Maradhi hatari kwa madereva barabarani

Friday January 11 2019

 

By Aurea Simtowe, Mwananchi [email protected]

Tunafahamu kuwa dereva mzuri ni lazima apitie chuo ili ajue sheria na alama za barabarani zikitazomuwezesha kuendesha chombo chake cha moto vizuri.

Hata hivyo, vipo baadhi ya vipimo vinavyofanywa kwa madereva ili kuhakikisha kama wako salama kiafya ikiwa ni njia mojawapo ya kujikinga na ajali zinazoweza kutokea.

Kuna wakati ajali hutokea licha ya dereva kuwa na sifa zote za ujuzi wa kuendesha gari ambazo husababishwa na maradhi.

Miongoni mwa maradhi hayo ni matatizo ya macho, ugonjwa wa moyo na tatizo la kupumua.

Ugonjwa wa moyo

Mkurugenzi wa Upasuaji kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), Dk Bashiri Nyangasa anasema mtu aliye na matatizo ya aina yoyote ya moyo anatakiwa kuendesha chombo cha moto kwa tahadhari kwa sababu endapo akipata shambulizi la ghafla anaweza kusababisha ajali.

“Ugonjwa wa moyo siyo sawa na magonjwa mengine kama malaria na kuhara, mtu ambaye mishipa ya moyo haipeleki vizuri hewa ya oksijeni kwenye kichwa, anaweza kupoteza fahamu papo hapo endapo atapata shambulizi.

“Sasa kama alikuwa anaendesha kwa kasi kubwa, upo uwezekano wa kusababisha ajali ambayo ni ngumu kuzuilika,” anasema Dk Nyangasa.

Kutokana na kuwapo kwa maradhi hayo, anasema wamekuwa wakiwashauri wagonjwa hasa waliofanyiwa upasuaji kutoendesha gari kwa kipindi cha miezi sita na wasikate kiti cha mbele wanapokuwa katika magari binafsi.

“Ukikaa kiti cha mbele ni lazima ufunge mkanda, sasa hiyo ina maana sehemu ambayo tumeifanyia upasuaji uifunge, ikitokea bahati mbaya mmepata mshtuko mkanda utabana sehemu tuliyoishona na kusababisha matatizo,” anasema Dk Nyangasa.

Matatizo katika mfumo wa upumuaji

Dk Peter Mathew kutoka Hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, anasema mtu mwenye matatizo ya upumuaji anashauriwa kutembea na kifaa maalumu kitakachomsaidia kupumua endapo tu atapata shambulio.

Anasema kutokana wagonjwa hao mara nyingi kuathiriwa na vumbi, moshi na hali ya hewa ni rahisi kwao kupata shambulizi.

“Anapopata shambulizi na kutumia dawa hatakiwi kuanza kuendesha papo hapo kwa sababu viungo vyake vya mwili hujirudisha katika hali ya kawaida na kupumzika, hivyo kuna wakati huweza kupitiwa na usingizi.

“Sasa akipata usingizi na gari inakwenda, yuko peke yake, uwezekano wa yeye kuchangia ajali barabarani ni mkubwa,” anasema Dk Mathew.

Matatizo ya macho

Zipo aina mbili za matatizo ya macho zinazowatesa watu wengi ambayo ni uoni wa mbali na uoni wa karibu.

Dk Mathew anasema mtu anapokuwa na uoni wa mbali hawezi kuona vitu vilivyokuwa karibu yake na yule aliye na uoni wa karibu hawezi kuona vitu vilivyo mbali.

Anasema kulingana na matatizo hayo kwa mtu husika, uendeshaji wake wa chombo cha moto unaweza kuathirika kwa namna mbalimbali ikiwamo kutoona baadhi ya alama.

“Kuna wengine watakuambia wanaona ukungu mbele kuna wengine akiangalia sana mishipa inamuuma; haya yote ni matatizo ya macho yanayotakiwa kufanyiwa matibabu ili dereva aweze kuwa salama,” anasema Dk Mathew.

