Mgawanyo wa madaktari uguse maeneo ya vijijini

Friday February 9 2018Peter  Elias

Peter  Elias 

Wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere, Serikali yake ilibainisha maadui watatu ambao ni ujinga, umasikini na maradhi. Mapambano dhidi ya maadui hao yalipewa uzito sawa licha ya kwamba hayakufanikiwa kwa asilimia 100.

Serikali za awamu zilizopita ziliendeleza mapambano dhidi ya maadui hao. Hata ilipoingia madarakani Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli iliendeleza jitihada za kupambana na maadui hao watatu wa tangu uhuru.

Nikijielekeza kwenye adui maradhi, ninaiona vita hii kama muhimu zaidi hasa katika zama hizi ambazo kuna maradhi mengi yanayosababishwa na mabadiliko ya tabianchi na mitindo ya maisha. Rais Magufuli alitoa maagizo muhimu wakati akifungua Kituo cha Mafunzo ya Kitabibu cha Mloganzila (Mamc), Novemba 25, mwaka jana, yalioonyesha dira na matumaini makubwa katika utoaji wa huduma bora za afya hapa nchini.

Kiongozi huyo alishauri madaktari waliojazana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) watawanywe kwenye hospitali nyingine nchini ikiwamo Hospitali ya Mloganzila ambayo itakuwa ikitoa pia mafunzo kwa wanafunzi wa fani ya udaktari.

Pia, aliwaagiza mawaziri wa afya na Tamisemi kuangalia uwezekano wa kuzifanya hospitali zote za mikoa ambazo zilikuwa chini ya Wizara ya Tamisemi ziwe chini ya Wizara ya Afya ili zihudumiwe kwa ukaribu zaidi. Jambo hilo tayari limetekelezwa. Jambo kubwa ambalo liliwagusa wengi lilikuwa ni kuhamishwa kwa madaktari waliokuwa wamelundikana Hospitali ya Muhimbili wakati hospitali nyingine za mikoa na rufaa zikikosa wataalamu wa afya.

Tunaambiwa watu wengi zaidi wanapatikana vijijini, lakini pamoja na wingi wao wanakosa huduma za afya za uhakika kwa sababu hospitali zao siyo tu zinakosa dawa na vifaatiba muhimu, bali hazina madaktari wa kutosha. Ni ukweli ulio wazi kwamba madaktari wengi hasa wale bingwa wanapenda kukaa mijini ndiyo maana wengi walikuwa Hospitali ya Muhimbili, jambo lililokuwa likisababisha wagonjwa kutoka maeneo mbalimbali nchini kuja Dar es Salaam kuwafuata wao. Muhimbili ilikuwa inaelemewa na wagonjwa wengi wanaotoka mikoani kuja kufuata huduma. Kufunguliwa kwa Hospitali ya Mloganzila kumepunguza foleni kubwa ya wagonjwa MNH.

Tatizo lililopo ni kwenye hospitali za mikoa, hazina wataalamu wa kutosha. Pia, vituo vya afya na zahanati za vijijini havina wataalamu wa afya wa kutosha, wanalazimika kwenda kwenye hospitali za mikoa au Muhimbili. Wakati Serikali ikitekeleza mgawanyo wa madaktari kwenye hospitali za mikoa, ivikumbuke vituo vya afya vilivyopo vijijini kwa sababu kama havitakuwa na uwezo wa kuwahudumia wagonjwa, hospitali za mikoa zitazidiwa.

Nchi hii ina wataalamu wa afya wa kutosha, tatizo lililopo ni mgawanyo sahihi ambao unagusa maeneo mbalimbali. Madaktari wengi wamejazana eneo moja pengine kwa sababu ya mapenzi yao binafsi katika eneo husika mathalani mkoani Dar es Salaam. Sekta ya afya ni muhimu kwa sababu inagusa uhai wa kila mwanajamii. Bila afya njema, Taifa haliwezi kutimiza malengo yake ikiwamo kukuza uchumi, kutoa huduma za kijamii na kukusanya mapato.

Natambua jitihada zinazofanywa na serikali katika sekta hii, lakini jitihada za makusudi zinahitajika ili kuwahakikishia wananchi usalama wa afya zao pindi wanapokabiliwa na maradhi mbalimbali. Serikali makini inawekeza kwenye sekta ya afya kwa sababu afya ni mali na wananchi wenye afya dhaifu hawawezi kuzalisha chochote.

Kwa pamoja tukishirikiana, tutajijengea mazingira bora na ya uhakika ya huduma za afya .

0763891422

kwa manufaa yetu wenyewe na vizazi vyetu vijavyo. Wananchi tutimize wajibu wetu, Serikali nayo itimize wajibu wake katika mapambano dhidi ya adui maradhi.