Kurejesha nidhamu sawa, lakini siyo kwa kutumia nguvu

Wednesday October 26 2016

By Idd Hamis

Uko usemi kwamba mlevi huchukia kuitwa mlevi lakini haachi kunywa pombe. Hivi karibuni umezuka mtindo wa wakuu wa wilaya kuwasweka ndani maofisa wa Serikali kwa makosa wanayotuhumiwa kuyatenda.

Mtindo huu ulianza Oktoba 28 mwaka jana wakati aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Paul Makonda alipowaamuru polisi kuwasweka ndani maofisa ardhi zaidi ya 10 kwa madai ya kuchelewa katika kikao cha kusikiliza migogoro ya wananchi Kata ya Wazo Hill katika wilaya hiyo.

“Hivi sasa wamewekwa mahabusu katika Kituo cha Polisi Wazo na tumelazimika kuahirisha shughuli hii kwa muda,” alisema Makonda ambaye hivi sasa ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam na huenda kilichompandisha cheo ni ‘ushupavu’ kama huo wa kuwaweka ndani maofisa hao wa Serikali.

Tarehe 20 mwezi huu vyombo vya habari viliripoti kwamba Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili amewaweka rumande kwa saa 48, Mkurugenzi    wa Mamlaka  ya Majisafi na Majitaka   Bunda (BUWSA), Mansour Mandeba   na Mhandisi Msaidizi, Maisha  Malecela.

Inadaiwa  maofisa hao walishindwa kutoa  huduma bora za maji  kwa wakazi wa Bunda na  kushindwa kutekeleza agizo  la mkuu huyo  wa wilaya  tangu   Agosti mwaka huu.

Agizo hilo liliwataka   kutoa maelezo ya kina  sababu  zilizofanya  mradi  mkubwa wa maji  uliogharimu takriban Sh9 bilioni kushindwa kuwapatia majisafi  wakazi wa mji huo wa Bunda mkoani Mara.

Mkuu huyo wa wilaya alidai  kuwa  watumishi hao  ni wahujumu uchumi  kwa kuwatoza  wateja  wa maji  tozo  zilizo chini ya  kiwango  kilichoelezwa katika  mwongozo wa Serikali na kusababisha  mamlaka hiyo kutojiendesha  inavyotakiwa. Je, adhabu ya mhujumu uchumi ndiyo hiyo?

Hata hivyo, huu ni mwendelezo wa matukio kama haya ya kuwaweka ndani watumishi wa Serikali Kuu au halmashauri kwa makosa ya kiutendaji ambayo si makosa ya jinai tena yenye sheria za kazi zinazoelekeza jinsi ya kushughulikiwa.

Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997, kifungu cha 15 (1) inawapa mamlaka wakuu wa mikoa na wilaya kutoa amri ya mtu kukamatwa na kuwekwa ndani kwa saa 48 pale anapobaini kwamba mhusika ametenda kosa fulani.

Kosa gani, tutafafanua huko mbele

Wakuu wa wilaya sasa wanatumia mamlaka hayo pale watendaji wao wanaposhindwa kutimiza maagizo yao. Suala la watendaji kuwekwa ndani limeshuhudiwa huko nyuma katika wilaya za Sengerema, Arumeru, Rorya na Newala.

Mkuu wa Wilaya ya Sengerema, Emmanuel Kipole alimsweka ndani kwa saa 12 Kaimu Mkurugenzi wa wilaya hiyo, Oscar Kapinga na kaimu mhasibu wa halmashauri hiyo, Paul Sweya Oktoba 13, mwaka huu kwa kushindwa kutekeleza agizo la mkuu huyo wa wilaya la kutafuta fedha kwa ajili ya kuwalipa wanaofanya usafi katika mji wa Sengerema.

Tukio jingine ni lile la Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti kuwaweka ndani madiwani wanne wa Chadema kwa madai kwamba wamekuwa wakimkwamisha kutekeleza kazi zake tarehe 12 Oktoba.

Miongoni mwa waliowekwa ndani ni Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Noah Lembrise ambaye alilala katika Kituo cha Polisi cha Usa River. Wengine ni Happy Gadiel, Nuru Ndosi na Winfrida Lukumay.

Akitoa maelezo kuhusu kitendo hicho, Mkuu huyo wa Wilaya alisema “hawa (madiwani) wamekuwa wakivuruga ziara zangu kwa kupita kwa wananchi na kupotosha dhima ya Serikali kuhusu maendeleo.”

Oktoba 16 huko wilayani Newala nako, Mkuu wa Wilaya, Aziza Mangosongo alimlaza katika kituo cha Polisi Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Maji Mradi wa Makondeko, Athumani Semkondo na fundi Mohamed Salum kwa saa 48 kwa kuvikosesha maji vijiji 14 vyenye wakazi 60,000.

Mangosongo alisema kulifanyika hujuma ya kuziba bomba ili maji yasipatikane katika vijiji hivyo lakini Kaimu Mkurugenzi huyo alishindwa kufuatilia taarifa aliyopewa kwamba vijiji hivyo havipati maji ili achukue hatua.

“Kama mkurugenzi alikuwa na taarifa na hakuchukua hatua, kuna nini kimejificha hapo? Lazima nitahisi kuna jambo ndiyo maana nikaamua akalale rumande kwa saa 48 kwa sababu nina mamlaka kisheria. Akae humo ndani kwanza ajitafakari,” alisema Mangosongo.

