Ujasiriamali unavyowakwamua wakimbizi wa Burundi Mkoani Kigoma

Thursday January 18 2018

Msimamizi wa kituo namba tatu cha kuchajishia

Msimamizi wa kituo namba tatu cha kuchajishia simu katika Kambi ya Mtendeli iliyopo wilayani Kakonko,  Nduimana Paul akiangalia simu za wateja wake. Kituo hicho kina soketi 96 na kinaweza kuchaji kati ya simu 25 hadi 30 kwa siku. Picha na Hadija Jumanne. 

By Hadija Jumanne, Mwananchi [email protected]

       Takwimu zilizopo za Umoja wa Mataifa (UN) zinaonyesha kuna zaidi ya watu milioni 65.3 walioyakimbia makazi yao kwa sababu tofauti.

Wanajumuisha wakimbizi kutokana na migogoro ya kisiasa kwenye mataifa yao, wanaotafuta hifadhi pamoja na walioyakimbia makazi yao.

Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi 315,000 wengi kutoka Burundi na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC). Nchi nyingi za Afrika Mashariki kama zilivyo nyingine, zinahifadhi wakimbizikutokana na migogoro inayoendelea kwa majirani zao.

Uturuki inaelezwa kuwa na wakimbizi wengi zaidi duniani wanaofika milioni 1.9 kutoka Syria. Kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia wakimbizi Duniani (UNHCR) na wadau wengine, mataifa haya hufanikiwa kukidhi mahitaji ya waathirika hao wa migogoro ya kisiasa na kiuchumi inayoendelea kwenye nchi zao.

Mwanzo, juhudi zilielekezwa kukidhi mahitaji ya chakula, malazi na afya lakini kwa siku za karibuni, masuala ya kiuchumi pia yamepewa kipaumbele.

Nchini Uganda kwa mfano, Serikali imetenga eneo maalum na kugawa mashamba kwa mamia ya maelfu ya wakimbizi inaowahifadhi kutoka Sudan Kusini. Eneo hilo lipo katika Mkoa wa Arua. Mpango huo, unaifanya Uganda kuwa nchi rafiki zaidi kwa wakimbizi duniani.

Kwa sasa, kuna makambi matatu ya wakimizi nchini; Nduta, Mtendeli na Nyarugusu zote zikiw amkoani Kigoma ambako juhudi za kuwawezesha kiuchumi wananchi hao wa mataifa jirani zinaendelea.

Desemba 2016, Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) lilianzisha utaratibu wa kutoa fedha taslimu, pamoja na mgao wa chakula na huduma nyinginezo kwa wakimbizi 10,000. Kutokana na mafanikio yaliyodhihirika, mpaka mwishoni mwa mwaka jana lilipanga kupanua mpango huo na kuwafikia wakimbizi 80,000.

Ukiacha vyakula wanavyogawiwa, wakimbizi hao walikuwa wanapewa Sh20,000 kila mwezi ili wanunue vyakula vya ziada kutoka kwa wananchi wanaozunguka makambi waliyomo jambo lililowawezesha kiuchumi.

Kuendelea kufanikisha huduma hizo, WFP inasema inahitaji Dola 6.8 milioni kwa mwezi ili wakimbizi hao wapate mgao wa chakula na fedha taslimu.

Kuongeza uhuru wa kipato kwa wakimbizi hao, UNHCR kwa kushirikiana na wadau wengine limekuja na mbinu mpya ya kutoa mafunzo ya ujuzi kwa wakimbizi vijana waliopo katika kambi za Mtendeli na Nduta.

Taasisi ya Good Neighbors Tanzania (GNTZ) imeanzisha vikundi vya ujasiriamali kwa wakimbizi ambavyo pamoja na mambo mengine, vinatoa huduma ya kuchajisha simu na vifaa vingine vya kiektroniki.

Ofisa mwandamizi wa taasisi hiyo, Hery Aidan mradi huo umeanzishwa kwa wakati muafaka kwa wakimbizi hao kutoka Burundi.

Anasema mradi unalenga kuwawezesha wakimbizi hao kujipatia kipato kipato cha ziada kupitia ujuzi wanaoupata lakini pia watakaporudi nchini kwao, wautoe kwa wenzao.

“Mradi wa kuchajisha simu umeanza kwa kutoa elimu ya biashara na ujasiriamali kwa wakimbizi wanaoishi kambini. Mafunzo haya ya miezi miwili yalianza kutolewa Julai 2017,” anasema Aidan.

Baada ya mafunzo hayo, anasema wahitimu waligawanywa katika makundi ya watu watano na kuwezeshwa vifaa vya kuchajia simu na vile vinavyotumia umeme.

Mradi huo una zaidi ya watu 20, Kambi ya Mtendeli kuna vituo vinne wakati Nduta na Nyarugusu kuna vituo vitano kila kambi.

Mafanikio

Msimamizi wa kituo namba tatu katika Kambi ya Mtendeli, Nduimana Paul anasema huchajisha simu na vifaa vingine kama vile tochi, kompyuta na ‘power bank’ na kila siku hupata kati ya simu 25 hadi 30.

Anasema simu ya kawaida huchajisha kwa Sh100 wakati zile za kisasa ni Sh200, tochi Sh300 na kompyuta mpakato Sh500.

“Kila kituo kinakuwa na soketi 96,” anasema Paul.

