Wabunge watoa ‘makucha’ kuukabili Mpango wa Maendeleo ya Taifa

Muktasari:

Kwa upande mmoja, umebainisha wabunge majasiri katika kujenga hoja za ama kushauri hatua za kiuchumi za kufuata au kukosoa hatua zinazofuatwa ambazo zinaonekana hazijafaulu kuweka uchumi katika hali nzuri. Lakini kwa upande mwingine umeonyesha wabunge ambao hawana hoja, bali wanashambulia hoja za wenzao na kujenga hoja kishabiki.

Mjadala wa mapendekezo ya Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa mwaka 2018/19 na mwongozo wa maandalizi ya mpango wa bajeti kwa mwaka 2018/19 umeibua mambo mengi.

Kwa upande mmoja, umebainisha wabunge majasiri katika kujenga hoja za ama kushauri hatua za kiuchumi za kufuata au kukosoa hatua zinazofuatwa ambazo zinaonekana hazijafaulu kuweka uchumi katika hali nzuri. Lakini kwa upande mwingine umeonyesha wabunge ambao hawana hoja, bali wanashambulia hoja za wenzao na kujenga hoja kishabiki.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai amebaini udhaifu uliopo na kuwashauri wabunge, hasa wa CCM, waibue mijadala yenye tija na kuacha tabia ya kupongeza kwa kisingizio kwamba wao ni chama tawala.

Spika anasema kwenye mambo ya msingi wawe wanafunguka, wasijifungefunge kwa kuwa CCM haitaki mipango mibovu..

Ndugai anakwenda mbali kuwa Katiba haikuweka utaratibu wa mipango ya nchi kupita na kujadiliwa bungeni kwa bahati mbaya, bali ililenga wabunge hao waseme kwa niaba ya wananchi.

Baadhi ya wabunge wanatambua wajibu huo na wengine hawajui. Miongoni mwa wanaotambua wamo Hussein Bashe (CCM) Nzega, Peter Serukamba (CCM) Kigoma Kaskazini na Freeman Mbowe wa Chadema katika Jimbo la Hai, ambao waliotoa michango ifuatayo. Endelea.

Hussein Bashe

Mbunge huyo anaanza kwa kutaja vigezo vya kupima uchumi wowote duniani akisema una kioo na kioo cha uchumi unaokua au kusinyaa au unaoshuka ni taasisi za fedha, biashara na soko la mitaji.

Anasema mikopo kwa watu binafsi imeshuka hadi asilimia 8.9 mwaka huu kutoka asilimia 25 za mwaka 2015 huku mikopo ya kibiashara nayo ikishuka hadi asilimia tisa kutoka 24 za mwaka 2015.

“Na maneno haya siyatoi pengine, ni ripoti za Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inayoishia Juni mwaka huu. Kilimo leo ni negative tisa (hasi) kutoka asilimia sita. Uzalishaji umeshuka kutoka asilimia 30 hadi asilimia 3,” anasema.

Akigusia ukurasa wa saba katika mpango huo wa maendeleo unaoonyesha mwenendo wa ukuaji wa Pato la Taifa kuanzia 2011 hadi 2017, Bashe anasema mwaka 2011 ukuaji huo ulikua kwa asilimia 9.1.

“Uchumi wetu unasemwa unakua kwa asilimia 6.8 lakini kwa mujibu wa ripoti hii ni asilimia 5.7. Serikali haijajipanga katika kutekeleza mpango huu,” anasema.

Anasema waziri anasema watafanya uhimilishaji wa mifugo 459,000 na wanapanga kuzalisha hay (mabunda ya majani ya ng’ombe) 445,000 ambayo kitakwimu hay moja lina uzito wa kilo 25.

“Chakula hiki ukikigawa kwa siku 365 kinalisha ng’ombe 1,600 tu. Huku unapanga kuzalisha ng’ombe 400,000 lakini unaandaa chakula cha kulisha ng’ombe 1,600?” anahoji Bashe.

Kuhusu usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi, Bashe anasema ukurasa wa saba wa mpango huo, unasema kufikia Juni 2017 uuzaji bidhaa nje ulikuwa zimeshuka kwa asilimia 29.8, lakini waziri ametoa kauli zisizoridhisha.

