Ubia wa Serikali, sekta binafsi utaimarisha miundombinu nchini

Thursday January 18 2018

 

By Profesa Honest Ngowi

        Suala la ubia kati ya Serikali na sekta binafsi ni miongoni mwa masuala makubwa ya kimjadala duniani. Ni dhana muhimu katika maendeleo ya uchumi inayotambua Serikali pekee haiwezi kufanya kila kitu. Pia, sekta binafsi nayo haiwezi kufanya kila kitu.

Kuna mambo yanayofanywa vizuri na sekta ya umma na mengine yakifanywa vizuri zaidi na sekta binafsi. Hata hivyo yapo mambo yanayofanywa vizuri zaidi kwa ubia wa sekta hizi.

Katika makala haya, ni sehemu ya mada iliyowasilishwa na mwandishi wa makala haya kwa wanafunzi 40 wa shahada ya uzamili katika biashara (MBA) wa Chuo Kikuu cha Harvard vkilichopo nchini Marekani ambacho ni kati ya vyuo bora zaidi duniani. Mada ilitolewa wiki hii, Januari 15.

Ubia

Ubia kati ya Serikali na sekta binafsi ni huunganisha nguvu kukamilisha jambo maalumu. Kila mbia anatoa mchango wake ili kukamilisha jambo lililopo mezani. Kati ya shughuli zinazoweza kufanywa kwa ubia ni pamoja na ujenzi wa miundombinu mikubwa.

Hii ni pamoja na barabara, madaraja, vituo vya magari, viwanja vya ndege na reli. Shughuli nyingine ni ukusanyaji wa mapato, usafi na uendeshaji wa shughuli mbalimbali za umma.

Kufanikisha jambo lililokusudiwa, kila mbia hutoa mchango ambao huweza kuwa fedha, utaalamu, uzoefu au uthubutu.

Michango ya wabia hutofautiana. Huweza kuwa asilima 50 kwa 50 au mfumo mwimgine watakaokubaliana. Bila kujali ukubwa wa mchango katika ubia husika, ni muhimu kila upande kuwa na sauti na kuheshimiwa.

Ubia ni muhimu ili wahusika wakamilishane katika mapungufu yao. Kuingia au kutokuingia katika ubia kutategemea wabia wanataka ushirikiano wao uwafanyie nini.

Kwa sekta binafsi jambo la msingi mwisho wa siku ni kutengeneza faida. Kwa sekta ya umma jambo la msingi ni huduma kwa jamii, ufanisi, mtaji, ubunifu na faida nyinginezo zitokazo sekta binafsi.

Aina za ubia

Zipo aina mbalimbali za ubia kati ya sekta ya umma na binafsi. Uamuzi wa namna ya kutekeleza ubia hutegemea hali halisi na kile kinachotafutwa katika ubia husika na ukubwa wa mradi husika pamoja na muda wa utekelezaji wake.

Mbia kutoka sekta binafsi huweza kujenga, kuendesha na kuukabidhi mradi husika serikalini baada ya kurejesha gharama zake na kupata faida waliyokubaliana. Ubia huweza pia kutekelezwa kwa sekta binafsi kuendesha mradi kimenejimenti au kwa kushirikiana na Serikali.

Mambo ya kuzingatia

Yapo mambo mbalimbali muhimu yanayohitaji kuzingatiwa ili ubia ufanikiwe. Mambo haya ni pamoja na sera, sheria na udhibiti. Hali halisi ya kisera, kisheria na kiudhibiti kwa ujumla wake na katika muktadha wa ubia katika nchi husika.

Sera, sheria na udhibiti mzuri, rafiki na wa kuvutia ni muhimu sana katika kuvutia na kubakiza wabia katika miradi mbalimbali. Pamoja na mambo mengine, sera lazima zitabirike, ziwe shirikishi na zenye mashiko kwa wabia hasa wa sekta binafsi.

Vilevile sheria katika ujumla wake na zile za biashara na mikataba kimahususi ni lazima ziwe rafiki, wezeshi na za kuvutia kwa wabia. Udhibiti ni muhimu lakini lazima uwe udhibiti mzuri na wezeshi kwa wabia.

Ili wabia waweze kupata wanachotaka ni lazima wawe na uwezo mkubwa wa kuelewa mambo yote muhimu katika ubia. Haya ni pamoja na yale ya kitaalamu na ya kawaida. Pale mbia anapokuwa hana ujuzi husika, ni vyema kutumia wataalamu kupata ushauri.

Miundombinu

Kama ilivyoelezwa awali, ubia unaweza kufanywa katika sekta yoyote ile. Kati ya sekta hizi ni pamoja na miundombinu ya aina tofauti.

Kwa mazingira ya nchi zinazoendelea kama Tanzania miundombinu husika katika ubia ni ya aina nyingi. Ipo midogo na mikubwa. Ipo ya Serikali Kuu na Serikali za Mitaa.

Mifano ya miundombinu inayoweza kutekelezwa kwa ubia ni pamoja na vituo vya mabasi. Mfano mzuri na mpya ni Kituo cha Mabasi cha Msamvu kilichopo mkoani Morogoro kinachohusisha Shirika la Hifadhi ya Jamii la Serikali za Mitaa (LAPF) na Halmashauri ya Manispaa Morogoro.

Pia ipo miundombinu kama madaraja. Mfano mzuri ni Daraja la Kigambano linalohusisha Shirika la Hifadhi ya Jamii (NSSF) na Serikali Kuu. Miundombinu ya masoko ni pamoja na Soko la Kimataifa la Mwanjelwa la mkoani Mbeya linaloihusisha Benki ya CRDB na jiji hilo.

Mifano ipo mingi ikiwamo Kituo cha Mabasi cha Moshi Mjini na Soko la Mburahati linalohusisha Vibindo na Halmashauri ya Kinondoni japo bado mchakato unaendelea.

Faida

Sekta binafsi hunufaika kwa fedha itakazopata baada ya mradi kukamilika wakati Serikali itapunguza matumizi ya fedha ambazo zingehitajika kuukamilisha mradi uliopo kwenye makubaliano ya ushirikiano huo.

Hili hutokea kwa sababu sekta binafsi hutoa mtaji hivyo kuiruhusu Serikali kutumia fedha zake kwenye mambo mengine muhimu kwa ajili ya maendeleo ya wananchi kama vile usambazaji wa maji, afya, elimu, ulinzi na usalama.

Pia, Serikali hupata muda mzuri wa kufanya kazi za umma vizuri na kwa ufanisi mkubwa zaidi huku ikiachia sekta binafsi yale yanayofanywa nayo vizuri zaidi.     

Advertisement