UCHAMBUZI: Mawakala sasa wawatupie jicho wachezaji K’njaro Queens

Michuano ya soka ya wanawake inayoandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), inamalizika leo kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam baada ya kuchezwa kwa wiki mbili.

Tanzania ambayo ilikuwa mwenyeji wa michuano hiyo ilikuwa na timu mbili za Tanzania Bara, ‘Kilimanjaro Queens’ na Zanzibar.

Timu za Kundi A ziliundwa na Kilimanjaro Queens, Zanzibar, Sudan Kusini na Burundi. Kund B Uganda, Kenya, Djibouti na Ethiopia.

Mashabiki waliojitokeza kwenye uwanja huo kushuhudia michuano hiyo walipata burudani kutoka kwa timu hizo ikiwemo Ethiopia ambayo ilikuwa kivutio.

Licha ya kutopata matokeo mazuri katika idadi kubwa ya mechi zake, wachezaji wa Ethiopia walionyesha vipaji ambavyo vilikuwa kivutio kwa mashabiki waliokwenda uwanjani.

Pia Kilimanjaro Queens ambayo kwa muda mrefu imekuwa kinara kwa ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika soka la wanawake ilionyesha ukomavu wake.

Haikushangaza Kilimanjaro Queens na Kenya kufuzu hatua ya fainali ya michuano hiyo kutokana na ubora wao. Mchezo wa fainali umepangwa kuchezwa leo kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.

Timu hizo zinatarajiwa kutoa burudani kwa mashabiki baada ya kucheza kwa kiwango bora tangu kuanza michuano hiyo. Kilimanjaro Stars inawania ubingwa huo kwa mara ya tatu mfululizo.

Viwango bora vya wachezaji hao, vimenikumbusha wachezaji wa zamani wa Twiga Stars waliokuwa chini ya Kocha Idd Machuppa mwanzoni mwa miaka ya 2000.

Hapa nawazungumzia Esther Chaburuma ‘Lunyamila’, Sweet Paul na aliyekuwa nahodha Mwaka Kaveva ambao waliibeba Twiga Stars na Kilimanjaro Queens katika michuano mbalimbali kwa muda wote kabla ya kustaafu.

Lunyamila na Sweet walikwenda Ulaya kucheza soka la kulipwa licha ya kutoa mchango mkubwa kwa Taifa kutokana na vipaji vyao.

Esther ambaye alikuwa maarufu zaidi kwa jina la Lunyamila alilopewa na mashabiki akilinganishwa na nyota wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Edibily Lunyamila, alicheza kwa mafanikio Ulaya na hata aliporejea aliendeleza ubora wake kwa timu ya Taifa.

Vipaji vya Kilimanjaro Queens na Zanzibar mwaka huu vinathibitisha Tanzania ilivyokuwa na hazina ya kutosha ya wachezaji wenye viwango bora ambao ni muda mwafaka kwao kwenda kucheza soka la kulipwa nje ya nchi.

Winga wa Kilimanjaro Queens Donisia Minja ni mfano wa wachezaji wenye sifa ya kucheza soka la kulipwa nje baada ya kuonyesha kiwango bora katika michuano hiyo. Pia wamo Opa Clement, Stumai Abdallah, Happiness Mwaipaja na Julitha Tamuwai ambao walikonga nyoyo za mashabiki.

Naamini michuano hiyo ilishuhudiwa pia na mawakala mbalimbali ambao wameona vipaji vya wachezaji wetu, hivyo ni wakati mwafaka kwao kutengeneza mtandao wa kuwatafutia timuza nje.

Mawakala wana nafasi kubwa ya kukuza kiwango cha soka nchini ikiwa watawajengea uwezo wachezaji wetu kwa kuwatafutia masoko nje ya nchi kwenda kuendeleza vipaji vyao.

Kama wanavyofanya kwa wanaume, mawakala hao sasa wageukie soka la wanawake kuendeleza vipaji vyao kuhakikisha vinachomoza kwa wingi nje ya mipaka ya Tanzania.

Hata hivyo, mawakala watakuwa na wigo mpana wa kupata wachezaji bora ikiwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) litaboresha Ligi Kuu ya wanawake kwa kusaidia kutoa udhamini ambao utakuwa chachu ya kupata timu zenye ushindani katika ngazi ya klabu.

Shirikisho hilo ambalo ndilo msimamizi mkuu wa soka nchini, lina wajibu wa kutoa miongozo katika ngazi ya klabu na vyama vya michezo vya mikoa kutengeneza mfumo bora utakaokuwa na manufaa kwa wachezaji wetu.

Ni vyema TFF ikatupia jicho soka la wanawake kwa kutengeneza mfumo utakaotoa nafasi kwa wachezaji kuanzia ngazi ya shule, vyuo na mtaani kupenda mchezo huo.

Pia mfumo huo utakuwa na manufaa endapo TFF itaongeza kasi ya kusaka wadhamini ili kupata ligi bora yenye ushindani ambayo itakuwa chimbuko la kupata wachezaji hodari wa timu za Taifa.

Hakuna namna zaidi ya kuwekeza kwa vijana ili kupata wachezaji ambao watakuwa hazina kwa timu zetu za Taifa. Taifa la Ethiopia ambalo kwa muda mrefu lilipitia katika vurugu za kisiasa, limefanikiwa kupata timu bora za soka la wanaume na wanawake baada ya kuwekeza.

Ni vyema kuiga kwa wenzetu waliopiga hatua katika eneo hilo mfano nchi za Ulaya ambazo klabu zao zimewekeza kwa kiwango cha juu katika soka la wanaume na wanawake.