Wafanyabiashara wanavyolilia ndege za mizigo Mkoani Mbeya

Muktasari:

  • Hata hivyo, huenda wakasubiri zaidi kupata huduma hiyo kutokana na kutokuwapo kampuni iliyojitokeza kutoa huduma ya ndege za mizigo kupitia uwanja huo unaotegemewa zaidi na mikoa ya nyanda za juu kusini.
  • Hadi sasa, kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya Meneja wa SIA, uwanja huo unahudumia wastani wa tani 55,000 kwa mwezi takriban mara 10 ya kiwango cha uwanja wa zamani uliokuwapo katikati ya jiji.

Baada ya kuonja huduma za ndege za abiria kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Songwe (SIA), wafanyabiashara mkoani Mbeya sasa wanataka kutumia fursa zaidi ya kusafirisha mizigo yao kwa usafiri wa anga ndani na nje ya nchi.

Hata hivyo, huenda wakasubiri zaidi kupata huduma hiyo kutokana na kutokuwapo kampuni iliyojitokeza kutoa huduma ya ndege za mizigo kupitia uwanja huo unaotegemewa zaidi na mikoa ya nyanda za juu kusini.

Hadi sasa, kwa mujibu wa takwimu kutoka ofisi ya Meneja wa SIA, uwanja huo unahudumia wastani wa tani 55,000 kwa mwezi takriban mara 10 ya kiwango cha uwanja wa zamani uliokuwapo katikati ya jiji.

Mamlaka zinaeleza kuwa sehemu kubwa ya mizigo inayobebwa ni midogomidogo ambayo mara nyingi huambatana na abiria wanaosafiri kwa kutumia ndege za abiria.

Hata wakati kukiwa na ndege za abiria pekee ambazo bado hazikidhi mahitaji, Mbeya ni miongoni mwa mikoa mitano inayoongoza kwa kuwa na viwanda vingi nchini ambavyo baadhi ya bidhaa zinazozalishwa husafirishwa kwenda mikoa mingine na hata nchi jirani za Zambia, Malawi na Jamhuri ya Demokrasia ya Congo (DRC).

Takwimu za Ofisi ya Takwimu ya Taifa (NBS) za mwaka 2015 zinabainisha kuwa Mbeya ni mkoa wa tano kwa viwanda nchini ikiwa na viwanda 2,982 na kati ya hivyo vikubwa ni 57 ambavyo vinatoa fursa lukuki kwa kiwanja hicho.

Wafanyabiashara wa mkoa huo wanasema uwepo wa uwanja huo ni chachu ya kutafuta masoko ya bidhaa zao ndani na nje ya nchi iwapo utakuwa na huduma zote muhimu.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rapha Group, inayomiliki kiwanda cha kusindika mazao ya nafaka Jijini Mbeya, Raphael Ndelwa anasema pamoja na Sia kufungua masoko ya ndani na nje bado kutokuwepo kwa ndege za mizigo ni “kikwazo” kwa kuwa ndoto zao haziwezi kutimizwa kwa sasa.

Ndelwa anasema kwa mwezi husafirisha nafaka za aina mbalimbali kwenda nje ya mkoa ukiwemo mchele kati ya tani 500 hadi 1,000, maharage tani 30 hadi 25, na wakati mwingine oda huwa inaongezeka zaidi.

“Nikisafirisha tani 30 za mchele kupeleka Dar es Salaam, natumia kiasi cha Sh3 milioni ambayo ni gharama ya kusafirishia mzigo tu, hapo bado gharama za kupakia na kushusha mzigo.

“Inakuwa ngumu mzigo mmoja kulipiwa gharama za kupakia na kushusha mara nne kama unataka kupeleka nje ya nchi. Ingekuwepo ndege ni rahisi na gharama nafuu”, anasema Ndelwa.

Mbali na wawekezaji wa viwanda na wakulima, kuna baadhi ya wafanyabiashara ambao huingiza bidhaa zao kutoka nje ya nchi ambao walitegemea kufunguliwa kwa uwanja huo kungepunguza zaidi gharama za uendeshaji.

Mfanyabiashara wa nguo za watoto na wakubwa jijini hapa, Nasra Haonga, anasema bidhaa zake huchukulia China na kuleta Mbeya hivyo hutumia gharama kubwa na muda mwingi kufikisha mzigo wake jijini hapa kwani hakuna ndege ya moja kwa moja kutoka China hadi Mbeya.

Anasema kila mwezi hufanya safari zake kwenda China kununua mzigo na hubeba mzigo wa kilo 320 ambao hulazimika kuusafirisha hadi Jijini Dar es Salaam kwa ndege kisha hutafuta usafiri wa basi kuupeleka Mbeya.

“Kama zingekuwepo ndege za moja kwa moja kutoka China hadi Mbeya hususan za mizigo zingenirahisisha biashara yangu kwa kutumia muda wa siku moja na hata gharama zingepungua,” anasema.