Kutokana na kushamiri kwa shughuli za kiuchumi, wakimizi hao wameunda vikundi vya kuweka na kukopa (Vicoba). Paul anasema kikundi kiomja kilichopo kambini hapo chenye wanachama 20, kimewakopesha Sh150,000 kila mmoja huku kikiwa na akiba ya Sh210,000.

Kuhakikisha kunakuwa na uendelevu wa huduma, anasema kila kituo cha kuchajisha simu hujiwekea akiba ya asilimia 10 ya fedha wanayoipata kutokana na kuchajisha simu kwa wiki.

“Kiasi kinachotunzwa ni kwa ajili ya kufanya marekebisho madogo madogo endapo chaja zitaharibika au kuziongeza kama watapata wateja wengi,” anasema.

Kumbukumbu za mapato hutunzwa. Oktoba 2017, kituo cha kwanza kambini hapo kilipata Sh109,800 na Novemba kikapata Sh987,000. Kituo cha pili kilipata Sh37,200 na Sh75,900 katika miezi hiyo miwili.

“Kituo cha tatu wamekusanya Sh196,400 Oktoba huku Novemba wakipata Sh167,100 na kituo cha nne walipata Sh46,300 Oktoba na Sh59,700 Novemba. Utaratibu huu upo katika kambi zote tatu,” anabainisha Aidan.

Vicoba

Ofisa mikopo wa taasisi ya GNTZ, Msilanga Donge ndani ya Kambi ya Nduta anasema wameanzisha kikundi cha kuweka na kukopa kiitwacho Amazaa kuwawezesha wakimbizi kujikwamua kiuchumi.

Ofisa huyo anasema kila kikundi kina watu 25 na mpaka sana kambi hiyo ina vikundi 35 vya kuweka na kukopa.

“Kila mwanachama anatakiwa kununua hisa tano kwa Sh500 kila moja. Mwanachama hawezi kuchukua mkopo mara tatu ya fedha aliyotunza,” anasema Msilanga.

Kabla ya kujiunga na vikundi hivyo, Msilanga anasema wanachama hufundishwa kutengeneza katiba, kuchagua viongozi kabla ya kuanza kuweka fedha. Baada ya wiki mbili, wanachama wanaweza kukopa kasha kuanza kujisimamia chenyewe.

Mkuu wa Wilaya ya Kakonko, Kanali Hosea Ndagala anasema mpango huo ni mzuri kwa sababu utawasaidia wakimbizi hao kujiongezea kipato hivyo kufanya mambo mengine yanayohitaji fedha.

“Vikundi hivi vinawapa elimu ya kutunza fedha, kukuza biashara na wasaa wa kujadili mambo mbalimbali yanayohusiana na fursa za biashara,” anasema Kanali Ndagala

Ofisa anayeshughulikia kazi za kijamii kutoka ofisi ndogo za UNHCR zilizopo wilayani Kibondo, Takaaki Miura anasema vikundi hivyo vimeanzishwa ilikuinua uchumi wa wakimmbizi wanaojihusisha na biashara ndogondogo.

Donge anabainisha kuwa kuanzishwa kwa vikundi hivyo ni kutokana na kukosa nafasi ya kupata mikopo kutoka katika taasisi za fedha zikiwemo benki za biashara.

“Wakimbizi hawana uwezo wa kupata mikopo ndio maana tumeamua kuja na mbinu ya vikundi ambavyo vitawasaidia badala ya kusubiri misaada ya mashirika mbalimbali,” anasema Donge.

Mratibu wa Kikundi cha Amazaa, Bigirimana Anatol, anasema amekopa na kufanikiwa kuendeleza biashara yake ya mchele na maharage ambayo huifanya kambini humo.

“Kuna wakati nilikuwa natamani kubadilisha chakula katika familia yangu lakini nilikuwa na shindwa, lakini baada ya kujiunga na kikundi hiki, sasa naweza kubadilisha chakula” anasema Anotol mwenye mtaji wa Sh300,000.

Muweka hazina wa kikundi hicho, Shirimana Odette anasema mpaka wana mtaji wa Sh762,000 tangu kilipoanzishwa April mwaka jana.

Anasema wanachama wananufaika na mikopo na kuboresha maisha yao. Anajitolea mfano yeye mwenyewe kuwa amekuza mtaji wake wa mchele na maharage kutoka Sh100,000 hadi Sh300,000 hivyo kusaidia kukidhi mahitaji ya familia yake yenye watoto watano.

“Nanunua mchele kutoka Soko la Muungano katika Kambi ya Nduta ambalo huwakutanisha wakimbizi na wenyeji kwa Sh1,700 na kuja kuuza kwa Sh2,000 kwa kilo moja. Maharage nanunua Sh1,200 na kuuza kwa Sh1,400,” anasema Odette.

Changamoto

Donge anabainisha kuwa wanachama hawana mtaji hali inayosababisha washindwe kununua hisa. Ugumu huo unatokana na wakimbizi hao kutokuwa na shughuli maalum za kuwaingizia kipato.

Ili kuwanufaisha wanachama wote wa Kikundi cha Amazaa kwa mfano, Odette anasema wanahitaji Sh500,000. Vikundi hivyo pia vinahitaji kujenga ofisi na mahema ya kufanyia mikutano yao.     

Advertisement