KOMBE LA DUNIA 2018-Viwanja 12 vitakavyokutanisha wanaume wa shoka Russia

Muktasari:

  • Hii ni mara ya kwanza kwa fainali hizo kwa idadi hiyo ikiwa ni mabadiliko na ahadi ya Rais wa Fifa, Gianni Infantino aliyoitoa wakati anawania nafasi hiyo mwaka juzi.

Fainali za Kombe la Dunia 2026 zinazowaniwa na Marekani, Canada na Morocco na mataifa mengine zitakavyokuwa kwa kuwa zitahusisha mataifa 48.

Hii ni mara ya kwanza kwa fainali hizo kwa idadi hiyo ikiwa ni mabadiliko na ahadi ya Rais wa Fifa, Gianni Infantino aliyoitoa wakati anawania nafasi hiyo mwaka juzi.

Lakini keshokutwa tu hapa, zimesalia kama siku 58 kabla ya fainali za mwaka huu na mchezo wa ufunguzi ambao mechi ya kwanza wenyeji dhidi ya Saudi Arabia wakati siku inayofuata, mkali wa mabao Ligi Kuu England, Mohamed Salah ataiongoza Misri dhidi ya wababe wa rafu, Uruguay. Vifuatavyo ni viwanja 12 ambavyo vumbi litatimka, nyasi zitaumizwa ili kumpata mbabe wa Kombe la Dunia mwaka huu kwa miaka minne ijayo.

1. Uwanja wa Luzhniki

Una uwezo wa kuzoa mashabiki 81,000. Umekarabatiwa na kufunguliwa mwaka 2017 kwani mara ya kwanza ulijengwa mwaka 1955. Ndiyo uwanja unaotumiwa na timu ya taifa ya Russia. Utachezewa mechi za Kundi A, 14 Juni kati ya Russia na Saudi Arabia; mchezo wa Kundi F wa Juni 17, Ujerumani na Mexico, mechi ya Kundi B, Juni 20 Ureno dhidi ya Morocco; Kundi C, Juni 26 Denmark itakwaana na Ufaransa. Pia mechi moja ya 16 Bora, Julai 1, nusu fainali Julai 11 na Fainali Julai 15. Uwanja huo una historia ndefu kwani uliandaa Michezo ya Olimpiki 1980 na Fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya 2008 ambayo Manchester United iliifunga Chelsea kwa mikwaju ya penalti.

Pia uwanja huo ulikuwa mwenyeji wa mashindano ya Ubingwa wa Riadha wa Dunia mwaka 2013.

2.Uwanja wa Spartak

Unamilikiwa na klabu ya Spartak Moscow kwa mechi zake za ligi na Ligi ya Mabingwa Ulaya. Una uwezo wa kuchukua mashabiki 45,360 kwa wakati mmoja, Ulifunguliwa 2014 baada ya kufanyiwa ukarabati mkubwa. Utachezewa mechi ya Kundi D, Juni 16 Argentina na Iceland; mechi ya Kundi H, Juni 19 Poland itakapokwaana na Senegal; Kundi G, Juni 23 Ubelgiji na Tunisia na mechi ya Kundi E, Juni 27 kati ya Serbia dhidi ya Brazil. Pia mechi ya 16 Bora itakayochezwa Julai 3.

Uwanja huo ambao pia unafahamika kwa jina la Otkrytiye Arena la wadhamini umenakshiwa kwa vito vya thamani ikiwemo almasi katika maeneo mbalimbali kuonyesha mvuto wake. Uwanja huo hubadilika rangi kutegemeana na rangi ya jezi za timu zinazocheza siku hiyo kama ulivyo Uwanja wa Bayern Munich wa Allianz Arena.

3. Uwanja wa Saint Petersburg

Unamilikiwa na klabu ya Zenit St Petersburg. Una uwezo wa kuzoa mashabiki 64,287 na ulifunguliwa 2017.

Mechi zitakazopigwa hapa ni ya Kundi B Juni 15, Morocco dhidi ya Iran, mechi ya Kundi A, Juni 19 Russia na Misri; Kundi E, Juni 22 Serbia dhidi ya Uswisi, Kundi D, Juni 26 Iceland itacheza na Croatia; pia mechi moja ya Raundi 16 itachezwa Julai 3; mechi moja ya nusu fainali Julai 10 na mechi ya kusaka mshindi wa tatu itakayochezwa hapo Julai 14.

Uwanja umejengwa eneo la kuvutia kwenye Ghuba ya Finland na unapendeza na umetajwa kwamba ni kati ya viwanja ghali duniani na thamani yake ni Dola1.5bilioni.

