MAONI: Maonyesho ya Sabasaba yatumike kuongeza ubora wa bidhaa, huduma

Msimu wa maonyesho ya biashara ya kimataifa maarufu kama Sabasaba umewadia na tayari ufunguzi rasmi ulifanyika Juni 28, mwaka huu huku wananchi na wadau mbalimbali wakimiminika kwenye viwanja vya Sabasaba yanakofanyika maonyesho hayo.

Licha ya kuwa na historia ndefu, Sabasaba kwa sasa inatambulika kama maonyesho ya biashara ya kimataifa ya Dar es Salaam ambayo hutoa fursa kwa wadau wa viwanda, kilimo na shughuli mbalimbali za kijamii kukutana kwa lengo la kutanua masoko, kukutanisha wadau na kujifunza mambo mapya zikiwamo teknolojia mpya.

Maonyesho ya Sabasaba sasa yamekuwa ya kimataifa kutokana na kuwa na sifa ya kimataifa kwa kushirikisha mataifa mbalimbali ya ndani na nje ya Afrika.

Kuimarika na kuboreka maonyesho hayo kunaonyesha ni kwa jinsi gani yalivyo na umuhimu na jinsi waanzilishi wake walivyokuwa na mawazo ya kuona mbali hasa kwa lengo la kuimarisha kilimo, kutengeneza fursa za masoko na kupata uzoefu kutoka kwa wengine.

Hata hivyo, ni vyema tukakumbushana matumizi sahihi ya maonyesho hayo hasa kwa washiriki na hata wananchi wanaofika kwa ajili ya kuona na kujipatia bidhaa, huduma mbalimbali ambazo huuzwa au kutolewa viwanjani hapo kila yanapowadia.

Ni muhimu kwa wadau hasa wa ndani wanaokwenda kuonyesha bidhaa na huduma zao kuhakikisha wanafanya hivyo kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu maendeleo ya teknolojia na kuwatengenezea mazingira rahisi kuzifikia teknolojia hizo ili ziwe msaada katika shughuli zao za kilimo au ujasiriamali.

Ni vivyo hivyo kwa taasisi zinazoshiriki maonyesho hayo za ndani ya nchi kuyatumia kujifunza kwa taasisi za nje za kimataifa na kutengeneza mtandao wa kupata ama wateja au washirika watakaoshirikiana nao katika shughuli zao hata baada ya maonyesho kumalizika.

Tunayashauri haya baada ya kuonekana sasa Sabasaba inatazamwa kama msimu wa kuuza na kununua bidhaa kwa bei ya punguzo na hivyo kila mmoja hujiandaa kwa mtazamo huo jambo ambalo si sahihi.

Sabasaba isichukuliwe kama eneo la kuuza na kununua bidhaa au kutoa na kupokea huduma, bali iendelee kuwa darasa kwa ajili ya kupata mbinu mpya za kilimo ili kuongeza uzalishaji na masoko ya uhakika.

Hatupingi au kukosoa uuzaji na ununuzi wa bidhaa au kutoa na kupokea huduma mbalimbali, lakini ni muhimu kutoisahau misingi na malengo ya kuanzishwa kwake.

Uwepo wa kampuni na taasisi mbalimbali kubwa za kimataifa zinazotambulika na zilizofanikiwa unapaswa kuwa neema na turufu muhimu itakayosaidia kuinua kilimo, ujasiriamali na mambo mengine muhimu kwa kilimo na biashara nchini.

Tusiishie kwenda Sabasaba kuona wanyama, kutazama maingizo mapya na ya kisasa ya simu na bidhaa zingine bali Sabasaba iwe kama darasa, mkulima aliyefanikiwa kuingia humo atoke akiwa na tofauti japo kwa kupata mteja mpya au mtaalamu atakayekuja kumuongezea ubora wa kilimo chake.

Kutanuka kwa maonyesho ya Sabasaba ambapo sasa hayajifungi na shughuli za kilimo pekee bali yanakutanisha sekta zote za maendeleo ya jamii ni jambo bora ambalo ni muhimu likatumika kikamilifu kuongeza kasi ya maendeleo ya Taifa.

umbukwe kuwa Serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Magufuli imejipambanua kwa kutaka kujenga Tanzania ya viwanda na kufikia kuwa nchi yenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025, hivyo majukwaa mbalimbali likiwamo hili la maonyesho ya sabasaba linaweza kuwa sehemu muhimu itakayosaidia kufikia huko.