TFF yaiweka Yanga mtegoni

Wednesday August 20 2014

 

By Vicky Kimaro, Mwananchi

Dar es Salaam. Yanga ipo kwenye hatari  ya kuondolewa  kwenye Ligi Kuu iwapo uongozi  wake utashindwa kuwasilisha muhtasari wa kikao cha  mabadiliko ya katiba ya klabu hiyo ndani ya siku saba.

Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) jana limeupa  uongozi wa klabu hiyo siku saba kuwasilisha muhtasari  wa kikao chake, la sivyo sheria itachukua mkondo wake.

Kwa mujibu wa kanuni ya 29 ya ligi inayozungumzia  udhibiti wa viongozi, kipengele (e) kiongozi wa klabu akishindwa kutoa taarifa zinazohitajika  kwa kipindi  cha siku 30, atafungiwa kwa kipindi kisichozidi miezi sita.

Pia, kanuni hiyo imeweka wazi katika kipengele (h)  ikisema  kuwa kiongozi au  klabu itawajibika kufuata  na kutii uamuzi au maagizo ya TFF.

Inaeleza kanuni hiyo kuwa atakayeshindwa kutii  uamuzi au maagizo hayo atafungiwa kwa kipindi  kisichopungua miezi sita (6)  au kutozwa faini ya Sh1  milioni au vyote kwa pamoja.

Kwa upande wa kilabu, endapo itashindwa  kutekeleza kanuni hiyo itaondolewa kwenye  mashindano na kushushwa daraja.

Jana, ofisa habari wa TFF, Bonifance Wambura  alisema kuwa shirikisho  hilo tayari limeiandikia Yanga  barua kwa mara ya pili  kuwakumbusha wawasilishe  muhtasari wa kikao chake cha mabadiliko ya katiba  kilichofanyika Juni Mosi kwenye ukumbi wa Bwalo la  Maofisa wa Polisi, Oysterbay jijini Dar es Salaam.

Alisema  TFF imeipa klabu hiyo siku saba  za  kuwasilisha muhtasari huo kwa kuwa muda wa viongozi  wao kukaa madarakani ulishamalizika.

“Tumewaandikia Yanga kwa mara nyingine  kuwakumbusha kuleta muhtasari wao na hawaruhusiwi  kupeleka katiba yao kwa msajili wa vyama vya michezo  hadi TFF ipitie kwanza na kuangalia iwapo imekidhi  vigezo vinavyotakiwa,”alisema Wambura

Aliongeza kuwa TFF haikubaliani na kamati za muda,  hivyo kitendo cha uongozi wa Yanga kuendelea  kubaki madarakani wakati muda wao wa uongozi  umemalizika ni sawa na kamati ya muda.

Kwa sababu hiyo, baada ya sikusaba kumalizika,  shirikisho hilo  litatoa msimamo ambao Yanga  watalazimika kuufuata.

“Kanuni zipo wazi, kama klabu ikipewa maelekezo ni  lazima wayafuate isipofuata kinachofuata  kinajulikana.”alisema

Tayari, TFF ilishaweka msimamo wa kutotambua kamati zilizoteuliwa na uongozi wa Yanga hivi karibuni  na kueleza kuwa ni batili kwa vile uongozi huo  umeshindwa kuwasilisha muhtasari wa mkutano wa  mabadiliko ya katiba kama wanavyotakiwa kikanuni.

Mkurugenzi msaidizi wa  uanachama  wa TFF, Eliud Mvela aliwahi kusema kuwa kitendo walichofanya Yanga ni kinyume cha katiba kwa kuwa uamuzi waliyopitisha katika mkutano wao hawatakiwi kuyafanyia kazi  hadi TFF na msajili wa vyama vya michezo ahalalishe.

Ofisa habari wa  klabu hiyo, Baraka Kizuguto  amekuwa akidai kuwa hakuna kipengele  kinachowabana  wala kuwalazimisha kuwasilisha  mapendekezo yao.

Hata hivyo,  jana Kizuguto alipoulizwa kuhusiana na  kupewa muda wa siku saba  alijibu kwa kifupi: “Katibu  amesema hawezi kukujibu swali lako.

Advertisement