Bigirimana, Balinya wafunika Yanga SC

Khatimu Naheka, Mwananchi

Morogoro. Kocha Msaidizi wa Yanga, Noel Mwandila amesema kipimo cha kwanza kwa wachezaji wapya wakiwemo wa kigeni kimeonyesha benchi la ufundi limesajili kikosi bora kwa mashindano ya msimu ujao.

Yanga imesajili wachezaji wapya 13 kati ya saba wa kigeni ambao ni Juma Balinya, Issa Bigirimana, Patrick Sobomana, Sadney Urikhob, Lamine Moro, Mustapha Selemani na Farouk Shikalo ambaye bado hajaripoti.

Kundi hilo la wageni lina wapya wazawa AbdulAziz Makame, Muharami Issa, Mapinduzi Balama, Ally Ally, Ally Sonso na Metacha Mnata.

Akizungumza mjini hapa jana, Mwandila anayesimamia kambi akimsubiri Mwinyi Zahera, alisema mpaka sasa hajaona kasoro katika ubora wa wachezaji wapya.

Alisema kipimo cha kwanza kilikuwa mazoezi ya utimamu wa mwili ambapo wote wamefanikiwa na anasubiri Sadney aliyeanza mazoezi jana na Shikalo ambaye bado hajajiunga na timu hiyo.

“Mwanzo unakuwa mgumu, lakini hawa wapya wameonyesha uwezo mzuri, tulikuwa tunafanya mazoezi ya fiziki tangu tumefika kambini na mpaka sasa sijaona tatizo, wamefanya vyema,” alisema Mwandila.

Hata hivyo, alisema anaendelea kuwasuka wachezaji hao kuwa katika ubora ambao benchi la ufundi linahitaji kabla ya mashindano.

“Mchezo wa kwanza tumecheza ndiyo, lakini ule ulikuwa ni wa kipimo cha kuingia kwa mazoezi ya fiziki na hata pumzi, wako sawa, walikuwa wanashambulia wote na kurudi kukaba.”

Mwandila alisema, “kipimo hakikuwa ushindi wa mabao kumi, hapana, tulitaka kujua jinsi wanavyojituma katika kukaba na kushambulia.”

Yanga inaendelea na mazoezi mjini Morogoro ili kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara pamoja na Ligi ya Mabingwa Afrika.