UCHAMBUZI: Malezi ya mzazi huandika hatima ya mtoto wake

Tuesday September 4 2018

 

Mzazi ana nafasi ya pekee katika kumwandalia mtoto hatima ya maisha. Ni mtu anayemtunza, kumhudumia na kumfundisha mtoto mpaka akue. Anaweza kumwambukiza tabia njema au mbaya.

Ni kutokana na nafasi ya muda mwingi wa kuishi na mtoto tangu anapozaliwa, hivyo anakuwa na sifa za kuwa mwandishi wa hatima ya mtoto husika.

Kiuhalisia hakuna mzazi anayetamani mwanaye awe na tabia mbaya. Kila mzazi ana shauku ya tabia nzuri kwa mwanaye. Anatamani mtoto wake ajinasibu kwa kutenda matendo mema ambayo yatarudisha sifa kwake.

Malezi ya wazazi ndiyo msingi wa kutabiri maisha ya siku za mbele ya mtoto kitabia. Kimazingira, haipingiki kwamba mzazi ndiye darasa msingi la malezi ya watoto. Wazazi wana jukumu kubwa la kuhakikisha hawakosei hata hatua moja katika malezi.

Hakuna mzazi ambaye angependa hatima ya mwanaye iwe ya misukosuko lakini ni vyema kuangalia malezi wanayowapa watoto.

Ikumbukwe kuwa mtoto anajifunza na kuiga yale yanayomzunguka tangu akiwa mchanga. Kama mzazi atakosea kumfunda mtoto, ni dhahiri hata ujana wake utakuwa ovyo.

Pengine lawama nyingi kwa kipindi hiki zinazowaandama watoto na vijana ni matokeo ya malezi kutoka kwa wazazi. Vijana wengi wamekosa mwelekeo wa kimaadili, heshima na kitabia. Wamegubikwa na tabia ambazo hazina ladha katika jamii. Haya yanawezekana kuwa ni matokeo ya familia wanazotoka.

Mathalani, kama wazazi ndani ya familia hawaheshimiani, hawatoi picha ya thamani ya kuheshimiwa, vivyo hivyo watoto nao watakuwa na ujasiri wa kutoheshimu wakubwa. Tusitegemee miujiza ya kuwafanya.

Kwa nyakati hizi, siyo kitu cha kushangaa kuwakuta watoto wanajibizana na wazazi tena kwa kukaripiana na wakati mwingine wazazi kwa kuona aibu wananyog’onyea na kuwa wapole ili kumaliza mambo, kitu ambacho kwa mantiki ya kawaida kinawapa watoto nguvu na kiburi cha ushindi.

Si kitendo kibaya mtoto kujibizana na mzazi kwa kuwa kinampa mtoto mawanda mapana ya kuhoji kile ambacho hajaridhia kukitenda.

Tatizo ni pale linapokuja suala ambalo linahitaji nafasi ya mzazi ijidhihirishe kwa mtoto, lakini kwa kuwa mtoto amepewa uhuru uliopitiliza na mazoea yasiyokidhi viwango, anajiinua na kutaka kuififisha nafasi ya mzazi.

Mathalani, mtoto anapofanya makosa ni wajibu wa mzazi kumwelekeza, kumkanya hata ikibidi kumpa adhabu. Viboko ni njia sahihi ya kumrudisha mtoto katika nafasi nzuri kinidhamu. Hata kwenye vitabu vitakatifu vimeelekeza kuwa usimnyime mwanao fimbo.

Wapo watoto ambao kwenye familia hata kama wakikosa hawashikiki kwa kuwa wameona mazingira ya wazazi yanawaruhusu kukataa adhabu. Haya ni matokeo ya malezi katika familia.

Athari kama hizi ndizo zinazowasukuma baadhi ya wanafunzi kuwadharau walimu shuleni, hata pale wanapofanya makosa kukataa kuadhibiwa.

Wazee wetu wanatuambia zama zao ukifanya kosa shuleni ungetandikwa viboko na mwalimu, ukirudi nyumbani mzazi naye anakuongezea adhabu.

Hali hii ilitokana na malezi ambayo wazee walikuwa wanawapa watoto wao. Yalikuwa malezi ya kutambua nini maana ya mzazi lakini pia malezi yalimfanya mtoto atambue ni nani anayeweza kumwadhibu pale anapokosea.

Tofauti na zama za sasa ambazo mazingira hayampi mzazi wa mwingine kumuonya mtoto wa mwenzake, wala hayampi mwalimu mamlaka ya kujisikia amani pale anapomwonya mwanafunzi.

Si muumini wa kushadadia viboko, lakini ninachomaanisha ni mzazi au mwalimu kuwa na uhuru wa kumkanya mwanafunzi pale anapofanya makosa.

Kwa kiasi kikubwa maadili na malezi kwa watoto na vijana yameporomoka, tunapoyafumbia macho yanazidi kuota mizizi na kuzidi kuandika hatima mbaya kwa watoto.

Kwa mfano, kijana anaweza kukutana na mzee njiani na kijana asimsalimie. Hili linajaribu kuleta tafsiri kuwa hayo ndiyo malezi na maisha ambayo kijana anaishi na wazazi wake.

Kwa upande mwingine tunaweza kuwalaumu watoto na vijana ilhali tukisahau kuwa wazazi ndiyo waandishi wa hatima za watoto wao.

Hii ina maana kwamba, namna wanavyowalea, wanavyowaonya na wanavyoishi nao ndivyo wanavyowatengenezea mfumo wa maisha.

Wahenga walisema, “mtoto umleavyo ndivyo akuavyo.” Hivyo wazazi wanakumbushwa kuwa tabia nzuri ni matokeo ya msingi wa malezi ndani ya familia.

0753590823