Astaafu michezo akiwa juu ya Mlima Kilimanjaro

AFP. Mchezaji wa zamani wa Baltimore Ravens, Haloti Ngata ametangaza kustaafu Ligi ya Taifa ya Mpira wa Miguu wa Kimarekani (NFL), akituma ujumbe kutoka kileleni mwa Mlima Kilimanjaro, baada ya kucheza kwa misimu 13.

“Nastaafu kucheza NFL nikiwa kileleni,” Ngata, 35, alisema katika ujumbe wake aliouweka katika mtandao wa Instagram ukiambatana na picha yake akiwa juu ya Mlima Kilimanjaro.

“Ni mtu tu aliyesimama kileleni mwa dunia akiwa na moyo uliojaa shukrani. Nakushukuru Mungu kwa kuniwezesha kucheza mchezo naoupenda kwa miaka 13 isiyosahaulika.

Nastaafu.”

Mchezaji huyo alitumia msimu wa mwaka 2018 akiwa na Philadelphia Eagles akitokea Detroit Lions ambako alicheza misimu mitatu.

Lakini atakumbukwa kutokana na uchezaji wake akiwa Ravens, ambako alicheza kwa karibu miaka kumi baada ya kusajiliwa kutoka chuoni mwaka 2006.

Akiwa Baltimore alikuwa sehemu ya ngome iliyokuwa inaogopewa.

Ngata, ambaye ana asili ya Tongan, alikulia Utah na pia aling’ara wakati akicheza raga ujanani, akifanya vizuri na timu ya shule ya Highland ya Salt Lake City.

Ukiwa na urefu wa mita 5,895, Mlima Kilimanjaro ni mrefu kuliko yote barani Afrika na wa pili duniani.

Hii si mara ya kwanza kwa wanamichezo na wasanii nyota duniani kupanda mlima huo mrefu na pengine kufanya kitu cha ajabu.

Mwaka juzi, wanasoka wa kike kutoka nchi 20 tofauti duniani walifanikiwa kupanda mlima huo na baadaye kushuka hadi urefu wa futi 18,799 kucheza mechi ya dakika 90 ya kwanza kuchezwa katika urefu huo kutoka usawa wa bahari.

Wanasoka hao wanawake waliamua kucheza mechi hiyo ikiwa ni katika harakati zao za kutaka haki sawa.

Mwaka 2009, mcheza sinema na mwimbaji kutoka Wales, Noel Sullivan, alipanda mlima huo, ikiwa ni kumbukumbu ya kaka na dada yake waliofariki wakati wakiwa wadogo.

Msanii mwingine, Cheryl Cole, alipanda mlima huo mwaka 2009, akiwa na watu wengine wanane maarufu duniani (akiwemo DJ wa Radio One, Chris Moyles, Gary Barlow na Alesha Dixon).

Pia mwaka 2010, mcheza tenis nyota wa zamani, Martina Navratilova alijaribu kupanda, lakini akaishia umbali wa mita 4,000 baada ya kuugua.