Guardiola adai Man City imenyimwa penalti mbili

Muktasari:

Kocha wa Manchester City ametoa matamshi makali kwa mwamuzi wa mechi ya jana Mike Dean kwa madai ya kuwanyima penalti mbili dhidi ya Liverpool.

London, England. Kocha Pep Guardiola amechukizwa Manchester City kutopewa penalti mbili alizodai zilikuwa halali katika mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Liverpool.

Guardiola alionekana akimtolea maneno makali mwamuzi namba nne wa mchezo Mike Dean kabla ya kushikana mkono na mwamuzi wa kati Michael Oliver.

Kocha huyo alidai Man City ilistahili kupewa penalti mbili katika mchezo huo ambao timu hiyo ilifungwa mabao 3-1, yaliyofugwa na Fabinho, Mo Salah na Sadio Mane.

Matokeo hayo yameifanya Liverpool kufikisha pointi 34 na Man City 26 katika msimamo wa Ligi Kuu na zote zimecheza mechi 12 kila moja.

Guardiola alilalamikia tukio la kwanza la beki Trent Alexander-Arnold kushika mpira akiwa ndani ya eneo la hatari.

Hata hivyo, msaada wa teknolojia ya VAR ilipotumika ilionekana kama kinda huyo hakukusudiam kushika mpira.

Alexander-Arnold alishika tena mpira akiwa ndani ya eneo la hatari, lakini Oliver alisema haikuwa penalti.

Matukio yote mawili yalimfanya kocha huyo kutoa kauli kali kwa Dean akidai Man City haikutendewa haki.

Wakati wachezaji wakishikana mikono baada ya mpira kumalizika, Guardiola alimfuata Oliver na kumwambia: Asante. Asante sana”.

Kocha huyo wa zamani wa Barcelona na Bayern Munich alisema hana namna zaidi ya kuipongeza Liverpool kwa matokeo hayo.