Anashauri kuwa mtu aliye na matatizo ya macho anatakiwa kutembelea vituo vya afya ili kupata matibabu ikiwamo miwani inayoweza kuwaongezea uwezo wa kuona mchana na usiku.

Mambo mengine hatari kwa dereva

Mbali na maradhi ya kiafya katika mwili, pia kuna mambo mengine yanayosababisha ajali za barabarani ikiwamo uraibu (unywaji wa pombe) na msongo wa mawazo.

Ili kuhakikisha hali hiyo inadhibitiwa kwa madereva wawapo barabarani, Serikali imekuwa ikiwapima madereva kujua kama wamekunywa pombe na kiwango cha pombe kwenye damu hakijazidi.

“Kwa hapa Tanzania, Sheria inataka iwapo mtu ametumia pombe, basi akutwe na kiwango cha pombe katika damu (BAC) cha 0.05g/dl au 0.08g/dl zaidi ya hapo anakamatwa,” anasema Mwanasheria wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni.

Hivi karibuni, Daktari mwandamizi wa Dharura na Maafa kutoka Wizara ya Afya, Mary Kitambi, alikaririwa na gazeti hili akisema: “Unajua mtu anapokunywa pombe umakini hupungua, lakini hata kiwango cha pombe kwenye damu kilichowekwa katika sheria kinatofautiana kwa mtu na mtu. Mwingine kiwango kwenye damu cha 0.05g/dl kitamlewesha kutokana na umbo na uzito wa mwili.”

Akizungumzia hilo, Dk Mathew anasema kama dereva ni mnywaji wa pombe, kuna kiwango anashauriwa kutumia na hiyo iko tofauti kwa watu wanene na wembamba. Anasema mtu mnene anashauriwa kunywa chupa mbili pekee ili asilete madhara na kuendesha taratibu kwa sababu pombe inatabia ya kulegeza viungo vya mwili wa mtu jambo linaloweza kuleta matatizo barabarani hasa ajali.

“Kuna ule msemo kuwa dereva hata alewe vipi, akikaa kwenye steering (usukani) yuko sawa; lakini si kweli, anaweza kusababisha ajali yenye kuleta majeraha ya kudumu na kugharimu maisha ya watu.

“Kwa wale wanaotumia pombe ni vyema wakaepuka kunywa na kuendesha ili kupunguza madhara ya pombe,” anasema Dk Mathew.

Mtaalamu wa Saikolojia, Daniel Marandu anasema kutokana na uendeshaji wa gari kutumia zaidi akili na hisia, hivyo inakuwa ni ngumu kwa watu wenye msongo wa mawazo kuwa makini barabarani.

Anasema dereva anapopata msongo wa mawazo, uwezo wake wa kufikiri unakuwa haupo katika kiwango kinachotakiwa na kupunguza umakini hasa pale akili inapopaswa kutumika zaidi.

“Hapa ndiyo unakuta mtu yuko hapa kimwili ila kiakili yuko mbali kutokana na mawazo aliyonayo inakuwa ni ngumu kuchukua uamuzi wa haraka. Kuna ajali nyingine zikitokea mashuhuda wanakuambia sijui dereva alikuwa anawaza nini.”

Pia, anasema kuna wakati dereva hupita sehemu ya kuvukia watu wakati taa nyekundu zimewaka na akiulizwa kwa nini alivuka, hujibu alikuwa mbali, hivyo huo ni msongo wa mawazo.

“Mambo hayo huweza kumfanya mtu kusababisha ajali inayoweza kugharimu maisha yake au kuleta majeraha,” anasema.

Marandu anasema mtu anapokuwa na msongo wa mawazo uliokithiri ni vyema kuepuka kuendesha vyombo vya moto na kupata ushauri wa wataalamu wa saikolojia pale anapoona ameshindwa kumudu hali hiyo.