“Waziri anatupa kauli ya kutia matumaini kwamba matarajio ni kurejea kwa uuzaji bidhaa nje kwa sababu tunajenga kukuza viwanda,” anasema.

Anasema katika ukurasa wa 26 wa mpango huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango ametaja viwanda kadhaa kikiwamo cha kuchenjua kilichopo Geita, kusindika nyama, Kisivan, Shinyanga, Mitobotobo farmas company Ltd cha kuzalisha mafuta ya kula, kuchambua pamba na kiwanda cha kufungashia Global Parking.

“Kiwanda cha kuzalisha vinywaji baridi na Sayona na kuzalisha bidhaa za ujenzi, hivi ndivyo tutasafirisha nje ya nchi ili kurudisha asilimia 26, brother! (kaka), tumeahidi kuondoa umaskini wa watu, haya siyo maneno yangu, ninanukuu maneno ya Waziri wa Mpango!

Anasema mapinduzi ya viwanda hayawezekani bila kuwekeza katika sekta ya kilimo na kwamba Serikali inajaribu kudhibiti mfumuko wa bei kwa kuwatia umaskini wakulima.

“Yaani tunadhibiti mfumuko wa bei kwa kumtia umaskini mkulima. Aina gani za uchumi hizi? Waziri amejikita kwenye kodi tu badala ya kujikita kwenye uzalishaji,” anasema.

Aidha, katika ukurasa wa 68 waziri anapozungumzia Sekta ya Kilimo, Bashe anashangazwa na uwekezaji wa Serikali katika sekta hiyo iliyobeba zaidi ya asilimia 70 ya ajira ya Watanzania.

Katika kusisitiza hoja hiyo, licha ya wabunge kuchangia maeneo mengi yanayohusu changamoto za kilimo, Bashe anasema hakuna sehemu ambayo waziri ameeleza namna ya kuanzisha mpango wa kuthibiti bei ya mazao ya chakula.

Anasema kwa ukweli uliothibitishwa kisayansi, gharama ya kuzalisha kilo moja ya mahindi shambani katika kipindi hiki ni Sh357. halafu huyu anayetumia sh357 shambani, bado gharama ya kupeleka stoo, kuweka dawa, kuweka mifuko, akiweka stoo kuna kauli inasema walanguzi ndiyo wenye mahindi, kote duniani kuna wazalishaji, wasambazaji, jukumu lako (Serikali) ni kuwawezesha wafanye biashara,” anasema.

Bashe alisema katika kitabu cha Mpango, waziri Mpango ameeleza namna miradi itakayosimamiwa kuwa ni pamoja na kuboresha mashine za kielektroniki (EFD) na kuanzisha maabara ya TRA.

“Haumsikii akisema tutawekeza bilioni moja kwenye kilimo cha mahindi ili tuweze kupata zaidi. Huwezi kukamua maziwa ng’ombe usiyemlisha,” alisema Bashe.

Alisema, “VAT (Kodi ya Ongezeko la Thamani) na PAYE (kosi ya mapato kwenye mishahara) zimeshuka, yeye anasema ni kwa sababu kampuni zimepunguza wafanyakazi,” anasema.

Bashe alisema katika kamati ya bajeti walimshauri Waziri Mpango kutoongeza kodi katika viwanda vya bia na vinywaji baridi kwa vile ingepunguza uwezo wa uzalishaji lakini hakuwasikiliza.

“Tulishauri kwamba, unaongeza ushuru wa bidhaa kwa TBL utapunguza uzalishaji kwa hawa watu, hakusikia, tumemwambia kwamba anaua viwanda vya vinywaji baridi, Cocacola akiingiza sukari sasa hivi analipa asilimia 25 badala ya asilimia 15, aina gani ya uchumi huu?

Aliwaambia wabunge wa CCM kuwa makini kwa sababu walipewa dhamana ya kuongoza taifa na Watanzania. Anasema hatakubaliana na makosa ya Waziri Mpango yatakayoharibu nafasi ya Rais Magufuli kuchaguliwa tena kupitia uchaguzi wa mwaka 2020.

Akikosoa uwajibikaji wa wizara hiyo, Bashe anasema; “Hadi Septemba mwaka huu kwa mara ya kwanza katika historia, wizara hiyo haijaweka wazi mwenendo wa usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi.

