Mbinu za kuchagua masomo ya kidato cha tano-1

Tuesday February 13 2018Christian Bwaya

Christian Bwaya 

Nianze kwa kukupongeza kijana uliyefaulu mitihani yako ya kidato cha nne ambayo matokeo yake yalitanganzwa hivi karibuni.

Ni dhahiri kuwa sasa unafikiri ukasome nini kitakachokuwezesha kutimiza ndoto zako.

Naandika makala haya kukusaidia kufanya maamuzi. Ingawa sifahamu mazingira yako, matokeo na ndoto ulizonazo, naamini ninao uzoefu kiasi unaoweza kukusaidia.

Mbali na kuwa mnasihi wa masuala ya ajira, nimepita safari inayoweza kukusaidia kuelewa ufanye nini.

Ugumu wa maamuzi

Miaka ipatayo 17 iliyopita nilifaulu vizuri sana mitihani yangu ya kidato cha nne. Nilipata alama za juu za daraja la kwanza. Tofauti na wenzangu waliokuwa wamefaulu baadhi ya masomo na hivyo kujikuta wana wigo mdogo wa uchaguzi wa masomo.

Mimi nilikuwa na fursa ya kwenda kusoma mchepuo wowote bila wasiwasi. Hili lilinigharimu kama nitakavyoeleza.

Wakati namaliza kidato cha nne Novemba 2000, walimu niliokuwa nao karibu, walinishauri nikasome masomo ya sayansi. Kwa maoni yao, nilikuwa nafanya vizuri kwenye masomo hayo. Walinieleza pia kuwa sayansi ina ‘soko.’

Walimu wengine walionifahamu vizuri zaidi walikuwa na maoni tofauti. Wao walifikiri ningesoma masomo ya sanaa ningefika mbali zaidi. ‘Tatizo’ ni kwamba hata kwenye masomo hayo, nilikuwa nafanya vizuri.

Shule niliyosoma, ilikuwa na mchepuo wa sayansi kwa kidato cha tano na sita. Hiyo ilitujenga dhana sisi wanafunzi wa vidato vya chini kuwa wenye uwezo mzuri kiakili husoma sayansi.

Ingawa tabia zangu na mambo yaliyonivutia nje ya darasa hayakuwa na uhusiano wowote na sayansi, sikuwa tayari kwenda kusoma masomo ya ‘watu waliofeli sayansi.’

Nikifupisha kisa changu, nilichaguliwa kwenda Same Sekondari, Kilimanjaro, kusoma masomo ya Fizikia, Kemia na Biolojia. Ingawa nilikuwa nimefaulu vizuri masomo hayo, lakini ndani yangu sikuwa na uhakika ninataka kufanya nini maishani.

Kuliko kwenda kusoma ‘masomo ya watu waliofeli sayansi,’ niliamua bora nisome sayansi ili niwe mwalimu wa ‘masomo yanayolipa.’

Kusoma kwa mkumbo

Nikiri kuwa nilisoma sayansi kwa mkumbo. Ndani yangu kuliishi uandishi wa habari. Nakumbuka nikiwa kidato cha tano niliwashawishi wenzangu kadhaa, leo wengine ni madaktari wa binadamu kuanzisha gazeti la shule.

Mara kadhaa mkuu wa shule alijibu hoja zetu tulizoziibua kwenye gazeti hilo lililobandikwa kwenye mbao za matangazo.

Nilifaulu kidato cha sita na nikaenda kusoma ualimu wa sayansi kama nilivyojiita kwa miaka miwili. Hata hivyo, ukweli ni kwamba sikuwa najua kwa hakika ninataka nini.

Nikiwa chuo tabia na shughuli zangu nyingi nje ya darasa zilinielekeza kwingine. Wakati mwingine huwa ninaamini nilivutiwa na ualimu kwa sababu ndiyo kazi pekee niliyoifahamu vizuri tangu nikiwa mdogo. Hiyo ndiyo kazi aliyoifanya baba yangu.

Unaweza kuona kwamba ingawa nilikuwa na fursa ya kusoma mambo mengine, nilijikuta naishia kusoma chochote kwa sababu sikuwa na taarifa sahihi zilizonisaidia kujitambua mapema.

