Tamu na chungu ya matumizi ya mitandao kwa wanafunzi

Muktasari:

  • Wapo waliojikuta wakipata sifuri kwenye mitihani yao, kwa sababu ya matumizi ya simu na mitandao.

“Niliumia nilipoona wameweka picha za utupu kwenye akaunti yangu ya facebook.Kibaya zaidi picha hizo walizitengeneza, yaani sura yangu ila mwili haukuwa wangu. Nilitamani kuacha shule ila nashukuru namaliza,”

Hivi ndivyo anavyosimulia mmoja wa wanafunzi wa sekondari (jina na shule vinahifadhiwa) aliyewahi kufanyiwa ukatili wa kingono kwenye mitandao ya kijamii, kiasi cha kuathirika kisaikolojia.

Mwanafunzi huyo anaamua kupaza sauti yake baada ya wasomi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Elimu (Duce) kuanzisha mfumo wa kujadili tafiti mbalimbali za kielimu wanazofanya.

Siku ya simulizi ya mwanafunzi huyu, wasomi hao walikuwa wakijadili utafiti kuhusu matumizi ya mitandao ya simu na athari zake kwa wanafunzi.

Mwanafunzi huyo anasema kuwa alikuwa anamiliki akaunti kwenye mtandao wa kijamii wa facebook, lakini aliacha baada ya kudhalilishwa na watu asiowajua waliotengeneza picha zake na kuzisambaza.

INAENDELEA UK 14

INAtoka uk 13

“Baba alininunulia simu kwa ajili ya kurahisisha mawasiliano, kwa hiyo nikawa namiliki akaunti kwenye mitandao ya kijamii, lakini niliacha kwa sababu naogopa tena kudhalilishwa kama ilivyotokea, ”anaeleza.

Usemavyo utafiti

Mwanafunzi huyo sio peke yake aliyefanyiwa ukatili kwenye mitandao.

Kwa mujibu wa utafiti huo, asilimia 80 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza hadi cha nne wanatumia mitandao, wakati asilimia 50 wanamiliki simu na wengi wao wameshakutana na ukatili wa aina mbalimbali, ukiwamo wa kingono.

Mtaalamu wa masuala ya kisaikolojia na makuzi ya watoto kutoka Duce, Dk Hezrone Onditi anasema utafiti alioufanya katika mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza, unaonyesha kuwa watoto wengi wanafanyiwa ukatili wa kingono kwenye mitandao hiyo.

Mtafiti huyo anasema wapo waliojikuta wakipata sifuri kwenye mitihani yao kwa sababu ya matumizi ya simu na mitandao.

“Wengine waliumizwa kisaikolojia kwa kufanyiwa ukatili wa kingono kwenye mitandao, lakini wapo waliofaulu vizuri, kwa sababu walitumia kwa ajili ya masomo,”anasema.

Anasema kibaya zaidi asilimia 50 ya wasichana wanaotumia simu za mkononi na mitandao ya kijamii wazazi wao hawajui suala hilo.

Hata hivyo, anasema katika utafiti huo walibaini kuwa wavulana wanatumia zaidi simu na mitandao kuliko watoto wa kike.

“Tuligundua kuwa asilimia 76 ya wanafunzi hawa wanatumia zaidi simu wakiwa nyumbani. Kwa hiyo suala kwamba, wanafunzi wanatumia simu na mitandao ya kijamii hilo lipo,”anasema.

Athari za matumizi

Dk Onditi anasema zipo athari nyingi za matumizi ya mitandao na simu kwa watoto walio chini ya umri wa miaka 18.

“Ni wazi kwamba wanapokuwa kwenye matumizi yao ya kawaida ya simu na mitandao, wanakutana na picha za utupu na za ngono,” anaeleza.

Anasema wengi wamejikuta wakifanyiwa ukatili wa kingono kwenye mitandao hiyo jambo ambalo limekuwa likiwaathiri zaidi kisaikolojia.

Anasema mwanafunzi anapoathirika kisaikolojia, jambo hilo ndilo hutawala ubongo wake kila wakati kwa kutafuta suluhisho na wakati mwingine kuona kama amedhalilishwa.

“Kwa hiyo ukifika muda wa masomo hawezi kuelewa na mwishowe anafeli masomo yake. Atawaza jinsi gani apambane na lile linalomsumbua kichwani kwake,”anaeleza.

Mtaalamu huyo wa saikolojia na makuzi ya mtoto, anasema wanafunzi wengi aliowahoji wameelezea namna wanavyoshindwa kumudu masomo yao au walivyofeli kwa sababu ya kuwaza ukatili waliofanyiwa kwenye mitandao ya kijamii.

Mtaalamu mwingine wa kisaikolojia kutoka taasisi ya vijana na makuzi, Dk Frank John anasema wasichana wengi wamejikuta wakiingia kwenye uhusiano bila kutarajia kwa sababu ya matumizi ya simu.

Ofisa programu kutoka HakiElimu, Florige Lyelu anasema ni hatari kubwa kwa mtoto kutumia simu na mitandao ya kijamii bila wazazi wake kujua.

“Mzazi unapokuwa hujui mtoto wako akiwa kwenye mtandao anakutana na nini ni hatari zaidi, hata kama unadhani mwanao amekua kumbuka yupo chini ya miaka 18,”anasema.

Mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tigan Gichomu anasema ni vizuri mitandao na simu vitumike kwa ajili ya mawasiliano na kimasomo, vinginevyo athari zake ni kubwa.

Faida za matumizi ya mitandao

Dk Onditi anasema katika utafiri wao walibaini wapo wanafunzi wanaotumia mitandao hiyo kwa ajili ya mawasiliano na wengine kitaaluma.

“Wengine wanawasiliana shule kwa shule na kubadilishana mambo wanayosoma, hili ni suala jema,”anasema.

Anasema wapo walimu walioweka mafunzo mengi kwa njia ya picha kwenye mitando hiyo ikiwamo ‘You Tube’ ambayo wanafunzi wakipata fursa ya kusikiliza wanaweza kufanya vizuri darasani.

Mwanafunzi Simon Moses wa Shule ya Sekondari ya mazoezi ya Chang’ombe, anasema katika matumizi yake ya simu na mitandao, amekuwa akikwepa matumzi yasiyo sahihi kwa sababu tayari anajua athari zake.

“Sio kwamba sikutani na picha za ajabu, nakutana nazo sana, lakini simu yangu naitumia kitaaluma na kuwasiliana na wenzangu,”anasema.

Ushauri wa wadau

Watafi wanashauri kuwapo kwa sera na sheria zitakazokuwa zinawalinda watoto dhidi ya ukatili wa kimitandao.

Anasema kwa sasa sera na sheria zilizopo haziwataji watoto moja kwa moja.

“Itafikia hatua watoto watakaa na simu darasani kwa sababu dunia inabadilika, sasa kinachotakiwa kufanywa ni kujua namna ya kuwalinda,”anasema.

Anasisitiza wazazi wawe karibu na watoto wao na kujua nini wanachokifanya kwenye mitandao ili iwe rahisi kuwasaidia.