Mazoezi kwa watu wasiojiweza

Umewahi kujua kuwa wale ambao hawawezi kufanya lolote wakiwa wamelala kitandani wanahitaji mazoezi ya mwili ili kuboresha afya na kujikinga na magonjwa?

Mazoezi si kwa wale wanaosimama na kutembea, kukimbia, kuogelea na kuendesha baiskeli bali hata wale waliolala pasipo kufanya lolote kama vile kupooza au kuzeeka.

Katika nchi zilizopiga hatua katika huduma za afya kuna vituo maalumu kwa ajili ya huduma kwa watu wa aina hii na moja ya huduma ni kuwafanyia mazoezi ya viungo.

Watu wa aina hii hujulikana kwa lugha ya kitaalamu kama Bed ridden Elderly or Patient.

Mara nyingi huwa ni wazee au wagonjwa wa kupooza viungo vya mwili, wengi huwa wanasaidiwa kufanya mambo mengi ikiwamo kulishwa, kwenda kujisaidia na kufanyiwa usafi.

Lakini bado jamii zetu za nchi zinazoendelea zinajisahau kuwa watu hawa wanahitaji huduma ya mazoezi ili kuwakinga na magonjwa ambayo yanaepukika.

Majumbani tunaweza kuwa na watu wa aina hii wamelala tu wakiumwa au kutokana na uzee huwa hawafanyiwi mazoezi yoyote pengine kutokana na watu hao kukosa ufahamu.

Moja ya tatizo baya la kiafya wanaloweza kupata watu wa aina hii ni tatizo lijulikanalo kitabibu kama Bed sores au pressure sores.

Ni aina ya vidonda vibaya ambavyo vikimpata mtu aliyelala tu kwasababu za uzee au ugonjwa huchelewa kupona na huwa na madhara mabaya.

Mazoezi kwa watu aina hii huwa ni muhimu ili kuwakinga na matatizo ya kiafya kama vile kuzuia kusinyaa na kupungua ukubwa wa misuli na pia kusaidia viungo vya mwili kuimarika.

Mara nyingi vidonda hivi vinajitokeza mara kwa mara zaidi katika makalio, chini ya mgongo, katika nyonga mabegani, nyuma ya mikono au miguu eneo lilolaliwa na uzito wa mwili.

Lakini vidonda hivi vinaweza kuzuiwa kirahisi endapo mgonjwa atakuwa anafanyishwa mazoezi kwa msaada kutoka kwa ndugu au jamaa wakaribu wanaomuuguza.

Wagonjwa wa aina hii wanahitajika angalau kwa siku kufanyishwa mazoezi mara moja kwa dakika 20-30 kwa siku tano kwa wiki.

Mazoezi wanayoweza kufanyishwa ni pamoja na mazoezi ya kunyoosha viungo vya mwili kuanzia katika shingo na kichwa, kiwiliwili, mikono , mikono na miguu.

Mazoezi ya kunyoosha viungo yajikite katika maungio ya mwili ikiwamo kifundo cha mguu, goti, viganja, kiwiko, mabega, nyonga na shingo.

Mazoezi ya watu wa aina hii yanaweza kuwa ya mchanganyiko ikiwamo mazoezi ya kupasha mwili moto, mazoezi ya kunyoosha viungo na kuimarisha uimara wa misuli.

Anayemfanyisha anaweza kuweka hesabu ya kukifanyisha kila kiungo ikiwamo kukikunja na kukikunjua au kukinyoosha na kukikunja mara kumi au zaidi katika kile uelekeo wa zoezi.

Zile sehemu ambazo ziko katika hatari ya kupata vidonda vinatakiwa kunyooshwa, kusingwa (massage) au kutomaswa pamoja na kugeuzwa geuzwa pande tofauti tofauti.

Kufanya hivi kunaondoa shinikizo katika eneo lililolaliwa na kugandamizwa na uzito wa mwili.

Mgandamizo wa eneo la mwili kwa muda mrefu husababishwa kuzuiwa kwa damu kutiririka katika eneo hilo.

Hivyo aina hii ya mazoezi mepesi huweza kusababisha mzunguko mzuri wa damu kwa wazee wasiojiweza au wagonjwa waliolazwa muda mrefu kitandani.

Kama mazoezi yatafanyika kwa ufanisi na kufuata ratiba huweza kuleta matokea makubwa kwa wazee wasiojiweza au wagonjwa na huboresha maisha ya wagonjwa hivyo kuweza kuishi maisha marefu.

Mwandishi wa makala haya ni daktari wa magonjwa ya binadamu