Nandy atamani kuwa kama Beyonce

Saturday March 11 2017
nand

Nandy ndiyo jina ambalo anajulikana zaidi katika uwanda wa muziki wa kizazi kipya akitokea katika Nyumba ya Vipaji (THT).

Umaarufu wa Faustina Mfinanga (23) ulikuja baada ya kushika nafasi ya pili katika mashindano ya Tecno Own The Stage.

Starehe limezungumza na Nandy mapema wiki hii ambaye ameweka wazi kuhusu mambo mengi ikiwamo muziki, vitu anavyovihusudu katika maisha yake na mipango mbalimbali ya kazi zake.

Umekuwa ukikaa muda mrefu kabla ya kutoa nyimbo mpya kwa nini?

Kwa sababu nataka kazi zangu ziishi zaidi masikioni mwa mashabiki wangu. Lakini, natarajia Aprili mwaka huu nitaachia wimbo mwingine, audio na video nitatoa lakini sijajua ni wimbo gani utaanza kwa sababu mpaka sasa tayari ninazo nyingi. Kwa sababu ya ubora wa kazi zangu zinaishi muda mrefu kama One Day inafanya vizuri kwa sasa ninaipa muda mrefu.

Unafikiri kuondoka THT?

Advertisement

THT ni chuo ambacho kinafundisha. Kwa kweli sijafikiria kuondoka hapo kwa kuwa tayari nipo chini ya lebo.

Kuna vitu hatarishi katika shughuli zako za kimuziki, unafanya nini kujiepusha navyo?

Naamini kwenye kazi nzuri na namwomba Mungu kwa kweli. Vishawishi ni vingi na ni jinsi mtu alivyo ndivyo vitampata, mimi situmii pombe na vingine.

Una tattoo (michoro mwilini)?

Sijawahi kufikiria kuchora na sitarajii kwa sababu sioni kama ina umuhimu katika maisha yangu.

Siwezi kuutoboa mwili wangu kwa kuwa nitakachokichora hakitakuwa na maana kwa maisha yangu ya baadaye.

Mitandao ya kijamii ina nafasi gani kwako?

Mitandao ya kijamii inasaidia kwa sisi wanamuziki kusambaza vitu vyetu vya muhimu na pia inaharibu kwa kuwa wengine wanaitumia vibaya. Kwa mfano mimi maisha yangu mwenyewe binafsi kwa nini niyaanike katika mitandao ya kijamii?

Unafikiri utaweza kushinda vishawishi ukiwa msanii wa kike mwenye umri mdogo?

Nimemweka mbele Mwenyezi Mungu, pia Watanzania waniweke kwenye sala zao. Nimepanga vitu vingi kwenye muziki wangu nataka kuwa  zaidi ya mastaa wa kike Bongo, siwezi kuwaangusha naona ndiyo kwanza naanza, nataka kuwa kuwa Beyonce wa Bongo.

Advertisement