Amunike awatega nyota 18 Stars

Dar es Salaam. Wakati Jonas Mkude na Ibrahim Ajibu wakienguliwa kwenye kikosi cha timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kilichoondoka jana kwenda kuanza kambi huko Misri kwa ajili ya maandalizi ya Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON), wachezaji 18 kati ya 32 walioteuliwa, wapo kwenye presha kubwa ya kupigania kushiriki fainali hizo zitakazofanyika Juni 21 hadi Julai 19.

Wachezaji hao 18 wana kazi ngumu ya kufanya katika kambi hiyo ndani ya siku nne zijazo ili kulishawishi benchi la ufundi kuwajumuisha katika kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 ambao watashiriki fainali za AFCON.

Kwa mujibu wa kanuni za mashindano hayo, kila timu inapaswa kuwasilisha orodha ya wachezaji 23 itakayowatumia, siku 10 kabla ya mechi ya kwanza ya mashindano na itakayochelewa kufanya hivyo itatozwa fainali ya Dola 20,000 (Sh 40 milioni).

Kwa vile mashindano hayo yanaanza Juni 21, Stars na timu nyingine zinapaswa kuwasilisha vikosi vya wachezaji 23 watakaoshiriki mashindano hayo, Jumanne ijayo ambayo itakuwa ni Juni 11.

Wachezaji hao 18 ambao wako kwenye ushindani mkali wa kutafuta nafasi ya kuwemo kwenye kikosi kitakachopeperusha bendera ya Tanzania katika mashindano hayo yatakayoshirikisha nchi 24, ni pamoja na makipa Metacha Mnata, Seleman Salula na Claryo Boniface wakati mabeki ni Vicent Philipo, Gadiel Michael, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, David Mwantika na Abdi Banda.

Viungo ambao hadi sasa hawajawa na uhakika kama watakuwamo kwenye kikosi cha mwisho ni Fred Tangalu, Yahya Zayd, Shiza Kichuya, Frank Domayo na Miraji Athuman wakati washambuliaji ni Thomas Ulimwengu, Kelvin John, Rashid Mandawa, Adi Yussuf na Shaban Iddi Chilunda.

Ingawa matarajio yanaweza kwenda tofauti, katika kundi la nyota 32 ambao wataingia kambini huko Misri, nyota 14 wanaonekana kuwa na nafasi kubwa ya kuwemo kwenye orodha ya mwisho kutokana na sababu mbalimbali.

Rekodi nzuri ya kinidhamu waliyonayo nje na ndani ya uwanja, kujituma, kufiti katika mbinu na mfumo wa kocha Emmanuel Amunike na uwezo wa kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani, ni vigezo ambavyo kiuhalisia vinavyowafanya mastaa hao 14 kuingiza mguu mmoja kwenye mashindano hayo.

Wachezaji hao ambao labda majeraha tu ndiyo yanaweza kuwafanya wazikose fainali hizo au mipango ya benchi la ufundi ibadilike ghafla ni pamoja na nahodha Mbwana Samatta, Saimon Msuva, Farid Musa, Hassan Kessy, Kelvin Yondani, Aggrey Morris, Himid Mao, Erasto Nyoni, Aishi Manula, Mudathir Yahya, John Bocco, Aron Kalambo, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Ally Abdulkarim Mtoni ‘Sonso’.

Wakati Manula na Kalambo wakiwa kwenye nafasi nzuri ya kuwemo katika kikosi cha mwisho kutokana na uzoefu na kupevuka kwao, vita kubwa itakuwa kwa makipa Seleman Sakula, Metacha Mnata pamoja na Claryo ambaye ni mchezaji wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 20.

Makipa hao watatu watakuwa na kibarua cha kuwania nafasi moja ya kushiriki AFCON kwa upande wa golini na kuungana na Manula na Kalambo ambao ni kama wamejihakikishia kuwepo katika kikosi cha nyota 23.

Ukiondoa vita hiyo ya makipa hao watatu, shughuli pevu itakuwa kwa mabeki watano ambao ni Banda, Tshabalala, Mwantika, Phillipo na Gadiel Michael ambao nao baadhi wataingizwa kwenye kikosi cha mwisho cha wachezaji 23 na wengine wataachwa.

Kutokana na Gadiel kutumika kwenye takriban mechi zote za kuwania kufuzu, nafasi inaonekana kuwa kubwa kwake kucheza AFCON, lakini pia Banda kutokana na uwezo wake wa kucheza nafasi nyingi tofauti uwanjani, anaweza akafikiriwa na kujumuishwa kwenye kikosi kitakachowasilishwa CAF. Hata hivyo, mabeki Mwantika, Tshabalala na Phillipo watapaswa kupambana ili kujihakikishia nafasi kikosini.

Ikionekana kama viungo Himid Mao, Mudathir Yahya na Erasto Nyoni wapo kwenye nafasi nzuri ya kucheza AFCON, shughuli itakuwapo baina ya viungo Fred Tangalu, Yahya Zayd, Shiza Kichuya, Frank Domayo na Miraji Athuman ambao watakuwa wakigombea miongoni mwa nafasi tisa zinazobakia katika kikosi cha mwisho kitakachowasilishwa CAF.