LICHA YA KUIZIMA CITY-Mourinho amtaka zaidi kwa pogba

Muktasari:

  • Unaweza kujiuliza kwa sasa akili ya kiungo huyo wa Manchester United inawaza nini au unaweza kujiuliza mengi tu anachofikiria kocha wake, Jose Mourinho kuhusu Pogba?

Achana na matokeo ya jana kati Manchester United na West Bromwich Albion. Unayakumbuka yale mabao mawili ya Paul Pogba dhidi ya Manchester City?

Unaweza kujiuliza kwa sasa akili ya kiungo huyo wa Manchester United inawaza nini au unaweza kujiuliza mengi tu anachofikiria kocha wake, Jose Mourinho kuhusu Pogba?

Wiki kadhaa zilizopita, ishu ilikuwa kiwango cha Pogba. Mourinho alifikia hatua akawa anamuanzishia benchi mchezaji huyo Mfaransa aliyemnunua kwa bei mbaya.

Lakini katika mchezo mzima dhidi ya Man City, ni kama Pogba alikuwa anawatumia salamu mashabiki wa Manchester United kwamba bado anaweza kufanya makubwa hata katika mechi kubwa baina ya majirani hao wa Manchester.

Alifunga mabao mawili ndani ya dakika 10 akifuta mabao ya mapema ya Vincent Kompany na Ilkay Gundogan. Dakika 20 kabla ya filimbi ya mwisho, Chris Smalling akahitimisha ushindi wa mabao 3-2.

“Nitaambieni kile nilichomwambia baada ya mechi na City,” alisema Mourinho.

“Sikutegemei uwe nyota wa kila mechi, sitegemei ufunge mabao mawili kila wiki na sitegemei ufunge katika kila mechi. Nataka kiwango chako kiwe sehemu fulani juu.

“Kwa hiyo kama mkiniuliza kwamba unategemea Paul awe Mchezaji Bora wa kila mechi? Jibu ni hapana? Kama unategemea afunge mabao katika kila mechi? jibu ni hapana.

“Lakini nategemea Paul --na nadhani ajipe changamoto hii mwenyewe -- kutunza kiwango chake na sio kucheza vizuri mechi moja na vibaya mechi nyingine.”

Mreno huyo alisema anategemea Pogba aonyeshe kiwango cha juu katika mechi na mazoezini.

“Lazima kiwango chake kisitetereke, kwanza mazoezini wakati wa mazoezi ya wiki na kwa wiki mbili hadi tatu zilizopita nimekuwa nikiridhishwa naye,” alisema Mourinho.

Kabla ya mchezo baina ya City na Man U, Guardiola alikumbusha kuwa aliwahi kupewa fursa ya kumnunua Pogba na Henrikh Mkhitaryan wakati wa dirisha dogo na bado anadhani Pogba atamfaa kikosini kwake.

Pogba ambaye alichangia kiasi kikubwa kuharibu sherehe za ubingwa za City, alifuatwa na Guardiola katikati ya uwanja baada ya mchezo huo na kuzungumza naye, kabla ya Mfaransa huyo kuwafuata mashabiki kushangilia pamoja na.

Kwa waandishi wa habari, Mourinho alisema: “Amecheza mpira mkubwa, lakini suala la kwamba kazungumza nini na Pep mimi msiniulize kwa sababu sijazungumza naye kuwa wameongea nini na Pep.

“Pia msiniulize suala la Pogba na wakala wake Mino Raiola. Mimi sijui wamezungumza nini, sijui.”

Hata hivyo, Mourinho amesema anaamini City watatumia fedha nyingi kufanya usajili msimu ujao, lakini akasema Manchester United haitaiga.