Amunike azivutia kasi Senegal, Algeria Afcon

Oliver Albert na Charles Abel, Mwananchi

Dar es Salaam. Wakati wapinzani wa Tanzania katika Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), timu za Kenya, Senegal na Algeria zimepanga kuweka kambi Ulaya, Kocha wa Taifa Stars Emmanuel Amunike anatarajiwa kuweka hadharani mikakati yake Mei Mosi, mwaka huu.

Taifa Stars imepangwa Kundi C na Kenya, Algeria, Senegal katika fainali hizo zilizopangwa kuanza Juni 21 hadi Julai 19, mwaka huu nchini Misri.

Kenya inayonolewa na Kocha Mfaransa Sebastian Migne inatarajiwa kuweka kambi Ufaransa na itacheza mechi mbili dhidi ya Madagascar Juni kabla ya kuivaa Uganda Juni 14 au 15. Timu hiyo itaingia kambini Mei 30 hadi Juni 17.

Algeria itakayoweka kambi Doha na Abu Dhabi itacheza mchezo mmoja wa kirafiki dhidi ya Mali Juni 16. Senegal itakayoweka kambi Hispania itacheza mechi mbili dhidi ya DR Congo na Nigeria.

Wakati timu hizo tatu zimeanika mikakati yao, Kocha wa Taifa Stars, Emmanuel Amunike na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wamesema wataweka hadharani mipango yao Mei Mosi, mwaka huu.

Kauli ya Amunike

Akizungumza Dar es Salaam jana, Amunike alisema anazifuatilia kwa karibu Kenya, Algeria, Senegal na ana taarifa kuhusu maandalizi yao ya kujiandaa na fainali hizo.

“Tumefuzu Afcon tunajua haya mashindano ni magumu yanatakiwa maandalizi ya mapema, tutacheza michezo ya kirafiki na timu ambazo zimetuzidi ili kujiweka sawa kabla ya fainali,” alisema Amunike.

Hata hivyo, Amunike alisema hawezi kuzitaja timu hizo kwa kuwa bado mazungumzo baina ya nchi hizo yanaendelea.

TFF yalonga

Akizungumza Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa TFF, Wilfred Kidao alisema Mei Mosi wataweka hadharani mipango ya maandalizi ya Taifa Stars kuhusu ushiriki wake wa fainali hizo. “Tumeona wenzetu wameweka wazi mipango yao, sisi Mei Mosi tutatangaza kila kitu ikiwamo wapi tutaweka kambi na timu gani tutacheza nazo mechi za kirafiki,”alisema Kidao.

Wadau

Mchezaji wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Sekilojo Chambua alisema Amunike anatakiwa kuanza maandalizi mapema ya kujiandaa na fainali hizo.

“Imebaki mwezi mmoja kabla ya kuanza fainali za Afcon, hivyo ni wakati wa kupanga mikakati thabiti kulingana na umuhimu wa mashindano yenyewe,”alisema Chambua.

Kocha wa zamani wa Yanga, Kennedy Mwaisabula alisema huenda TFF imeshindwa kuiweka kambini Taifa Stars mapema kwa kuwa ligi nchini zinaendelea na wachezaji wapo katika kuzipigania klabu zao.

“Kenya, Senegal na Algeria zimetangaza mikakati yao lakini si kwamba zimeanza kambi muda bado upo,” alisema.