ni wa kuzidisha na sio kupunguza. Hauingii kwenye ndoa ukaue maono yako bali ukayaongeze na kunyanyua juu.

Ongelea ndoto na malengo ya maisha yako ukiwa na marafiki zako. Katika ngazi ya urafiki au uchumba penda sana kuongelea ndoto zako au maono yako na huyo unayempenda ili kujua kama ndoto zenu ni halisi na je hazina migongano au tofauti kubwa?

Kwa nini ninafunga ndoa?

Kabla sijamaliza mafundisho haya naona ni vyema nikikusaidia kufahamu sababu mbaya za kuingia kwenye ndoa. Nimesema awali kwamba watu wengi wanaingia kwenye ndoa kwa sababu binafsi na pasipo kujiuliza maswali flani flani.

Mtu akishasikia hisia za kusisimka na kuhisi anampenda kijana au dada flani anahisi basi niko tayari kuishi naye maishani kama mume na mke kumbe hiyo sio sababu yamsingi.

Kutokufahamu sababu hizi kumesababisha maumivu na majuto mengi baada ya ndoa nyingi kuvunjika huku mmoja akiwa anampenda mwenzake na mwingine anamwona mwenzake kama shetani, kumbe kamwe hakuwahi kumpenda ila alisukumwa na mazingira fulani kuingia kwenye hiyo ndoa.

Sababu ni hizi

Kuingia kwenye ndoa ili kutafuta kusaidiwa. Usijaribu kuwa na lengo la kufunga ndoa kwa ajili ya kupata msaada, aidha inaweza kuwa msaada wa kijamii au kifedha. Tunaoa ili tutimize malengo sio kupokea msaada.

Kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya umri. Hatuoi kwa sababu ya umri, umri sio tiketi ya kufunga ndoa.

Unaweza kuhamaki sana kwa sababu unaona umri wako umeenda (hususani wanawake) mara ukija kumpata mtu ambaye umeamua kukurupuka naye unakuja kujuta zaidi ya ulivyokuwa peke yako.

Angalia vigezo vya msingi kwa mke au mume na sio umri wake au umri wako. Kupevuka kiakili na kihisia hakusababishwi na umri.

Unaweza ukaolewa na mtu ana miaka 40 lakini bado anawaza na kufikiri kama mtoto.

Kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya upweke. Usifunge ndoa kwa sababu ya upweke. Kuna tofauti kati ya upweke na kuwa peke yako “there is a difference between loneliness and to be alone”. Upweke unahusu moyo “emotional” na kuwa peke yako inahusu hali ya nje ya mwili “physical”. Ndoa haiwezi kutatua matatizo ya upweke hususan endapo kama uliyempata sio sahihi kwako. Unaweza ukaolewa au ukaoa na baada ya hapo ukaendelea kuishi mpweke kama ulishindwa kumpata mtu sahihi.

Kuingia kwenye ndoa kwa msukumo wa wazazi au marafiki. Usioe kwa sababu ya msukumo. Usioe au kuolewa kwa sababu wazazi wamekwambia uoe au uolewe au kwa sababu marafiki zako wengi nao wameoa au wameolewa. Kumbuka hiyo ndoa unayoenda kuianzisha ni ya kwako na sio ya wazazi wako au marafiki zako. Kuingia kwenye ndoa ili kutafuta kuwa huru. Usifunge ndoa kwa sababu unahitaji kuwa huru kutoka kwa wazazi wako.

Yamkini wazazi wako wanakubana sana na unashindwa kuishi kwa uhuru au kufanya yale unayoyataka sasa unahisi ukiolewa utatoka kwa wazazi wako na kuwa huru zaidi. Wako waliowaza kama wewe wakajikuta wamejiingiza kwenye jela ngumu kuliko waliyokuwa nayo awali.

Kuingia kwenye ndoa kwa sababu ya mimba au mtoto. Yawezekana sana mmepata mtoto au umempa mtu mimba au umepewa mimba na bado hamjaingia kwenye ndoa.

Kama hamna upendo wa dhati na kama hamkuwa mna mipango ya kuingia kwenye ndoa nawashauri subirini kwanza.

Ni bora kumlea mtoto hamjaoana mkiwa na amani kuliko kuingia kwenye ndoa wakati penzi penu halikuwa la ndoa bali ni la mpito halafu mkashindwa hata kupata muda wa malezi kwa jinsi ambavyo kila siku ni vita moja kwenda vita nyingine.

Wanawake niwasihi sana, tabia za kumtegeshea mwanaume mimba ili akuoe ni ufunguo wa kilio kwa watu wengi sana. Mimba au mtoto sio tiketi ya kuingia kwenye ndoa.

Advertisement