Maktaba hii isiwe pambo, itumiwe ipasavyo

Sunday February 11 2018

 

Ujenzi wa maktaba ya kisasa na kubwa kuliko zote barani Afrika unaoendelea katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kwa gharama ya Sh90 bilioni utakuwa umekamilika na wajenzi kuukabidhi rasmi ifikapo Julai.

Juzi, Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako na Balozi wa China nchini, Wang Ke walikwenda katika chuo hicho kujionea maendeleo ya mradi huo na kuelezwa kuwa umekamilika kwa asilimia 90.

Maktaba hiyo inayojengwa kwa msaada wa Serikali ya China, ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 2,100 kwa wakati mmoja na kuhifadhi vitabu 800,000.

Akizungumza katika ziara hiyo, Waziri Ndalichako alisema ujenzi huo umezingatia wanafunzi wenye mahitaji maalumu (walemavu) pamoja na tatizo la kukatika kwa umeme kwani limewekewa mfumo wa sola kwa ajili ya taa na viyoyozi.

Balozi Ke alisema kwamba anafurahi kuona maendeleo mazuri ya ujenzi wa jengo hilo ikiwa ni miezi 20 tangu Rais John Magufuli aweke jiwe la msingi akisema hiyo ni kutokana na ushirikiano mzuri uliopo baina ya wataalamu wa Tanzania na China.

Hatua ya ujenzi wa maktaba hiyo ya kihistoria imetokana na ukweli kwamba idadi ya wanafunzi katika chuo hicho imekuwa ikiongezeka mwaka hadi mwaka.

Mathalan, kwa mujibu wa tovuti ya chuo hicho, www.udsm.ac.tz idadi ya wanafunzi imeongezeka kutoka 14 mnamo mwaka 1961 hadi kufikia 21,502 (wanaume wakiwa 13,641 na wanawake 7,861) wa shahada ya kwanza na wasio wa shahada katika mwaka wa masomo wa 2011/2012.

Bila shaka idadi hiyo ambayo haihusishi wanafunzi wa masomo ya shahada za juu za uzamili na uzamivu, imeongezeka na wote hao, wanahitaji kupata vitabu kwa ajili ya rejea mbalimbali kukidhi mahitaji ya masomo yao.

Tunaipongeza Serikali na uongozi wa UDSM kwa kufikiria kuwa na aina hii ya maktaba tukiamini kwamba rejea itaongeza uwezo wa wanafunzi kupata maarifa bora zaidi kwa manufaa ya Taifa na ulimwengu kwa ujumla.

Tunaamini kwamba wanufaika wa maktaba hiyo hawatakuwa wanafunzi wa UDSM pekee, bali jengo hilo ambalo linakusanya na kutunza nyaraka mbalimbali kama majarida, vitabu na magazeti, litakuwa kimbilio la watu wengi wakiwamo wasomi wanaofanya tafiti na hata wanafunzi wa vyuo vingine.

Tanzania kama zilivyo nchi nyingi za Afrika, imekuwa ikikabiliwa na tatizo kubwa la maktaba. Sehemu ambayo watu wanaotaka kupata taarifa na ujuzi wa masuala mbalimbali huenda kujisomea. Ni imani yetu kwamba sote na zaidi wanafunzi wa UDSM wataitumia vyema fursa hii ya kuongeza ujuzi.

Hatutegemei kwamba kuna vitabu vitakavyotunza katika maktaba hiyo ambavyo vitakaa kwa miaka kadhaa kama mapambo bila kupekuliwa, ikiwa hivyo malengo ya kujengwa kwake hayatakuwa yamekidhiwa kama ilivyokusudiwa.

Wakati tukiwashajiisha wanafunzi wa UDSM kuitumia kikamilifu maktaba hiyo kujiongezea maarifa, tunatoa wito kwa jamii kuanza utamaduni wa kujisomea masuala chanya ambayo yanaweza kubadili aina na mifumo duni ya maisha inayowazunguka na kuwa bora zaidi.

Suala la kujisomea lisiachwe kwa wanafunzi na kada fulani ya watu pekee, la hasha. Kila mtu kwa ujuzi na weledi wake, anayo fursa ya kujiongezea maarifa na hiyo ndiyo tofauti yetu na viumbe wengine walioumbwa na Mwenyezi Mungu katika ulimwengu huu.