Kwa watakaofika kwenye uwanja huo, Saint Petersburg unavutia na kiukweli unatumika kama kivutio cha utalii pia.

4. Uwanja wa Kaliningrad

Una uwezo wa kuchukua mashabiki 35,212. Unamilikiwa na timu ya Baltika Kaliningrad

Mechi zitakazopigwa hapo ni ile ya Kundi D, Juni 16 Croatia na Nigeria; mechi ya Kundi E, Juni 22 Serbia itakapocheza na Uswsi; Kundi B, Juni 25 Hispania na Morocco na mechi ya Kundi G, Juni 28 England itakapokwaana na Ubelgiji.

Kaliningrad uko mbali kidogo kutoka katikati ya Russia na pia uko katikati ya Poland na Lithuania.

5. Kazan Arena

Uwanja huu unamilikiwa na klabu ya Rubin Kazan wenye uwezo wa kuchukua mashabiki 45,379. Ulizinduliwa mwaka 2013.

Utachezwa mechi ya Kundi C, Juni 16 Ufaransa na Australia; mechi ya Kundi B, Juni 20 Iran dhidi ya Hispania; Kundi H, Juni 24 Poland itakwaana na Colombia; Kundi F, Juni 27 Korea Kusini na Ujerumani; pia mechi moja ya Raundi 16 Juni 30 na mechi ya Robo Fainali ya Julai 6. Uwanja huo unafanana kwa kiasi fulani na Uwanja wa Wembley na ule wa Arsenal wa Emirates. Ulizinduliwa miaka minne iliyopita. Ukiuangalia kwa juu, unafanana na Mto Kazanka.

Ni uwanja pekee Ulaya wenye skrini kubwa kwa nje ikionyesha mechi inapochezwa, na kwamba watu wanaweza kuona kila kinachoendelea ndani wakiwa nje.

6. Uwanja wa Nizhny Novgorod

Uwanja huu unabeba mashabiki 44,899 waliokaa kwa wakati mmoja na unaotumiwa na klabu ya Olimpiyets Nizhny Novgorod

Mechi ambazo zimepangwa kupigwa kwenye uwanja huo ni ile ya Kundi F, Juni 18 Sweden dhidi ya Korea Kusini; Kundi D, Juni 21 Argentina na Croatia; Kundi G, Juni 24 England itacheza na Panama; Kundi E, Juni 27 Uswisi dhidi ya Costa Rica.

Pia mechi ya 16 Bora itakayochezwa Julai 1 na mechi moja ya robo fainali itakayopigwa Julai 6.

Uwanja huo uko katikati ya Moscow na Kazan, na ni uwanja mpya. Nizhny Novgorod pia uko eneo la kuvutia katika mto Volga na Oka rivers, na unaweza kuchezewa katika hali zote, wakati wa jua na mvua.

7. Uwanja wa Samara (Cosmos Arena)

Huu uwanja unaweza kubeba mashabiki 44,918 tangu kufunguliwa kwake. Klabu ya Kylia Sovetov ndiyo yenye kuumiliki kwa sasa.

Uwanja huo utatumika kwa mchezo wa Kundi E, Juni 17 Costa Rica dhidi ya Serbia; Pia mechi ya Kundi C, Juni 21 Denmark itacheza na Australia; mechi ya Kundi A, Juni 25 Uruguay itacheza na wenyeji Russia na mechi ya Kundi H, Juni 28 Senegal dhidi ya Colombia na mchezo wa 16 Bora Julai, 2; na ule wa robo fainali Julai, 7.

Uwanja huu ambao uko sehemu ya mkoa wa Volga, ni kati ya viwanja ambavyo vimejengwa kisasa zaidi.

8. Uwanja wa Volgograd Arena

Uwezo wa uwanja huu ni kuchukua mashabiki 45,568. Unamilikiwa na Klabu ya Rotor Volgograd.

Mechi zitakazopigwa hapa ni za Kundi G Juni 18, Tunisia itakuwa mwenyeji wa England; Kundi D, Juni 22 Nigeria itapambana na Iceland na mechi ya Kundi A, Juni 25 ni Saudi Arabia dhidi ya Misri. Pia mechi ya Kundi H, Juni 28 ambayo Japan itacheza dhidi ya Poland.

Mpambano wa kwanza kwenye uwanja huo utakuwa kati ya England na Tunisia Juni 18.

9. SARANSK - Mordovia Arena

Uwanja huu uwezo wake ni mashabiki 44,412 na ulizinduliwa mwaka jana kwa ajili ya fainali hizo. Klabu ya Mordovia Saransk ndiyo wamiliki wa uwanja huo.

