Tarura iboreshe barabara, kuinua uchumi vijijini

Thursday January 18 2018

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango.

Joseph Alphonce  ni Mtakwimu na Ofisa Mipango. Anapatikana kwa 0685214949/0744782880. 

By Joseph Alphonce

        Serikali imeanzisha Wakala wa Barabara Vijijini (Tarura) ambao utatekeleza majukumu ambayo awali yaliyokuwa chini ya Serikali za Mitaa.

Halmashauri kwa sababu mbalimbali, zilishindwa kusimamia na kutekeleza miradi mingi ya barabara. Utafiti mbalimbali unaonesha kila mwaka miradi ya barabara mjini na vijijini ilikuwa ikikamilika kwa wastani wa asilimia 30 tu. Mingi haikukamilika.

Tarura, pamoja na majukumu mengine ina malengo makuu matatu ambayo ni kuhakikisha barabara zinapitika muda wote, kupunguza gharama za matengenezo kwa vyombo vya moto vinavyotumia barabara husika na kupunguza muda wa safari.

Ni matumaini ya kila Mtanzania kuona Tarura inakuja na ufumbuzi wa changamoto zilikuwa zinasabisha halmashauri kutekeleza miradi ya barabara kwa wastani wa asilimia 30.

Utekelezaji makini wa majukumu ya Tarura utawezesha wananchi kujikwamua kiuchumi kutokana na unafuu utakaokuwepo kutokana na kuimarika kwa miundombinu ya usafirishaji hivyo kuhakikisha kila mmoja ananufaika na ukuaji wa uchumi wa nchi.

Wafugaji, wakulima na wafanyabiashara wadogo, kati na wakubwa watanufaika kwa ubora wa miundombinu ya barabara vijijini ambako bidhaa nyingi ama hununuliwa au kuuzwa huko.

Tarura ina inapaswa kuhakikisha barabara zinapitika muda wote. Jukumu hili lina manufaa kwa ukuaji wa uchumi maendeleo ya mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla. Mzalishaji wa bidhaa hatakuwa na hofu ya kufika sokoni kwa kwa wakati na kuuza bidhaa zake pasi na kuharibika njiani.

Miundombinu imara ya barabara itashawishi wafanyabiashara wa magari ya abiria na mizigo kuingiza vyombo vyao kwenye shughuli za usafirishaji. Fursa za ajira zitaongezeka, Serikali itapanua wigo wa makusanyo ya kodi na yasiyo ya kodi.

Pato la Taifa litakua hivyo wastani wa pato kwa kila mwananchi nalo litaongezeka. Kupitia makusanyo yake Serikali itakuwa na wigo mpana wa kuboresha na kuimarisha miundombinu ya barabara na maeneo mengine yenye uhitaji.

Wanufaika wa barabara badala ya kutumia fedha nyingi kugharamia matengenezo ya vyombo vya usafiri wataelekeza fedha hizo kwenye utekelezaji wa majukumu mengine ambayo yatasaidia kupunguza changamoto ya ajira na kuongeza mapato.

Halikadhalika watu watapata muda mwingi wa kutekeleza shughuli za maendeleo kwa kuzingatia ukweli kuwa muda wa safari kutoka sehemu moja kwenda nyingine utakuwa umepungua kutokana na uimara huo wa miundombinu utakaoruhusu kasi kubw aya vyombo vya moto.

Kwa mfano, miaka kadhaa iliyopita wakazi wa Bariadi kutokana na ubovu wa miundombinu walilazimika kutumia zaidi ya saa 16 kusafiri kutoka wilayani humo hadi jijini Mwaza. Baada ya Serikali kuimarisha miundombinu sasa wanatumia wastani wa saa tatu mpaka nne.

Muda mwingi ambao watu walitumia kusafiri umeokolewa hivyo kuutumia kwenye shughuli nyingine za maendeleo. hakuna taifa lililowahi kuendele abila wananchi wake kufanya hivyo kwanza.

Ukiangalia, nchi yenye mabilionea wengi nayo ni miongoni mwa mataifa tajiri. Huko, huduma nyingi za jamii na miundombinu pamoja na vyote vinavyohitajika kwa binadamu vina ubora unakubalika kimataifa.

Wananchi hawawezi kuendele akama miundombinu inakwaza wao kutekeleza majukumu yao. Mawasiliano ni kitu muhimu kwa ulimwengu wa sasa. Inapokuwa rahisi kwa mtu kusafiri kutoka sehemu moja kwend anyingine kunatoa fursa ya kufanya mambo mengi kwa wakati mmoja.

Chukua mfano, endapo ingekuwa inawezekana kutumia saa moja kusafiri kutoka Morogoro mpaka Dar es Salaam bila shaka Dar isingekuwa na foleni ndefu zinazowafanya wakazi wake wapoteze muda mwingi. Watu wangekuwa radhi kuishi Morogoro na kufanya kazi jijini humo.

Hayo yote yatawezekana endapo miundombinu itaimarishwa. Juhudi zinazoonyeshwa na serikalikwa kuimarisha miundombinu ya usafiri hasa barabara, anga na reli zikiunganishw ana kitakachofanywa na Tarura huenda ikafanikisha mtu kuishi mji mmoja na kufanyakazi mji mwingine.

Watumishi watakopata nafasi ya kuingia Tarura wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, ubunifu na uzalendo kwa kutambua kuwa wana dhamana ya kuhakikisha miundombinu ya barabara inaboreshwa na kutumika kama fursa ya kukuza uchumi wa kaya na taifa kwa jumla.

Wanapaswa kutekeleza miradi watakayokabidhiwa kwa uaminifu ili iwe na viwango vitakavyodhihirisha thamani ya fedha itakayotumika. Rushwa iepukwe na ubora uzingatiwe kwani hata nao watanufaika na urahisi utakaopatikana baada ya kukamilika.

Takwimu zinaonyesha Watanzania wengi wanaishi vijijini na wanategemea kilimo. Kufanikisha mapambano dhidi ya adui umasikini, kundi hili lazima liwekewe mazingira rafiki ya kukuza kipato. Barabara imara zinazopitika mwaka mzima ni miongoni mwa kitu muhimu kinachohitajika kufanikisha lengo hilo.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango wa halmashauri     

Advertisement