Tuache tabia ya kubembeleza wahalifu

Wednesday February 14 2018

 

Kwa kiasi fulani tunaweza kusema kasi ya biashara na matumizi ya dawa za kulevya Zanzibar imepungua katika siku za karibuni.

Siku hizi utawaona vijana wachache waliokubuhu kwa matumizi ya dawa hizi wakisinzia ovyo katika vijiwe, tofauti na hali ya iliyokuwapo miaka kama mitatu hivi iliyopita.

Hapa watu na taasisi zilizojikita katika kampeni ya kuelimisha vijana kutokana na janga hili na zaidi Jeshi la Polisi kwa kuvalia njuga suala hili wanastahiki kuwavulia kofia na kuwapa pongezi kwa kazi nzuri iliyofanyika.

Hata hivyo, bado kazi iliyobakia ya kuirejesha hali ya visiwani kuwa ya kawaida kama ilivyokuwa miaka iliyopita si ndogo hata kidogo.

Kwa maana hiyo polisi wanapaswa kuwa na mikakati mizuri zaidi kusafisha uozo uliopo kumaliza tatizo la dawa kulevya.

Naamini kwa kuelewa kazi nzito iliyobakia ndio tukamsikia Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mjini Magharibi, Hassan Nassir Ali ambaye juhudi zake za kuongoza mapambano dhidi ya uhalifu katika mji wa Unguja akiahidi kuwasaka wauza dawa za kulevya.

Kwa kweli ahadi ya kamanda Nassir si tu inafaa kupongezwa bali pia kuungwa mkono na kila raia mwema.

Hata hivyo, ahadi hiyo ingefaa kuonekana utekelezaji wake, badala ya kuwapa wahalifu taarifa ya kuwapo mpango wa kuwasaka.

Biashara ya dawa ya kulevya ni ya hatari na kwa hivyo wanaojiingiza katika biashara hii hawapaswi kupewa fununu ya kuwepo msako mkali wa kuwabana.

Kwa vile watu hawa wamezipa mgongo sheria na wamejitokeza kifua mbele kuharibu maisha ya maelfu ya watu kwa kuwauzia dawa hizi hatari, hawastahiki wema wa aina yoyote ile, isipokuwa kukamatwa na kuwajibishwa kisheria.

Panapotokea mtu hataki kuheshimu sheria ni wajibu wa vyombo vya dola kumuwajibisha kisheria.

Mwaka jana nilielezea katika safu hii kutofurahishwa na tangazo la Kikosi cha Usalama Barabarani cha Zanzibar kuwaambia wanaoutumia gari walizouziwa na Serikali bila ya kubadili namba, badala ya kutangaziwa ni vizuri wangekamatwa na kushtakiwa kwanza.

Sikufahamu mantiki ya tangazo kwa sababu walichofanya watu wale ni uhalifu na hawakustahiki kupewa onyo. Hii ni kwa sababu kila mtu, pamoja na hao waliouziwa hayo magari, anajua kuwa mtu binafsi, hata akiwa waziri, hawezi kutumia gari lake likiwa na namba za Serikali.

Uzoefu umeipelekea jamii kujenga imani kuwa gari lenye namba za Serikali halitumiki kufanya uhalifu, ijapokuwa zimekuwapo taarifa za baadhi ya magari hayo kutumika vibaya na hasa kusumbua raia wasiokuwa na hatia.

Hatari niliyoona wakati ule ni kwamba kuruhusu watu binafsi kutumia magari yenye namba za Serikali ni kutoa mwanya wa kuyatumia kusafirishia majambazi, bidhaa za wizi, gongo, bangi na dawa za kulevya.

Haiwezekani na haikubaliki kuwaambia wanaouza dawa za kulevya kwamba dawa yao ipo jikoni.

Tuiache dawa ichemke polepole bila ya wao kujua, baadaye tuwashtukize na kuwanywesha kwa kuwakamata na kuwapeleka mahakamani.

Hili si suala la kupeana onyo au kubembelezana. Hawa watu ni hatari na hawafai kupewa onyo la aina yoyote kwani kama wangekuwa na chembe za utu basi wangefanya biashara nyingine na sio ya kuuza dawa za kulevya.

Onyo la kuwepo msako linawasaidia hawa majahili kuchukua hatua za kuhakikisha hawakamatwi na ushahidi utakaomtia hatiani wakati nyumba zao zitakapopekuliwa.

Watu hawa wanapopata fununu ya kuwepo msako, basi hulala kifudifudi na kujifanya ni watu wema na wacha Mungu.

Labda hapa kwa mara nyengine nitoe mfano wa namna watu waliojua nyumba zao zingepekuliwa kutafuta gongo walivyofanya waonekane sio tu wahalifu bali ni wanapenda amani na wenye kufuata sheria.

Miaka michache iliyopita Jeshi la Polisi Zanzibar lilitangaza tarehe ya kuanza zoezi la nyumba zinazouza gongo.

Zoezi likafanyika na polisi walipofika katika nyumba moja maarufu inayouzwa gongo wakakuta mazingira safi na kulikuwa sio tu hapauzwi gongo bali hata wateja hawakuwapo.

Askari walipofika hapo waliamini wangefanikiwa kuwanasa wauzaji na watumiaji wa gongo baada ya kuona pikipiki na baisikeli zimeegeshwa nje ya hio nyumba.

Polisi waliingia ndani bila ya kupiga hodi na kukuta watu wamekaa kwenye jamvi, wengi wakiwa na kanzu na wamekamata tasbihi wakifanya ibada.

Pembezoni palikuwapo sanduku kubwa lililojaa misahafu na vitabu vya maulidi, birika la kahawa, bakuli la vikombe vya kahawa, halua, tende na visheti.

Askari walikaribishwa kwa furaha na kuombwa waende uani kutia udhu (kuuweka mwili safi kama wanavyofanya Waislamu wanapotaka kusoma kitabu kitukufu cha Kuran au wanapotaka kusali) ili wajiunge na ibada.

Polisi walibaki wameduwaa na kutazama usoni na hakuna aliyeweza kutamka jambo. Katika baadhi ya nchi hali iliyojitokeza pale hutengenezewa mchezo mfupi wa kuchekesha au wa sinema ili kuifurahisha jamii.

Hapa tujiulize: Hivyo kweli baada ya kutolewa tangazo la kusaka gongo askari watarajie wawakute walevi wakiwa na vinywaji vyao wakati tayari walishaambiwa kuwepo msako wa nyumba hadi nyumba zinazouza gongo?

Au vipi utatangaza msako wa makahaba wanaojificha katika pembezoni mwa barabara usiku na ufike hapo na kuwakuta wanangojea wateja wakati walijua siku ile walikuwa wanasakwa.

Ni vizuri kamanda Nassir na askari wake wakaendeleza mapambano kimyakimya na hata bila ya kuviarifu vyombo vya habari na baada ya kuwakamata wanaouza dawa za kulevya ndio mambo yawekwe hadharani.

Wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni wauaji na hawafai kuonewa huruma wala kufanyiwa wema au hisani. Sheria za kupambana nao zipo na tuzitumike bila ya muhali ili kuinusuru Zanzibar na watu wake.

Advertisement