Kusema hivyo haimaanishi nakukatisha tamaa kijana unayetaka kuwa mwalimu. Hata kidogo. Najaribu kukuonyesha nilivyosoma bila malengo yanayoeleweka.

Nikiwa chuo kikuu, nikawa msomaji mzuri sana wa vitabu. Nilitumia muda mrefu kusoma vitabu vya maisha ya kawaida kuliko Biolojia na Kemia. Hapo ndipo nilianza kubaini ndani yangu kulikuwa na kitu gani. Hatimaye, ilinichukua miaka kadhaa migumu ‘kukata kona’ ili nikuze kile nilichokigundua ndani yangu.

Natamani usipite njia niliyopita mimi. Natamani usibahatishe kama ilivyokuwa kwangu. Ndio maana ninaandika mfululizo wa makala haya kukusaidia kufikia ndoto na wito wako kwa urahisi zaidi kuliko mimi. Naanza na swali la kwanza.

Kitu gani kinakugusa?

Kila mtu analo eneo la maisha linalomvutia kulifuatilia kwa karibu. Kuna kitu ambacho ukikisikia kinazungumzwa mahali moyo wako unasisimka.

Unapokuwa kwenye mazungumzo na watu wengine, masikio yako yanasikia kitu hicho hata kama watu wengine hawakisikii. Unanunua vitabu, unafuatilia televisheni na mitandao na karibu kila unachokifanya kinazunguka zaidi kwenye eneo hilohilo.

Unapoendelea kusoma hapa tayari kuna kitu kinakujia kichwani. Inawezekana ni matatizo fulani ya watu, hitaji fulani unalofikiri jamii yetu inalo au ubunifu fulani unaoamini bado jamii haijauona.

Labda ni masuala ya teknolojia. Inawezekana ni mfumo fulani wa maisha, imani au fikra katika jamii unazofikiri ungepewa nafasi ungezibadilisha. Chochote kile kinachogusa fikra zako, usikidharau unapofanya maamuzi ya nini ukasome kwa kidato cha tano.

Mimi nilipenda sana kusoma vitabu vinavyohusu elimu ya nafsi na tabia za watu. Sikuhitaji kufundishwa sana kuelewa eneo hilo kwa sababu ndicho kitu kilichokuwa kinanigusa tangu nikiwa kijana wa sekondari.

Hata hivyo, kama nilivyotangulia kueleza, nilisoma mambo mengine kabisa yasiyohusiana na hicho kilichonigusa. Hatimaye ilinibidi kutumia nguvu nyingi kubadili mwelekeo.

Unajitambulisha na kitu gani?

Kwa kawaida, kuna vitu tukivifanya vikaleta matokeo fulani tunajisikia fahari. Kila mtu ana eneo lake akilifanya vizuri anajisikia kuridhika. Huhitaji kulipwa kufanya kitu hicho kwa sababu ndicho kinachokutambulisha.

Kuna watu wanajisikia fahari kuimba. Huhitaji kuwalipa waimbe. Wengine fahari yao ni ubunifu, wengine uongozi, wengine biashara.

Kile kinachokuletea ufahari, mara nyingi, utapenda kujitambulisha nacho. Utatumia muda mwingi kukielewa kuliko unavyofanya kwenye maeneo mengine.

Nikirejea mfano wangu, tangu nikiwa shule rafiki zangu walinifahamu kwa tabia yangu ya kupenda kusoma magazeti na vitabu. Nilisoma makala ndefu bila kuruka aya. Niliwafahamu waandishi maarufu karibu wote. Sio ajabu leo na mimi ninaandika makala.

Jiulize, kitu gani ukikifanya vizuri unajisikia fahari? Je, watu wanakusifia na kukutambua kwa kitu gani? Ukiweza kuuoanisha uwezo huo na kazi unayoifanya itakuwa rahisi kupata mafanikio makubwa zaidi. Kasome masomo yanayokuelekeza kusoma hicho kinachokugusa. Itaendelea


Advertisement