“Kwani mnaficha nini? Aliwahi kusema ndugu Abdulrahman Kinana 9Katibu mkuu CCM) wakati akizungumza katika hafla ya la Kigoda cha Mwalimu pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, “Namnukuu (Kinana) alisema: “Jambo muhimu la Kiongozi ni kusikiliza watu wake, viongozi hamna hakimiliki ya hekima, ukweli wala kuwa sahihi kila siku.”

Peter Serukamba

Kabla ya Bashe, Peter Serukamba alisema mipango yote mitatu ya Serikali kwa miaka mitatu mfululizo ni kama imeigizwa akitumia maneno ‘copy and Paste’.

Serukamba ambaye alianza na deni la Taifa alisema katika mpango wa 2016/17, Serikali ilisema Oktoba 2015, deni la taifa lilikuwa limefikia dola bilioni 19 ikilinganishwa na dola bilioni 18 za Oktoba 2014.

Anasema katika mpango wa 2017/18, serikali ilisema deni ni dola bilioni 18. “Sasa mwaka uliopita ilikuwa 19 (bilioni) na mwaka uliofuata tunaambiwa ni bilioni 18 lakini kuna ongezeko, hawakuishia hapo, wanasema dola bilioni 18 wanalinganisha na dola bilioni 16 za mwaka 2015,” anasema Serukamba.

“Mpango wa mwanzo Oktoba ilikuwa ni dola bilioni 19 na mpango wa Pili wanasema ilikuwa ni dola 16, kwenye mpango mpya wanasema deni limefikia dola bilioni 26 ukilinganisha na dola bilioni 22 za mwaka 2016 Juni, lakini kwenye ripoti ya Juni tunaambiwa ni dola bilioni 19, kwa hiyo moja ya matatizo makubwa tuliyo nayo hapa ni takwimu zinazoletwa na wizara.”

Anasema takwimu hizo zinaandaliwa na Wizara ya Fedha na haiwezekani kujitokeza makosa ya mchanganyiko wa zaidi ya dola bilioni tatu. “Kwa hiyo ninachotaka kusema hapa ukiangalia mipango yote mitatu ni copy and paste’.”

Anasema bunge hilo linapanga kwa sababu ya kutekeleza utaratibu lakini yanayoenda kutekelezwa yanajulikana kwa wizara hiyo bila Bunge kufahamu lolote.

“Ukipitia yote wamebadilisha lugha lakini kinachosemwa ni kilekile. Deni la Taifa linapanda kwa Sh4 trilioni kwa mwaka. Maana yake tumeamua kwamba kila kitu kinafanywa na Serikali, hatuwezi kuendelea,” anasema.

“Hatuwezi kuendelea. Halipo Taifa duniani ambalo kila kitu wanajenga kwa fedha za Serikali. Tumekwenda Moscow uwanja wa ndege wa kimataifa umejengwa na mtu binafsi.”

Serukamba alisema Serikali inasema inatekeleza miradi kwa ubia na sekta binafsi (PPP), lakini katika kitabu cha waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango hakuna mradi ulioonyeshwa.

“Serikali hii haiamini katika sekta binafsi. Nataka Bunge hili tukubaliane Waziri wa Fedha atuambie, Serikali hii haikubaliani na Sekta binafsi. Kama tumerudi kwenye ujamaa tuambiane,” alisema.

“Namuonea huruma sana Rais. Anahangaika lakini wenzake hawamwambii ukweli. Humu ndani waziri anaongelea kukusanya kodi peke yake. Tunakusanya kodi kwa nani?”

“Leo mabenki yanakufa. Mabenki yote yanaonyesha kushuka kwa faida. Hata mabenki makubwa. Hata uchumi unaofanya vizuri tunaangalia ufanisi wa sekta ya mabenki na ufanisi wa soko la mitaji”

“Nchi ni yetu sote. Haiwezekani viwanja vya ndege tujenge kwa pesa zetu, reli tujenge kwa pesa zetu, umeme pesa zetu, barabara kwa pesa zetu sisi ni nani. Dunia yote imeenda kwenye sekta binafsi”

“Leo ukienda kwenye mabeki kila kitu kimeshuka. Mikopo binafsi mwaka 2015 ilikuwa asilimia 25.5 leo ni asilimia 8. Mikopo ya biashara mwaka 2015 ilifika asilimia 24.6 leo ni asilimia tisa.”