Anasema kwa sasa hulipia Dola za Marekani saba zaidi ya Sh15, 000 kwa kilo moja ya mzigo wake kwenye ndege na akifika Dar es Salaam hushusha na kupakia tena kwenye basi jambo linaloongeza gharama nyingine.

Waipigia magoti Serikali

Wafanyabiashara hao, wanaiomba Serikali iwasaidie kuwatafutia wawekezaji wa mashirika ya ndege za kutoka nje ya nchi ambazo zitakuwa zinafanya safari zake angalau mara moja kwa mwezi kwani wanaamini hiyo itatoa mwanga kwa wao kwenda nchi husika kutafuta masoko yanayoendana na bidha zao.

Pamoja na kwamba wafanyabiashara hao wanahitaji ndege za mizigo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo, (TCCIA), Mkoa wa Mbeya, Emile Malinza ana wasiwasi kuwa wawakezaji wa usafiri wa anga huenda wanakwamishwa na kutokamilika kwa miundombinu muhimu.

“Kwa mfano, hata jengo la abiria lile kubwa bado halijakamilika, pia hakuna maghala au majengo ambayo wafanyabiashara watayatumia kwa ajili ya kuhifadhia mizigo yao kabla ya kusafirishwa kwa ndege,”

“Hakuna kituo cha mafuta, lakini pia hata sasa watu wanashindwa kwa ndege hizi zinazotua kutokana na masharti ya usafiri kuwa sio rafiki kwa abiria,” anasema Malinza bila kufafanua zaidi masharti hayo.

Malinza anasema TCCIA Mkoa wa Mbeya inawahamasisha wananchi kuendelea kuunga mkono jitihada za Serikali kuwekeza kwenye miundombinu ndani ya uwanja huo ili ukamilike na fursa zilizopo ziweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Hata hivyo, wataalamu wa masuala ya uchumi na biashara wanaona wafanyabiashara ndiyo hawajatumia vyema fursa za uwanja huo.

Mtaalamu wa uchumi, Dk Stephen Mwakajumilo anasema licha ya uwanja huo kutokamilika kwa asilimia 100, lakini bado wananchi wa Mbeya na ukanda mzima wa Nyanda za Juu Kusini hajawaonyesha kuchangamkia fursa za kiuchumi zilizopo kwa kuweka vitega uchumi vya kwao kando kando mwa uwanja.

Dk Mwakajumilo anasema fursa ya uchumi kupitia uwanja huo kwa wakazi wa Mbeya ipo kubwa kwani sio kila kitu kitakamilishwa na Serikali kwa kuwa kuna miundombinu mingine inatakiwa kuwekezwa na wawekezaji kama kitega uchumi binafsi.

“Pale watu wanahitaji kuwekeza kwenye ujenzi wa maghala ya kuhifadhia mizigo wakati ikisubiri kusafirishwa na ndege, watu wajenge hoteli za maana, lakini hili naona mwamko haujawa mzuri kwa wakazi wa Mbeya,” anasema Dk Mwakajumilo.

Kampuni za ndege nazo zinaona fursa hiyo. Japo hazina ndege za mizigo kwa sasa, bado wanaona wanaweza kutumia zilizopo kusafirisha sehemu ya shehena iliyopo.

ATCL walonga

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Ndege la Tanzania, (ATCL), Ladislaus Matindi anasema shirika hilo lipo kwenye mchakato kuleta ndege za mizigo ili kuongeza ufanisi wa kibiashara.

“Labda kutojua tu lakini kama ni suala la kubeba mizigo, si dhani kama Mbeya kwa sasa kuna mizigo mingine na mikubwa kiasi hicho, kwani ndege yetu inayofanya safari zake Mbeya-Dar- es- Salaam ina uwezo wa kubeba abiria na mizigo hadi tani saba.

Lakini matarajio yetu baadae ni kuleta ndege za mizigo tu ambazo kufikia June mwakani zitakuwa zimetua nchini, na zikifika ndio tutajua zitakuwa zikifanya safari zake wapi na wapi ikiwa ni safari za ndani na nje ya nchi,” alisema Matindi.

Serikali nayo inajua uwepo wa mahitaji ya ndege za mizigo katika uwanja huo mpya.

Serikali yavutia wakezaji ndege za mizigo

Meneja wa uwanja huo, Amiry Hassan anasema wanaamini endapo ndege za mizigo zikianza kufanya safari zake katika huo idadi ya mizigo itaongezeka zaidi na wafanyabiashara wengi watahamasika kuutumia katika kusafirisha bidhaa zao.

Anasema kinachofanyika hivi sasa ni kuendelea kuwashawishi wenye mashirika ya ndege ya ndani na nje ya nchi yaweze kuelekeza ndege zao za mizigo kwenye uwanja huo ili kuongeza fursa za kibiashara.