Mechi za Kundi C ya Juni 16 Peru itacheza na Denmark; Kundi H, Juni 19 Colombia dhidi ya Japan; mechi ya Kundi B, Juni 25 Ureno itakwaana na Iran na mechi ya Kundi G, Juni 28 Panama itaingiliana na Tunisia.

Kiukweli, uwanja huu unavutia mno na umepambwa kwa rangi za orange, nyekundu, nyeupe, na ukuta wake umenakshiwa kwa marumaru kwa ajili ya kuufanya ung’ae kuonyesha kuwa Mordovia umesanifiwa kiufundi hasa.

10.ROSTOV-ON-DON - Rostov Arena

Uwezo wa uwanja huu ni kuchukua mashabiki 45,000 na umekamilika tayari kwa mashindano hayo. Ulikuwa unafanyia ukarabati mkubwa. Klabu ya Rostov ndiyo wamiliki wa uwanja huu.

Mechi zitakazotumika kwenye uwanja huu ni za Kundi E ya Juni 17 kati ya Brazil na Uswisi; Kundi A, Juni 20 Uruguay dhidi ya Saudi Arabia; Kundi F, Juni 23 Korea Kusini itacheza na Mexico; Kundi D, Juni 26 Iceland na Croatia; mechi moja ya 16 Bora itakayochezwa Julai 2.

Uwanja huo uko umbali wa kilomita 1,000 Kusini kutoka mji wa Moscow (ni kama kutoka Dar es Salaam hadi Kagera). Uwanja wa Rostov-on-Don unapendeza na utakuwa kivutio cha aina yake kwa watakaofika hapo.

Mashabiki wa Manchester United waliofika kuona mechi dhidi ya Rostov wakati wa michuano iliyopita ya UEFA Europa watakuwa na kumbukumbu nzuri na uwanja huu.

11.Uwanja wa Sochi (Fisht)

Tangu kufunguliwa mwaka 2013, uwezo wake ni kuchukua mashabiki 47,659 na timu mbalimbali za Russia huutumia kwa mechi zao.

Mechi zilizopangwa kuchezwa hapa ni za Kundi B ya Juni 15 Ureno ya Cristiano Ronaldo itakuwa na rafiki zake wa Hispania; Kundi G Juni 18 Ubelgiji itacheza na Panama; Kundi F, Juni 23 Ujerumani dhidi ya Sweden na mechi ya Kundi C ya Juni 26 Australia itakapocheza na Peru. Mechi nyingine ni ya 16 Bora itachezwa Juni 30; na robo fainali Julai 7.

Kimsingi, ujenzi hasa wa uwanja huu ulianza mwaka 2014 na uliwahi kuandaliwa Michezo ya Olimpiki na Paralimpiki. Uwanja ulivunjwa wote na kujengwa upya kwa ajili ya Kombe la Dunia.

12.Uwanja wa Yekaterinburg (Central)

Unakamilisha safu ya viwanja 12. Huu unachukua mashabiki 35,000. Umefanyiwa ukarabati kukidhi mashindano kwani mara ya kwanza ulifunguliwa mwaka 1957. Ukarabati ulianza mwaka 2014 hadi mwaka jana 2017. Unamilikiwa na klabu ya FC Ural.

Mechi zitakazopigwa hapa ni ya Kundi A, Juni 15 Misri na Uruguay; Kundi C, Juni 21 Ufaransa itacheza na Peru; Kundi H, Juni 24 Japan dhidi ya Senegal na mechi ya Kundi F Juni 27 kati ya Mexico na Sweden.

Uwanja huu uko mbali zaidi ya viwanja vingine kutoka mji wa Moscow. Ni umbali wa kilomita 1,800 kutoka Moscow na kilomita 2,300km kutoka ulipo uwanja wa Saint Petersburg. Hili ni kombe la Dunia ambalo timu zitakuwa zinasafiri kila mara mwendo mrefu kati ya saa mbili hadi tatu.

Mashabiki wa England wamesema hawataki kuusikia Uwanja wa Yekaterinburg kwa kuwa uko mbali mno na itawalazimu kugharimika zaidi. Kwa ndege ni umbali wa saa 3 kutoka Moscow lakini ni saa tano kutoka ulipo Uwanja wa Saint Petersburg.

Kama ulivyokuwa Uwanja wa Luzhniki mjini Moscow, uwanja huu umefanyiwa ukarabati mkubwa kwani mara ya kwanza ulifunguliwa mwaka 1953.

Kwa mji huo, ulipo Uwanja wa Yekaterinburg unaweza kuona vizuri safu za milima Ural.