Atiki: Safari yangu kwenda kucheza NBA iko hivi

Mchezaji kikapu wa Tanzania, Atiki Ally amesema ameanza kutengeneza msingi utakaomuwezesha kucheza Ligi maarufu ya kikapu duniani ya NBA.

Amesema amebakisha hatua moja kukaribia kucheza kwenye ligi hiyo ambayo inasifika kwa kuwalipa fedha nyingi wachezaji wake.

Atiki ambaye anasoma nchini Canada ambako alipata ofa ya masomo ya ‘high school’ hivi karibuni alichaguliwa katika kikosi cha nyota watano bora (All Stars) wa mashindano ya vyuo nchini humo.

Baada ya mashindano hayo, Mtanzania huyo chipukizi alitajwa kuwa miongoni mwa nyota wa kikosi bora cha mashindano hayo, hatua ambayo Atiki anasema imemuongezea morali ya kupambana zaidi.

Akizungumza na gazeti hili kwa simu kutoka Canada, Atiki alisema anachokifikiria kwa sasa ni kupata chuo atakapohitimu kidato cha sita mwakani.

“Nikifanikiwa kupata chuo na kucheza ‘division one’ itakuwa ni hatua moja kubwa kwangu katika kutimiza ndoto yangu kucheza NBA,” alisema mchezaji huyo.

Alisema tangu ametua Canada miaka miwili iliyopita amekuwa katika kiwango kizuri huku akipata ushirikiano wa wachezaji na viongozi wake wa timu ya shule ya TVDSB.

“Mafanikio ninayopitia ni ushirikiano ninaopata, sitobweteka, nitapambana kuhakikisha napata nafasi ya kucheza NBA ambayo

ili ucheze lazima utokee ‘college’.”

Kocha wa Atiki nchini, Bahati Mgunda alisema mafanikio ya mchezaji huyo ni faraja kwa Tanzania.

“Anapaswa sasa kupambana ili kucheza division one, akifanikiwa huko kwenda NBA itakuwa ni rahisi kwake,” alisema Mgunda.

Alisema kwa namna anavyomfahamu Atiki, hana shaka na nafasi yake ya kupata chuo.

“Akifanikiwa kupata chuo hiyo ni nafasi ya mwisho ya kuonekana katika Ligi ya NBA, kwani nyota wa NBA lazima watokee huko,” alisema.