UCHAMBUZI: Mchango wa TRA katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais John Magufuli

Muktasari:

Pamoja na changamoto kadhaa zilizopo, Rais John Magufuli amefanikiwa kwenye maeneo mengi ndani ya miaka mitatu ya uongozi wake. Miongoni mwa mafanikio hayo ni ukusanyaji wa mapato, jukumu linalotekelezwa kwa umakini na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA).

Watanzania wameshuhudia miaka mitatu ya utawala wa Rais John Magufuli wenye mafanikio katika ukusanyaji wa mapato yanayotokana na kodi.

Mafanikio hayo ni muhimu kwani hakuna nchi iliyoendelea bila watu wake kulipa kodi. Nchi zote zilizopiga hatua na kufanikiwa kuboresha huduma za afya, miundombinu ya umeme, usafirishaji, elimu na mengine mengi wananchi wake hulipa kodi kwa hiari na kwa wakati.

Kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato nchini kumetokana na ushiriki wa viongozi kupambana na ukwepaji kodi unaosababisha upotevu wa mapato. Katika kipindi hiki tumeshuhudia mapambano makali dhidi ya ukwepaji kodi na upotevu wa mapato ya Serikali.

Akifungua rasmi Bunge la 11 jijini Dodoma mwishoni mwa 2015, Rais Magufuli aliahidi kupambana na ukwepaji kodi na upotevu wa mapato ya Serikali, na amekuwa akisisitiza umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo ya Taifa.

Vilevile, amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha wananchi kulipa kodi kwa hiari huku akikemea udanganyifu unaofanyika kwenye risiti za kielektroniki (EFD), jambo linalorudisha nyuma ukusanyaji mapato.

Katika miaka mitatu ya uongozi wa Rais Magufuli, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imefanikiwa kuongeza ukusanyaji mapato kutoka wastani wa Sh850 bilioni kwa mwezi mwaka 2015 hadi Sh1.3 trilioni.

Kwa miaka mitatu iliyopita, ukusanyaji umeongezeka kila mwaka ambapo mwaka 2015/16 yalikuwa Sh12.5 trilioni, 2016/17 yakafika Sh14.4 trilioni na 2017/18 yakawa Sh15.5 trilioni na kufanya jumla ya Sh42.4 trilioni ndani ya kipindi hicho.

Pia, taarifa ya makusanyo ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa fedha 2018/19 kuanzia Julai hadi Septemba 2018, TRA imekusanya Sh3.84 trilioni ikilinganishwa na Sh3.65 trilioni zilizokusanywa kipindi kama hicho 2017/18.

Ongezeko la ukusanyaji mapato ni hatua ambayo kwa kiasi kikubwa imechangiwa na udhibiti wa mianya ya ukwepaji kodi.

Ukiachilia mbali kuongezeka kwa makusanyo, TRA imefanikiwa kuboresha mifumo ya ukusanyaji mapato kwa lengo la kumrahisishia mwananchi kulipa kodi stahiki na kwa wakati.

Moja ya yaliyofanyika ni la uhakiki wa namba ya utambulisho wa mlipakodi (TIN), kwa nia ya kuboresha daftari la walipakodi na kuifanya namba hiyo itumike katika mawasiliano na TRA hususan katika huduma za kielektroniki.

Katika muktadha wa kuhakikisha watu hawakwepi kodi, TRA imeendelea kudhibiti uingizaji wa bidhaa za magendo kwa kuimarisha doria mipakani na mipaka isiyo rasmi ambayo ni maarufu kwa kupitisha bidhaa za magendo. Udhibiti huu unalenga kuhakikisha bidhaa zote zinazoingizwa nchini zinapita njia rasmi na kulipiwa kodi na ushuru stahiki ikiwa ni njia ya kulinda viwanda vya ndani.

Aidha, idara ya huduma na elimu kwa mlipakodi imejikita kuwahudumia na kuwaelimisha walipakodi na wadau mbalimbali umuhimu wa kulipa kodi kwa hiari, kwa manufaa yaTaifa lao.

Kupitia idara hiyo, mamlaka imefanikiwa kuongeza uelewa wa masuala ya kodi kwa wananchi.

Mafanikio mengine ni ufunguzi wa vituo vya pamoja vya huduma mipakani kikiwamo cha Rusumo na Mutukula mkoani Kagera. Vituo vingine ni Holili cha Kilimanjaro na Tunduma mkoani Songwe.

Vituo hivi kwa pamoja husaidia kuharakisha utoaji wa huduma mipakani, kuokoa muda wa kushughulikia mizigo na abiria, kukuza biashara na hatimaye kuongeza ukusanyaji mapato baina ya nchi zinazopakana.

Sambamba na hayo, Serikali imeendelea kuwajali na kuimarisha uhusiano na wafanyabiashara nchini ambapo kuanzia Julai Mosi imetoa msamaha maalumu wa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi kwa asilimia 100 na mwisho wa kuwasilisha maombi ya msamaha huo itakuwa Novemba 30.

Msamaha huo unalenga kutoa unafuu kwa walipakodi wenye malimbikizo ya madeni kwa kuwapa fursa ya kulipa kodi ya msingi baada ya kuondoa riba na adhabu kabla ya Juni 30, 2019.

Hadi mwishoni mwa Oktoba, TRA ilikuwa imepokea maombi kutoka kwa walipakodi 2,029 yanayofikia jumla ya Sh245.6 bilioni.

Baadhi ya walipakodi hawa wameshapewa majibu na waliobaki wapo katika hatua mbalimbali za kushughulikiwa maombi yao.

Kuondoa riba na adhabu kwenye malimbikizo ya madeni ya kodi ni hatua mojawapo ya kuwasaidia wafanyabiashara wenye malimbikizo hayo kutokwepa kodi ikiwa ni sehemu ya ahadi ya Rais kuhakikisha mianya ya ukwepaji inadhibitiwa ipasavyo.

Mwandishi ni ofisa habari wa TRA. Anapatikana kwa namba 0753 986 541