“Hakuna anayesema na tukisema utaanza kupewa majina. Mambo hayako sahihi kwa sababu moja tu, mpango wetu wa mwaka huu ndiyo wa mwaka jana na ndio wa mwaka juzi,” anasisitiza Serukamba.

Freeman Mbowe

Katika mchango wake, Kiongozi wa Kambi wa Rasmi ya Upinzani bungeni, Freeman Mbowe anasema:

“Nashukuru kwa kunipa nafasi nichangie kidogo mambo machache ambayo ni vyema tukakumbushana, katika mazingira ya kawaida ya namna ya utawala wa nchi yetu ulivyo, CCM ina dhamana kubwa kwani ndicho chama kinachozalisha Serikali.

Lakini wakati wa uchaguzi, wakati tayari ilishatoka ilani ya CCM, tulisikia kauli yenye ukakasi, badala ya kuwa Serikali ya CCM mnaona raha sana kujiita Serikali ya Magufuli na juzi Rais katika ziara alirudia kauli hiyo.

(Rais) alisema CCM kuna majizi, katika vyama za siasa kuna majizi akachanganya vyama vyote na upinzani na chama chake akasema ndiyo sababu anasema ni Serikali yake. Sasa tunakuuliza ni Serikali ya CCM, chama kinachosimamia Serikali yake au tuna Serikali ya mtu anajisimamia mwenyewe.

Napata wakati mgumu sana ninaposikia wabunge wenzetu wa CCM wanajinasibu Serikali yetu (Rais) kashajinasibu ni Serikali yake, nimesikia michango ya wabunge wote, niwashukuru sana.

Hatutaisaidia nchi hii kwa kuwa wanafiki, tutaisaidia nchi hii, tutaisaidia Serikali yetu, tutawasaidia wananchi wetu wote kwa kuwa wakweli, kuwa critical (kukosoa) kwa mambo tunayofikiri ni ya lazima, tupongeze pale panaohitajika kupongezwa tuko tayari kupongeza.

Lakini wakati tunapokosea tusipoikemea Serikali, tusipoiambia Serikali ukweli na wale wanaoikosoa Serikali wanaonekana wanastahili ya kufa, wanaoikosoa Serikali wanaonekana wanastahiki ya kuumizwa hatutafika.

Chama Cha Mapiduzi, chama chochote cha siasa kikifikia hatua ya kutokutaka ushauri, kikifikia hatua ya kuweka pamba masikioni kutokusikiliza watu wanasema nini, chama hicho hata kikiwa na nguvu gani za kijeshi lazima kitakufa, CCM kifanye wajibu wake.

Nimefuatilizia ndani ya vikao vya CCM, mtanisamehe, nimefuatilizia kuona kama mambo haya yanajadiliwa katika vikao vya chama nako hakuna, lazima tuambiane ukweli ninyi ndio mmepewa dhamana sisi ni wapinzani, yakitokea…

Tuna mfumo upi, mmesimama wapi katika msingi wa itikadi, ninachokiona mnakifanya kwa juhudi sana ni katika kulirejesha taifa hili katika ujamaa, ndugu zangu sera za ujamaa zinapendeza na ni tamu sana kuzizungumza.

Lakini ukweli wa uhalisia wa hali halisi wa binadamu, tunaambiwa tuking’ang’ania siasa za kijamaa, hatutajenga uchumi wa nchi hii kwa kutumia bunduki, hatutajenga uchumi wa nchi hii kwa kutumia ubabe na vitisho, ni lazima Serikali itambue kwamba Sekta Binafsi ] ni injini ya uchumi na Serikali ni bodi.

Ili gari liende linahitaji injini, bodi na matairi, Serikali ni bodi na matairi na injini ni sekta binafsi. Hakuna taifa lolote limeendelea duniani kwa kuipuuza sekta binafsi, hakuna taifa lolote limeendelea kwa kufikiria sekta binafsi ni wezi tu.

Kufanya biashara katika nchini hii ya awamu hii ya tano ni kiama. Wafanyabiashara wote wa ndani na nje wanalia, Waziri wa Fedha, Dk Philip Mpango tumemwambia katika kamati ya bajeti.