Hali kama hiyo ilitokea pia katika Wilaya ya Rorya baada ya mkuu wa wilaya hiyo, Simon Chacha kuwaweka ndani watu 10 akiwamo Diwani wa Kigunga (Chadema), Vitalis Joseph baada ya kutokea mgogoro kati ya vijiji viwili na kusababisha mazao kufyekwa.

Sheria zetu zinasemaje?

Sheria ya Tawala za Mikoa ya mwaka 1997 (The Regional Administration Act) kwenye kifungu cha 15 (1) imeweka sharti muhimu kwa mkuu wa wilaya ikiwa atahitaji kutumia mamlaka ya kuamrisha mtu akamatwe.

Kifungu hicho kinamtaka afanye hivyo pale ambapo atakuwa amejihakikishia kuwa kosa lililotendwa na mhusika athari yake huwa ni kukamatwa na kushtakiwa na tena sheria imeweka masharti ya namna ya kushtaki.

Sasa tujiulize je wakuu hawa wa wilaya waliotumia madaraka yao kuwasweka ndani watumishi wa Serikali Kuu au Serikali za Mitaa, makosa yanayodaiwa kutendwa na hao watumishi yanakidhi masharti yaliyo katika sheria hiyo hapo juu? Ni wazi wakuu hao wametenda kosa.

Sheria hiyo iko wazi katika kifungu cha 15 (1) kwamba ikiwa Mkuu wa Wilaya atatumia mamlaka yaliyowekwa na kifungu husika kwa maana ya kutumia madaraka yake vibaya, atakuwa ametenda kosa na anaweza kushtakiwa kwa mujibu wa kifungu cha 96 cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu (Penal Code).

Je, tangu Makonda, Chacha, Mangosongo, Mnyeti, Kipole na sasa Bupilipili watende makosa hayo ya matumizi mabaya ya madaraka yao kuna kiongozi yeyote wa juu wa Serikali iwe ni Waziri Mkuu, Makamu wa Rais au Rais John Magufuli aliyeonyesha kushtuka?

Kifungu hicho cha 96 (1) na (2) kinaeleza kuwa mtu yeyote ambaye ameajiriwa kwenye utumishi wa umma (akiwemo Mkuu wa Wilaya) anayetenda au kuamrisha utendekaji wa jambo kwa kutumia vibaya madaraka ya kazi yake, kitendo chochote cha dhuluma ambacho kinazuia haki ya mwingine atakuwa ametenda kosa na akitiwa hatiani anaweza kufungwa miaka mitatu jela.

Wakuu hawa wa wilaya wamezuia haki ya watumishi waliowaweka ndani kuwa huru hata kama ni kwa dakika moja au saa moja bila uhalali. Hiki ni kielelezo kibaya kabisa cha utawala wa JPM kulea matumizi mabaya ya madaraka.

Watumishi wote ambao waliwekwa ndani na wakuu hawa wa wilaya wanaweza kufungua mashtaka dhidi ya wakuu hao na sheria ikachukua mkondo wake. Hakuna mtu aliye juu ya sheria za nchi awe ni mkuu wa wilaya, mkoa, waziri au hata rais.

Bahati mbaya iliyoko ni kwamba sheria ya kanuni ya adhabu kifungu cha 96 (3) ambayo ingewasaidia watumishi hao kupata haki yao imeweka sharti kuwa uendeshaji wa shitaka dhidi ya wahusika hautaanzishwa mpaka kitakapotolewa kibali cha Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).

Wakati wa uongozi wa Rais mstaafu Jakaya Kikwete kuna Mkuu wa Wilaya ya Bukuba, Albert Mnali aliwahi kuamrisha kuwachapwa viboko hadharani walimu wa shule tatu za Katerero, Kanazi na Kasenene mkoani Kagera mwanzoni mwa mwaka 2009.

Februari mwaka huo, Kikwete alimvua madaraka mkuu huyo wa wilaya kwa kosa hilo. Kosa la kuwachapa walimu viboko ni sawa na hili linaloanza kuzoeleka la wakuu wa wilaya kuwasweka ndani watumishi wa umma.

Inavyoelekea wakuu hawa wa wilaya wanafuata maelekezo ya JPM aliyowahi kuyatoa Machi mwaka huu kwa wakuu wa mikoa alipowaambia “ninyi mna mamlaka ya kuwaweka watu ndani hata masaa 48, wekeni watu ndani ili wajue mnatakiwa kuheshimiwa.

Tusiogope kuchukua uamuzi, nafuu uchukue uamuzi hata kama ni mabaya yatarekebika huko mbele”. Alisema JPM.

Katika mazingira haya, ni vugumu kwa wakuu wa wilaya na mikoa kujizuia kuchukua hatua kwa sababu mkuu wa nchi alishawawashia ‘taa ya kijani’. Kwa maelezo hayo ya rais ni wazi uamuzi wanaouchukua wakuu hawa ni mabaya.

Ni jambo muhimu kurudisha nidhamu ya watumishi wa umma, lakini isirudishwe kwa njia ambazo huonekana katika nchi zinazotawaliwa kwa mabavu.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii anapatikana kwa barua pepe: [email protected] na [email protected]

Advertisement