MAONI: Mamlaka za maji zibuni miradi mpya

Friday January 18 2019

Hatimaye wakazi wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga wameanza kupumua. Shida iliyokuwa ikiwaelemea ya uhaba wa maji sasa inaelekea kutoweka.

Hatua hiyo inatokana na juhudi zilizofanywa na viongozi kuongeza uzalishaji sambamba na usambazaji wa maji, hivyo kupunguza kero iliyokuwapo kwa muda mrefu.

Taarifa tulizo nazo ni kwamba hadi mwaka 2015, wakazi wa wilaya hiyo waliokuwa wakipata maji safi walikuwa kati ya asilimia 25 hadi 30, lakini sasa wameongezeka hadi kufikia asilimia kati ya 55 na 60.

Hii ni taarifa yenye matumaini na kwa hakika kilichofanyika Handeni ni kitendo cha kupongezwa kwa kuwa kero ya maji katika wilaya hiyo ni ya siku nyingi na wananchi wametaabika kwa kiasi cha kutosha.

Hata hivyo, shida ya maji haipo Handeni pekee. Hiki ni kilio kilichoenea karibu kila kona ya nchi, licha ya kuwapo kwa mamlaka nyingi za maji, ambazo kimsingi tunaweza kusema zimekuwa mamlaka kwa jina lakini zina walakini mkubwa wa kufikisha maji ipasavyo kwa wananchi.

Mamlaka na taasisi za usimamizi wa maji nchini haziwajibiki ipasavyo katika kubuni vyanzo vya maji, kusimamia usambazaji na hata mgawanyo wa maji.

Hata katika mazingira yenye maji ya kutosha, mamlaka nyingi zina udhaifu wa kudhibiti uharibifu wa vyanzo vya maji, hivyo kuchangia kupungua au kuisha kwa maji.

Jamii isipokuwa na maji, mambo mengi yanaweza kuibuka ikiwamo uvunjifu wa amani kama tunavyoshuhudia katika maeneo mbalimbali nchini, ambayo wananchi wamejikuta katika migogoro isiyoisha itokanayo na uhaba wa maji katika shughuli zao za uzalishaji.

Tukiacha migogoro ambayo mwishowe imekuwa ikizaa hata mapigano kama tunavyoshuhudia mara kwa mara, uhaba wa maji Handeni na maeneo mengi nchini, umekuwa ukihatarisha ustawi wa jamii hasa kwa kusababisha migogoro baina ya wanandoa. Uzoefu unaonyesha kuwapo kwa ndoa zinazoyumba au hata kuvunjika kwa sababu ya maji.

Mbali ya kukuza uwajibikaji, tunaamini kero ya shida ya maji katika maeneo mengi nchini inaweza kufika kikomo ikiwa mamlaka za maji zitaufanyia kazi ushauri wa Waziri wa Maji na Umwagiliaji, Profesa Makame Mbarawa ambaye amewahi kunukuliwa akizitaka mamlaka hizo kujiendesha kibiashara, hatua inayoweza kuzipa uwezo mkubwa wa kujenga miundombinu mikubwa ya kisasa.

Kuendelea kusubiri misaada ya miradi itokanayo na msukumo wa Serikali au wahisani na kuwekwa kando kwa uwajibikaji wa kibunifu, ni baadhi ya mifano inayonyesha udhaifu wa mamlaka za maji na hivyo wananchi katika maeneo mengi kuendelea kutaabika kwa kukosa huduma hiyo muhimu kwa shughuli za kimaisha na uzalishaji.

Tanzania ya viwanda na ya uchumi wa kati ambao Serikali ya Awamu ya Tano inaipigia debe, pamoja na mambo mengine muhimu inahitaji uhakika wa maji kwa wananchi katika maeneo yote.

Ikiwa Handeni sasa angalau wananchi wameutua ule mzigo wa miaka nenda rudi wa kukosa maji, hali hii iwe chachu kwa maeneo mengine yote nchini ambayo wananchi bado wanaendelea kulilia maji.