JULIANA SHONZA : Nilihama Chadema baada ya kugundua Natumika vibaya

Juliana Shonza

Muktasari:

‘Shikamoo dada’ nageuka nyuma na kugundua kuwa ni Juliana Shonza naitikia na kumuomba akae. Ananijibu asante. Tunazungumza mawili matatu na kuagana kisha wote tunanyanyuka na kuingia bungeni kwa kazi iliyotupeleka.

Ni asubuhi na mapema yapata saa 2.30 hivi nikiwa katika mgahawa katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma. Msichana mdogo na mrembo mwenye rangi ya chungwa ananishika bega na kunisalimia kwa heshima.

‘Shikamoo dada’ nageuka nyuma na kugundua kuwa ni Juliana Shonza naitikia na kumuomba akae. Ananijibu asante. Tunazungumza mawili matatu na kuagana kisha wote tunanyanyuka na kuingia bungeni kwa kazi iliyotupeleka. Naweka mihadi naye, bila hiyana anakubali tuonane saa saba baada ya Bunge kuhairishwa.

Muda unafika naye kama alivyoahidi, anakuja moja kwa moja eneo ambalo tulikubalina. “Nimekuja dada.” Namkaribisha aketi tayari kwa mahojiano.

Huyu si mwingine ni mbunge wa viti maalumu CCM. Juliana ambaye awali alijulikana kama kijana wa Chadema kabla ya kukihama na kuijiunga na CCM. Juliana mwenye umri wa miaka 28 anasema, aliamua kukihama chama hicho baada ya kugundua kuwa kinatumia vijana kufanya fujo na kukosa msaada.

Mwaka 2012 akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), alipigiwa simu na mmoja wa viongozi (hamtaji) aliyemtaka aandae vijana kwa ajili ya kufanya maandamano lakini kabla hawajafika mbali polisi waliwakamata na kulazimika kulala ndani kwa siku mbili.

“Wakati wote huo niko chini ya ulinzi sikuona kiongozi yeyote aliyekuja kuniwekeza dhamana wala kunitembelea japo kunipa pole, tulifunguliwa kesi iliyodumu kwa zaidi ya miaka miwili, siku zote hizo sikuwahi kumuona kiongozi yoyote anakuja kufuatilia.”

Juliana anasema hali hiyo ilimkatisha tamaa na kuona vijana wanatumika kama chambo na hakuna dira yeyote inayowawezesha vijana.

Aliingiaje katika siasa?

Juliana anasema kuwa siasa ipo katika damu kwani alianza akiwa anasoma chuo kikuu na alikuwa mbunge wa bunge la wanafunzi, wakati huo akiwa tayari ameshajiunga na Chadema.

“Unapozungumzia vijana wa kwanza wa Chadema mimi ni mmojawapo. Mwaka 2011 nilianzisha Umoja wa Wanafunzi wa Chadema Tanzania (Taso) na nilikuwa mwenyekiti wa kwanza kabla ya kuchanguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa Baraza la Vijana Taifa (Bavicha),” anasisitiza.

Hata hivyo, Juliana anasema jambo lilomfanya ahame Chadema ni baada ya kuanza kushiriki vikao vikuu ndipo alipogundua kuwa hakuna dira yoyote ya vijana katika chama hicho pia baada ya kuanza kuhoji matumizi ya ruzuku jambo liloleta mgogoro baada ya kuhoji mapato na matumizi ya fedha hizo zinazofikia Sh300 milioni.

“Siyo hilo tu hata nilipohoji kwanini hakuna mfumo wa upatikanaji wa viti maalumu, lakini pia hakuna maandalizi yoyote ya kuchukua dola.”

Maisha ya familia

Juliana anasema alikutana na mchumba wake mwaka 2012 na miaka miwili baadaye walifunga ndoa na hawajajaliwa kuwa na mtoto. Hata hivyo, anasema kuwa anashukuru Mungu kumpatia mume mwema ambaye amekubaliana na kazi anayoifanya na wakati mwingine inamlazimu kusafiri au kurudi usiku hasa kipindi cha kampeni.

“Kwangu siasa ni maisha hata wakati ananichumbia nilimjulisha kuwa mimi ni mwanasiasa na akakubalina hilo, ananisaidia kunishauri nini nifanye ili niweze kufanikiwa, amekuwa msaada kwangu.”

Juliana anasema anapopata nafasi akiwa nyumbani anapenda kupika ili kuhakikisha anamuandalia mumewe chakula kizuri anachopenda.

Vikwanzo anavyokutana navyo

Juliana anasema, changamoto kubwa ni kudhaniwa malaya ingawa yeye huipuuza kwani anaamini suala la mapenzi ni makubaliano baina ya watu wawili.

Anasema tatizo jingine ni mfumo dume hasa pale jamii inapoamini kuwa mwanamume ndiye mwenye uwezo na kutokubali kuwa wanawake pia wanaweza.

Katika hilo Juliana anamshukuru Rais mstaafu Jakaya Kikwete kwa kuwapa nafasi wanawake jambo linaloonekana kuendelezwa na Rais wa Awamu ya Tano, Dk John Magufuli.

Matarajio yake

Juliana anasema kuwa kitu ambacho hatakisahau ni pale wanawake wa Mkoa wa Songwe walimchagua kuwa mwakilishi wao na kuwaahidi kuwatumikia.

“Kwanza nimeingia bungeni nikiwa nimejipanga kuitumia vizuri nafasi hii, walionichagua waone hawajafanya makosa, nitakuwa sauti ya wanawake na vijana lakini kikubwa zaidi, nawashauri wanawake wenzangu wasikate tamaa, tujiamini, tujitambue tusome kwani elimu ndiyo msingi wa kila nafasi,”

Juliana Shonza ni nani?

Ni mtoto wa kwanza kati ya wanne wa mzee Shoza. Alizaliwa mwaka 1987 mkoani Mbeya na kwa sasa unajulikana kama Mkoa wa Songwe.

Mwaka 1995 alianza elimu yake ya msingi katika Shule ya Msingi Mwenge na baadaye kujiunga na Shule ya Sekondari Kibasila. Alihitimu kidato cha nne na mwaka mwaka 2006 na alijiunga na kidato cha sita katika Shule ya Sekondari Dakawa.

Mwaka 2008 alifanya Shahada yake ya kwanza ya Sayansi ya jamii katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na baadaye aliendelea na masomo ya Shahada ya pili katika fani hiyo chuoni hapo.

Kwa sasa Juliana ni mbunge wa viti maalumu kwa tiketi ya CCM chama ambacho alihamia rasmi kwama 2013 na kukabidhiwa kadi na Mwenyekiti wa chama hicho, Jakaya Kikwete akiwa mjini Dodoma.