MAONI: Mhariri wa Jamii ni mtumishi wako, acha woga

Friday January 17 2020Ndimara Tegambwage ni  Mhariri Meza ya wa Jamii

Ndimara Tegambwage ni  Mhariri Meza ya wa Jamii 

Mpaka sasa nimepokea maoni ya wasomaji 12 juu ya makala yangu ya Ijumaa iliyopita iliyokuwa na kichwa, “Mawazo yako mtaji wako katika chombo cha habari.”

Mmoja wa wasomaji ametoa maoni kama ifuatavyo: “Kumbe Ndiyo maana gazeti limegeuka la Ovyo akina Ndimara Tegabwange bado wamejibanza kwenye kichaka cha Uhariri wa Jamii kumbe wanafanya Siasa. Ndimara kinara wa Upinzani anakuwagaje Mhariri kwenye gazeti linalodai halina upande wa kisiasa?” (maoni hayakuhaririwa).

Maoni haya yamewasilishwa kwa njia ya Twitter yakiwa na jina la Dr. Frey Edward Cosseny @CossenyEdward. Hayana mfano wowote kuwa “gazeti limegeuka kuwa la ovyo.” La ovyo vipi. Limegeuka tangu lini. Awali lilikuwa vipi. Ni maoni yake lakini ya jumlajumla tu.

Katika mazingira ya kawaida maoni haya yanastahili kujibiwa na mwajiri wa Mhariri wa Jamii. Lakini kwa kuwa mimi ndiye Mhariri wa Jamii, na hata kama jina langu la pili limekosewa – kwa makusudi au bila kukusudiwa – nina sehemu ya kujibu; na ndivyo nifanyavyo sasa.

Naomba wasomaji wajue kuwa Meza ya Mhariri wa Jamii haisikitiki wala kuchukia kupokea kauli za aina hii. Ukweli ni kwamba ninazipokea mara kwa mara na kuzijibu. Mara zote nimeeleza kuwa “hicho ni sehemu ya chakula” cha Mhariri wa Jamii. Sasa twende pamoja. Mhariri wa Jamii haandiki habari – zile stori zinazosomwa magazetini na kwenye mitandao ya kijamii. Hatoi maoni juu ya kipi cha kuandika na jinsi gani kiandikwe.

Mhariri wa Jamii hapitii kinachotakiwa kuchapishwa. Kazi hii inafanywa na walioajiriwa kuifanya; nao ni maripota, wasanifu wa habari na wahariri kwa ngazi mbalimbali. Kile ambacho walio katika chumba cha habari wametafuta au wamepokea kutoka kwa wenzao, ndicho wanafanyia kazi. Kwahiyo, wanapokea, wanasoma, wanamwita aliyeleta taarifa ili kupata taarifa zaidi; wanafanya uhakiki wa taarifa na vyanzo vyake; wanafanya uamuzi na kuchapa kile ambacho kinatokea baadaye kuwa habari.

Advertisement

Ni hivi: Mhariri wa Jamii anaona gazeti na kulisoma kama mteja mwingine aliyelinunua kituoni au mkononi mwa wauza magazeti; au analisoma kwenye mitandao ya kijamii kama wengine wanavyosoma. Hastahili, hatakiwi na hana hata uwezo wa kushawishi. Bali, kuna nafuu kwa wasomaji wanaonunua nakala kituoni au mkononi mwa muuzaji. Maoni ya msomaji yaweza kuchukuliwa kwa uzito wake na kufanyiwa kazi; na kwa njia hiyo akawa miongoni mwa wamiliki wa chombo husika.

Lakini moja ya kazi kuu za Mhariri wa Jamii ni kupokea na kusoma katika barua, kwenye Twitter, baruapepe, mitandao ya kijamii na hata kwa simu maoni ya wasomaji juu ya vyombo vya habari. Zaweza kuwa pongezi, lawama, shutuma, malalamiko, masahihisho; chochote walichonacho.

Hapo ndipo Mhariri wa Jamii anakuwa kiungo cha msomaji na wanaoendesha vyombo vya habari. Anapokea maoni, anajibu maswali; mengine anayafanyia uchunguzi; anawasilisha matokeo ya uchunguzi kwa kampuni akiwaambia: hivi ndivyo wasomaji wanavyowaona; wanavyoona kazi zenu; wanavyotaka viandikwe au wasivyotaka kuona na kusoma.

Mhariri wa Jamii basi ni jicho la wasomaji lakini pia mdomo wao; na kwa hiyo nguvu yao katika kumiliki vyombo hivyo kwa njia ya kutoa maoni; kwani hoja zinazodai utekelezaji huweza kutekelezwa iwapo zimethibitishwa kwa utafiti na kukutwa zinakidhi kanuni za taaluma.

Aidha, kwa maoni ya wasomaji na kwa kupitia Mhariri wa Jamii, malalamiko ya kawaida ya wasomaji, ambayo si ya madai ya kwenda mahakamani, huweza kuishia mezani kwa kuyatolea maelezo; na hata kwa kuomba radhi pale inapostahili.

Licha ya kupokea maoni ya wasomaji, kuyachambua, kuyatafiti, kuyawasilisha kwa wanaohusika ili yafanyiwe kazi na kujibu wasomaji, Mhariri wa Jamii ana kazi nyingine ya kuchunguza kama kweli kazi ya uandishi inayofanywa inakwenda kwa misingi ya maadili ya taaluma.

Hii nayo anaifanya baada ya kusoma na kuchambua magazeti, taarifa na habari katika magazeti na kwenye mitando ya Mwananchi Communications Limited (MCL).

Ukweli ni kwamba katika utoaji habari wa kila saa na kila siku, inawezekana kukawa na kosa hapa au pale. Ni makosa hayo, hasa ya kitaaluma, ambayo huonwa na wasomaji na mengine kuonwa na Mhariri wa Jamii, ambaye huyaweka bayana mbele ya watendaji kwa niaba ya wasomaji ili yaweze kusahihishwa.

Hii ni kazi inayofanywa kwa umakini na mtu makini; bila woga, bila upendeleo na bila nia mbaya. Wasomaji pamoja na anayeitwa Dr. @CossenyEdward, wanaalikwa kutembelea kampuni ya MCL kupata maelezo juu ya chochote wanachotaka kujua zaidi. Ni vema kurejea kaulimbiu ya Meza ya Mhariri kwamba mawazo yako ndio mtaji wako katika chombo cha habari. Tunajali. Kila maoni ni maoni. Leta maoni yako.

Mhariri Jamii anapatikana kwa namba 0763670229