Mgogoro Acacia, wananchi sasa ufike mwisho

Muktasari:

  • Hivi karibuni timu ya makatibu wakuu watano kutoka katika wizara mbalimbali ikiwamo Nishati na Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Maji wakiongozwa na katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Malongo walitembelea mgodi huo na kuagiza kufanyika kwa kikao cha maridhiano.

Mgogoro wa fidia baina ya wakazi wa vijiji vinavyozunguka mgodi wa dhahabu wa Acacia North Mara uliopo Nyamongo wilayani Tarime na mgodi huo umekuwa ni wimbo wa miaka nenda - miaka rudi.

Hivi karibuni timu ya makatibu wakuu watano kutoka katika wizara mbalimbali ikiwamo Nishati na Madini, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira); Ardhi na Nyumba na Maendeleo ya Makazi pamoja na Maji wakiongozwa na katibu mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Joseph Malongo walitembelea mgodi huo na kuagiza kufanyika kwa kikao cha maridhiano.

Kwa mujibu wa mawaziri hao, Wizara ya Ardhi, ofisi ya mkuu wa Mkoa wa Mara pamoja na uongozi wa mgodi huo wanapaswa kukutana na kutatua mgogoro huo wa fidia.

Kauli za mawaziri hao zinafuatia agizo lililotolewa Septemba 7, mwaka jana na Rais John Magufuli wakati wa ziara yake mkoani Mara ambapo alipokea malalamiko ya wananchi juu ya fidia wanayodai mgodini muda mrefu.

Katika ziara hiyo, Rais Magufuli aliziagiza mamlaka husika kuhakikisha kuwa suala hilo linapata ufumbuzi wa kudumu.

Ni matarajio yangu kuwa suala hili sasa litafikia ukingoni na kila upande utapata haki yake ili amani iweze kutawala, lakini kubwa zaidi ikiwa ni shughuli za maendeleo ziweze kufanyika kama kawaida.

Naamini pamoja na mgogoro huo kuchukua muda mrefu endapo utatatuliwa wahusika watakuwa wamepata mwarobaini kama siyo suluhusho la kudumu juu ya uhusiano mbaya kati ya wananchi na mgodi huo.

Nasema hivyo kwa kuwa hivi sasa baadhi ya watu wamekuwa wakitumia mgogoro huo ambao kila upande unadai una haki kuwa ni mtaji wa kisiasa hasa unapofika wakati wa chaguzi huku wanaharakati nao wakijaribu kuingilia kati bila mafanikio.

Aidha, mgogoro huo umekuwa ukitajwa kuwa miongoni mwa visababishi vikuu vya uhusiano mbaya kati ya mwekezaji na wananchi hao.

Kwa muda mrefu kumekuwapo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya wananchi wanaodai kupunjwa malipo yao, huku mgodi huo ukisisisitiza kuwa malipo hayo ni halali.

Hatua hiyo iliwahi kusababisha baadhi ya wananchi kususia hundi za malipo na kuitaka Serikali kuingilia kati lengo lao likiwa ni ili wapate stahili zao bila kupunjwa.

Ikumbuke kuwa wawekezaji wakubwa kama Acacia wanahitajika nchini ili kuweza kusukuma gurudumu la maendeleo ya jamii.

Hakuna ubishi kuwa kama huwezi kufanya maendeleo endelevu katika eneo lenye migogoro, huwezi kufanikisha lengo zima la kuwaendeleza watu wote kwa wakati mmoja.

Pia ili mwekezaji apate faida na kulipa kodi suala la amani na utulivu si tu ni jambo la msingi, bali ni nguzo muhimu kwa mustakabali wa uwekezaji wa aina yoyote.

Umefika wakati sasa tuseme basi na kila mwenye haki apate haki yake maana kama ni kutumika au kunufaika nao wamenufaika.

Mara zote katika mgogoro huu wananchi wamekuwa waathirika wakuu kiasi kwamba miongoni mwao wamewahi kupoteza maisha.

Sitarajii ‘hadithi’ hii kuendelea kusikika katika masikio ya Watanzania kwa vile ninaamini kuwa mamlaka zilizopewa jukumu la kulishughulikia suala hili zina uwezo mkubwa wa kulitatua kwa kutumia wataalamu wake.

Jambo la msingi katika kukabiliana na mgogoro huo ni kwa pande zote kuzingatia sheria, taratibu na kanuni ambazo zitawaongoza kufikia uamuzi badala ya kuweka mbele masilahi yao.

Upo uamuzi ambao hapo awali ulifanywa na mamlaka mbalimbali katika kuhakikisha suala hili linafikia mwisho, lakini sijui ni kwa makusudi au ni bahati mbaya mgogoro huo haukumalizika.

Mfano wa uamuzi huo ni ule uliofanywa na kamati ya mwaka 2016 iliyoundwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo kuchunguza chanzo cha migogoro kati ya wakazi wa vijiji hivyo pamoja na kufanya tathmini ya fidia katika eneo hilo.

Kamati hiyo pamoja na mambo mengine iligundua kuwa mgogoro huo ulikuwa ukisababishwa na madai ya muda mrefu ya fidia.

Pia ilibaini kuwa wananchi hao walikuwa wanadai zaidi ya Sh11 bilioni kama fidia, jambo ambalo lilisababisha waziri huyo kuagiza mgodi huo uhakikishe kuwa fidia hiyo inalipwa kabla ya Mei 31, 2017. Hata hivyo, Profesa Muhongo mpaka anaondoka madarakani agizo hilo halikutekelezwa.

Hata hivyo, sitarajii agizo la hivi karibuni iwapo pia litapotelea hewani kama ilivyotokea kwa maagizo mengine ya awali. Ni wazi kwamba wananchi wamechoka kila siku kusikia juu ya suala moja tu la fidia, kwani yapo mengi ya msingi ambayo yanawatatiza watu hao wanaozunguka mgodi huo ikiwamo kuwekewa mazingira mazuri ya kilimo.

Beldina Nyakeke ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Mara, anapatikana kwa simu namba 0784 561 531