Mapenzi ni utu siyo utajiri: Mifano kutoka fasihi ya Kiswahili

Tuesday May 15 2018

 

Katika makala haya dhana ya mapenzi itajadiliwa kwa muktadha wa uhusiano kati ya mume na mke kwa watu waliooana au ambao wana mwelekeo huo. Katika nyakati hizi, vijana wa kike wanapoingia katika uhusiano wa kimapenzi, mathalani uchumba, baadhi yao hupata wakati mgumu wakiwaweka wenza wao katika mzani wa utajiri na umaskini. Vijana wengi wa kike siku hizi hususan katika mazingira ya mijini humkubali mchumba kwa kuangalia uwezo wake wa kifedha, mali au kazi anayofanya.

Miongo kadhaa iliyopita, suala hilo halikuwa na sura hiyo. Kilichoangaliwa katika kumkubali mchumba kwa mfano, ni utu wa mtu, maadili, uchapakazi na sifa nyingine nzuri zilizokubaliwa na jamii.

Suala la uwezo wa kifedha na mali halikupewa kipaumbele. Kijana wa kiume aliyeonyesha uadilifu kwa jamii na uchapakazi, hata kama hakuwa na fedha au mali, alifanikiwa kupata mchumba kwa haraka. Halikadhalika, vijana wa kike walioonyesha uadilifu na uchapakazi, walikuwa na ‘soko’ kubwa.

Kwa kifupi tunaweza kusema kuwa, uadilifu na uchapakazi vilikuwa mtaji mkubwa wa uhusiano katika suala la uchumba na ndoa. Vijana waliokubaliana kuoana wakiwa wachapakazi na waadilifu, walifanya kazi kwa bidii wakiwa pamoja kama wanandoa na hivyo kujiletea maendeleo ya haraka.

Lakini kadiri siku zinavyozidi kupita, mambo yamekuwa yakibadilika si mijini wala vijijini. Kwa sababu hiyo, ndoa nyingi za kifahari zimekuwa zikifungwa lakini hazidumu.

Wengine kwa kujiingiza katika uhusiano na wale waliowafikiria kuwa ndio watu wa kufaa kwao, wamejikuta katika mazingira magumu: wamepewa mimba na kubwagwa kabla ya ndoa au wameishia kutelekezwa na watoto na kadhalika. Hata hivyo, kwa maelezo haya haimaanishi kwamba watu wote wenye uwezo wa kifedha ndio wanaofanya hivyo, la hasha!

Kwa kurejelea riwaya ya ‘Nyota ya Rehema’ iliyoandikwa na M.S. Mohamed (1976), mwandishi anaibua dhamira ya utu kupitia mhusika Sulubu ambaye anamsaidia mhusika Rehema akiwa taabani hajitambui.

Mwandishi anamchora Rehema akikata shauri la kuondoka nyumbani kutokana na mateso aliyokuwa akiyapata baada ya mama yake mzazi kufariki (uk. 22).

Akiwa msituni anapatwa na masaibu. Mwandishi anasema: “...Rehema alijitoma mbio katika mwitu, akajipiga na jiti hili na lile, kuanguka fudifudi juu ya masiki na miiba; akapotewa na fahamu” (uk. 25).

Katika hali hiyo Rehema aliokolewa na maskini mkulima Sulubu kwa kumpa dawa, chakula na kukaa naye mpaka fahamu zilipomrudia na kurejea katika hali ya kawaida. Baada ya Rehema kutangatanga na maisha ya mjini, baadaye alizingatia ushauri wa Bikiza, rafiki ya mama yake kwenda kwa baba yake kuomba shamba la Ramwe. Kisha alikata shauri la kubadilisha mtindo wa maisha, yaani kwenda kuishi huko shambani.

Katika hilo alimkumbuka ‘mtu’ muhimu sana aliyemwokoa maishani - Sulubu, mwenye utu na mchapakazi. Alimfuata, wakakubaliana kuishi pamoja mume na mke, wakisaidiana katika raha na taabu.

Katika kisa hiki kuna mengi ya kujifunza lakini kubwa kulingana na lengo la makala haya ni suala la utu na uadilifu katika uhusiano. Kupitia utu, uadilifu na uchapakazi, pesa na mali hupatikana. Uchaguzi wa wenza kwa kigezo cha pesa au mali una changamoto nyingi, mojawapo ikiwa ni migogoro na kutodumu kwa uhusiano wa wanandoa.

Advertisement