Tunamwona Rais anahimiza viwanda tunashangaa, tumeanza lini sera ya viwanda, hakuna kitu kipindi tunakabiliwa na tatizo kubwa kama hiki katika suala la viwanda kwa sababu tunaandika nyaraka nyingi, tuna sera nyingi tatizo letu kubwa ni utekelezaji.

Tunapanga mipango mingi tatizo kubwa ni utekelezaji, Watanzania ni wazuri sana katika kutengeneza sera, kwa miaka kumi au 15 iliyopita, tumekuwa na sera mbalimbali zinazozungumzia viwanda akizijata baadhi kuwa ni; Industrial Development Policy, vision 2025, Tanzania integrated Industrial development strategy 2025 na mipango mitatu ya miaka mitanomitano.

Ukiangalia sera zote hizi zinazungumza kitu kimoja na katika zote hakuna iliyokamilika hata moja kwa asilimia hata kumi au 15, tunazungumza kilimo kwanza tumezungumza sana na kilimo kwanza kimeishia wapi.

Watu wametumia fedha, leo Rais anahimiza viwanda ili ikifika 2025 iwe nchi ya uchumi wa kati lazima viwanda vya kuzalisha viweze kuchangia asilimia 40 ya Pato la Taifa sasa Tanzania inachangia chini ya asilimia tano.

Lakini tunajiuliza vilevile hivi viwanda vinavyohimizwa kujengwa soko liko wapi, huwezi kujenga uchumi wa viwanda kwa kutegemea soko la ndani ni lazima uzalishaji mkubwa uende soko la jirani.

Ndio sababu wenzetu wa Asia walifungua kwanza mipaka yao, ili bidhaa inayotengenezwa iweze kuuzwa Uganda au Kenya lakini sasa ukiangalia sera zetu tunafunga mipaka hatufungui mipaka.

Tunachoma vifaranga, tunauza mifugo tunategemea tutawezaje. Kuna suala la utawala bora, tunalizungumza wenzetu mnatuona kama utani hili jambo si utani hali ya usalama wa nchi yetu. Ukizungumza unashtakiwa, ukichambua uchumi unashtakiwa sisi wa upinzani tufanye nini huo na ndio wajibu wetu?

Serikali inatoa takwimu za uongo, Benki Kuu inatoa takwimu zinazotofautiana na Wizara ya Fedha na watu wa takwimu kila mtu anatoa takwimu zake ili kuilinda Serikali, ndugu zangu kama hatutajipa ujasiri wa kuikosoa Serikali pale inapobidi, tukaacha kuunda sheria ndogo ndogo za kutudhibiti humu ndani na nje, msiba utatuumbua.

Hali yetu ya maisha ni ngumu na uchumi si ‘flyover’ (barabara za juu) au ndege sita, uchumi ni kipato cha wananchi wa kawaida waweze kuboresha maisha yao kutoka pale walipo kwenda bora zaidi.

Watanzania wanazidi kuwa maskini na kundi dogo la watu pengine ndio wanaweza kuona faida ya kukua kwa uchumi, kukua kwa uchumi tunaoambiwa hakuendani na hali ya maisha ilivyo na tukisema tunaonekana ni wachokozi.

Ukweli yako mambo mengi yanaendelea katika nchi hii msipomwambia Rais hammsaidii, yako mambo ya ukanda, lakini tunapaswa kujiuliza chanzo cha maneno hayo ni nini kwa nini hayakuzungumza huko nyumba, hayakuzungumzwa miaka mitatu iliyopita.

Tuache kuwa na ‘double standard’ sisi ni chama cha siasa kina wanachama nchi nzima, tusingependa kufika kuanza kunyoosheana kidole huyu ni kabila fulani, dini fulani, au rangi gani.

Lakini yako mambo yanafanyika yanasababisha hayo ila yasipozungumzwa misiba itakuja kutuumbua, hivyo mmwambie bwana mkubwa kwamba unapofanya mambo mengine tenda haki pande zote tutampongeza, tutamsifu lakini kama haki moja unaipeleka sehemu moja kwingine unawanyima, hapana.

Uchaguzi unazalisha viongozi kutoka maeneo mbalimbali na watu wote wana haki ya kuchagua na kihistoria viongozi waliotangulia walihakikisha nafasi katika mashirika ya umma zinagawiwa kiusawa ila mkitaka kuleta vithibitisho nitaleta kwamba kuna kanda haitendewi haki.